Tuesday May 3, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

TFF kudhaminiwa kwa Bil.5.6bon/-

24th April 2012
Print
Comments

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limepata uhakika wa kudhaminiwa kwa Sh. Bilioni 5.5 kwa mwaka, imefahamika.

Kiwango hicho kimejulikana kupitia taarifa iliyotolewa katika mkutano mkuu wa shirikisho hilo uliofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam .

Taarifa iliyotolewa jana na Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura imeonyesha kwamba TFF inatarajia kukusanya jumla ya Sh. Bilioni 7.5 kwa mwaka, huku asilimia 74 ya mapato hayo (Sh. Bilioni 5.5) ikitokana na fungu watakalopata kutoka kwa mdhamini. 

Hata hivyo, Wambura hakutaja jina rasmi la mdhamini wala mchanganuo wa mapato hayo. 
Taarifa hiyo ilieleza zaidi kuwa TFF inatarajia kutumia Sh. bilioni 7.2 kwa mwaka.

Wambura alieleza kwamba vyanzo vingine vya mapato ya TFF ni viingilio vya uwanjani vinavyotarajiwa kuchangia kwa asilimia 22 na vyanzo vingine kama haki za matangazo ya televisheni na ada za ushiriki wa timu katika mashindano mbalimbali.

Alieleza zaidi kwamba TFF inatarajia kupokea fedha nyingine kama misaada kutoka katika Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), ambayo hupokea kila mwaka na zaidi ikilenga kwenye maendeleo ya timu.

Wambura alisema vilevile kuwa mkutano huo mkuu umeridhia Kamati ya Ligi ya TFF kuendelea na mchakato wa kupendekeza mifumo mitatu tofauti ya chombo kitakachosimamia au kuendesha Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara.

Alisma kuwa kamati hiyo ambayo sasa inaongozwa na Wallace Karina, itatakiwa kuweka wazi faida na athari za kila mfumo uliopendekezwa na baadaye kufanya mawasilisho kwenye Kamati ya Utendaji ili kutoa baraka zake na hatimaye kuanza kutumika.

Aliontgeza kuwa wajumbe wa mkutano mkuu walielezwa na Rais wa TFF, Leodegar Tenga, kuwa lengo la kuunda chombo maalumu cha kuendesha ligi ni kuongeza ufanisi na pia kuifanya sekretarieti ya TFF kushughulikia zaidi maendeleo ya mchezo wa soka.

Pia ilielezwa kuwa uuzaji wa timu mbalimbali unatakiwa utekelezwe baada ya kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa klabu husika, ambao wanachama wake ndio watakaotoa ridhaa ya uuzwaji na kuelekeza kwamba timu ikishauzwa, inabaki katika mkoa husika.

YANGA YAJIRUDI
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga ambaye pia mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF akiwakilisha klabu za Mkoa wa Dar es Salaam, Mohamed Bhinda, aliwaomba radhi wajumbe wa Mkutano huo kwa kitendo cha wachezaji wa Klabu yao kumpiga refa Israel Nkongo wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu dhidi ya Azam iliyochezwa Machi 10 mwaka huu.

Wambura alisema kwamba Bhinda alimuomba pia Rais wa TFF (Tenga) kutoa msamaha wa adhabu ya kulipa faini iliyotolewa na Kamati ya Ligi kwa wachezaji wao wawili.

Hata hivyo, taarifa imeeleza kwamba Tenga alimshukuru Bhinda kwa ujasiri aliouonesha wa kuomba radhi mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF, lakini aliongeza kuwa kwa vile yeye ni muumini wa kanuni, na adhabu hizo zimetolewa kwa mujibu wa kanuni, kamwe hawezi kutoa msamaha na hivyo wachezaji hao walipe faini kama walivyotakiwa.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles