Friday May 24, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Kada wa CCM, Farijala wafungwa miaka mitatu

25th July 2012
Print
Comments
Wafanyabiashara na ndugu wawili, Rajabu Maranda na Farijala Hussein

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam imewahukumu kwenda jela miaka 18 wafanyabiashara na ndugu wawili, Rajabu Maranda na Farijala Hussein baada ya kupatikana na hatia ya makosa sita kati ya saba waliyokuwa wanakabiliwa nayo ikiwemo kujipatia Sh bilioni 2.2 za Akaunti ya malipo ya Madeni ya Nje (Epa) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Hata hivyo, watatumikia miaka mitatu jela ambayo itakwenda sambamba pamoja na kifungo cha awali cha miaka mitano kutokana na kifungo cha miaka mitatu kwa kila kosa ambayo ni kula njama, kughushi nyaraka, kuwasilisha hati bandi na kujipatia Sh. 2,266,049,041.25.

Jopo la mahakimu  lililosikiliza kesi hiyo lilikuwa na hukumu mbili tofauti ya kwanza iliandaliwa na Mwenyekiti wake, Hakimu Fatuma Masengi ambaye ni Jaji wa Mahakama Kuu aliyepewa kibali na Jaji Mkuu Tanzania kusikiliza kesi hiyo ambaye aliona washtakiwa hao hawana hatia.

Hukumu nyingine ni ambayo imetumika na mahakama imeandaliwa na mahakimu wawili, Projestus Kahyoza na Katalina Revocat ambayo iliwatia washtakiwa hatiani katika makosa sita kati ya saba waliyoshtakiwa.

Akisoma hukumu, Hakimu Kahyoza alisema baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi saba wa upande wa mashtaka mahakama bila kuacha shaka imeona washtakiwa hao wana hatia kwenye makosa sita kati ya saba.

Alisema upande wa mashtaka umeweza kuthitisha shtaka la kula njama kwa kuwa katika maelezo ya onyo ya mshtakiwa Hussein ambayo yalipokelewa kama kielelezo na mahakama hiyo, yanaeleza kuwa alipewa maelekezo na ndugu yake Maranda kuhusu kuandaa nyaraka za kughushi jina la kampuni pamoja na mahali ambapo ofisi ya kampuni hiyo itakuwepo.

Aliendelea kusoma: “Katika ushahidi ulitolewa na Jamhuri hapa mahakamani hakuna ubishi kama washtakiwa walighushi nyaraka za kusajili jina la kampuni kutumia majina ya Paul Tobias na Fundi Kitunga, mahakama hii inaamini shtaka hili kweli washtakiwa walighushi nyaraka hizo.”

Akizungumzia shtaka la kuwasilisha nyaraka bandia, Hakimu Kahyoza alisema washtakiwa waliwasilisha nyaraka hizo wakati huo (United Bank of Afrika (UBA) ambapo walifungua akaunti ya pamoja.

Alisema kwa kutumia majina ya uongo (Paul na Fundi) mahakama inaamini washtakiwa walighushi hati ya kuhamisha deni wakionyesha ni wakala kutoka Kampuni ya   B.Graciel ya Ujerumani kwenda Kampuni ya Money Planers & Consultant ya Tanzania.

Alisema mahakama inaamini washtakiwa waliwasilisha BoT hati za kughushi kwa ajili ya maombi ya Sh. bilioni 2.2 ambazo walifanikiwa kuhamishiwa kupitia akaunti yao iliyokuwa benki ya UBA. Aliongeza kuwa:

"Mahakama inawaona washtakiwa hao hawana hatia kwenye shtaka la sita la wizi ambalo hakuna shahidi wa upande wa Jamhuri aliyethibitisha kama washtakiwa waliibia BoT.”

Alifafanua kwamba kutokana na maelezo yote hayo hakuna ubishi kwamba washtakiwa walijipatia fedha kwa njia ya udanganyifu baada ya kula njama, kughushi nyaraka na kuwasilisha hati bandia BoT.

Kwa upande wa Hakimu Masengi alisema katika hukumu yake ambayo itakuwa kumbukumbu ya mahakama, ameona ushahidi uliotolewa na washtakiwa hauna nguvu ya kuwatia hatiani na kwamba jukumu la kuthibitisha kesi ni la Jamhuri.

Alisema katika kesi hiyo BoT haijafika mahakamani hapo kueleza au kulalamika kama waliibiwa fedha hizo na hata ile kampuni ya B.Graciel ya Ujerumani hawajalalamika kuibiwa fedha hizo na washtakiwa.

Hakimu Masengi alisema Wakala wa Majina ya Biashara (Brela) hawajalalamika kupokea nyaraka zilizoghushiwa na washtakiwa mahakamani hapo na kwamba ushahidi huo wa Jamhuri unaonyesha ni jinsi gani wameshindwa kuondoa mashaka mbele ya mahakama hiyo.

Hakimu Revovat alisoma hukumu hiyo kwamba washtakiwa wataanza kutumikia kiifungo hicho kuanzia jana sambamba na kifungo cha awali.

Katika kesi hiyo,washtakiwa wanadaiwa kuwa Machi 20 na Desemba 25, mwaka 2005 washitakiwa walijipatia ingizo la Sh. 2,266,049,041.25 wakidai kwamba Kampuni ya B.Graciel ya Ujerumani imehamishiwa deni na Kampuni ya Money Planers & Consultant ya Tanzania.




 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment