Thursday Jun 20, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Wenyeji wajitahidi kubakiza Kombe Kagame

23rd July 2012
Print
Comments
Maoni ya kATUNI

Michuano  ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) imefikia katika hatua ya robo fainali ambapo wenyeji Simba, Azam, Yanga na Mafunzo ni miongoni mwa timu nane zilizofikia hatua hii.

Timu mbili tu kati ya nne za wenyeji ndizo zitakazokuwa na nafasi ya kutinga nusu fainali kwani kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Shirikisho la Soka Afrika Mashariki na Kati (CE CAFA), klabu hizo zitaanza kwa kuvaana zenyewe ambapo leo, Yanga na Mafunzo zitakutana katika mechi ya pili itakayochezwa jioni ya leo huku Simba ikicheza dhidi ya Azam kesho.

Ni mechi muhimu kwa timu hizi ambazo zilipata fursa ya kuwa wawakilishi katika michuano hiyo ya juu kuliko yote kwa ngazi ya klabu Afrika Mashariki na Kati baada ya Simba (Bara) na Mafunzo (Zanzibar) kuwa vinara wa ligi kuu zao, Azam iliyoshika nafasi ya pili kunufaika na uenyeji wa Tanzania Bara katika michuano hiyo na Yanga kupata tiketi ya moja kwa moja kwa vile ndio mabingwa watetezi.

Sisi tunawatakia kheri wawakilishi hawa ili waonyeshe soka safi katika hatua ya robo fainali na mbili za mwisho zikitarajiwa kufanya vizuri zaidi katika hatua itakayofuata.

Tunaamini kwamba hadi kufikia sasa, Simba, Yanga, Mafunzo na Azam wameshajiandaa vya kutosha kwa mechi za leo na kesho.

Ni matumaini yetu vilevile kuwa wachezaji wa timu zote wanajua kuwa wakati wakishuka dimbani, watatakiwa kupeperusha vyema bendera za Tanzania na Zanzibar kwa kucheza soka la kuelewana, wakipeana pasi safi na kujitengenezea nafasi nzuri za kufunga.

Kamwe hatutarajii kuona soka lisilokuwa na mvuto pindi timu za wenyeji zitakapokutana. Na tunajua kuwa wachezaji wa timu zote wanatambua umuhimu wa kujituma kwa uwezo wao wote uwanjani ili hatimaye kuwaondolea Watanzania machungu ya kile walichokikosa katika michuano mbalimbali iliyopita ya ngazi ya klabu barani Afrika.

Lakini, wakati walimu wa timu hizi wakiendelea kuwapa wachezaji mbinu mwafaka za kuibuka na ushindi kuanzia leo na pengine hadi fainali, sisi tunaona iko haja ya kukumbushia baadhi ya mambo.

Kwanza, wachezaji wa timu zote wajue kuwa wanacheza kwenye ardhi ya nyumbani. Hii inamaanisha kuwa kisaikolojia, hawatakuwa na presha kubwa kama ilivyo kwa wageni.

Watakuwa 11 uwanjani kukabiliana na idadi ya wachezaji kama hao kutoka kwa wapinzani wao. Mamia ya mashabiki watakaojaa uwanjani watajigawa katika kuwashangilia hata leo na kesho wakati watakapovaana wenyeji tupu kwani imeshazoeleka kuwa wapinzani wa Yanga katika kila mechi huungwa mkono na mashabiki wa Simba; na pia, timu inayocheza dhidi ya Simba huungwa mkono na mashabiki wa Yanga.

Hivyo, changamoto pekee kwa kila timu ni kucheza soka zuri, lisilokuwa la kubutua hovyo ili kujihakikishia mashabiki wengi. Ni wazi kwamba kwa kufanya hivyo, Watanzania watafarijika na kiwango bora kitakachoonyeshwa na timu zao na kisha wote kuwa kitu kimoja katika kuiunga mkono yoyote kati ya nne za wenyeji itakayosonga mbele na kukutana na timu kutoka nje ya Tanzania.

Simba na Azam zilizomaliza kileleni katika ligi kuu ya Bara zilifanya kazi ya ziada kupata nafasi ya kuliwakilisha taifa katika michuano inayoendelea, sawa na Mafunzo waliotwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Zanzibar msimu uliomalizika na Yanga ambao wanashiriki kutetea taji lao.

Angalizo kwa wachezaji wa timu hizi za wenyeji ni kwamba watakapokuwa uwanjani, wanapaswa kuongozwa na kanuni moja maarufu zaidi ya soka, ya ‘kosa moja goli moja.’

Washambuliaji wa timu hizi wanapaswa kufanya kila wawezalo katika kuzitumia vyema nafasi watakazopata kwa kufunga magoli ya kutosha, huku walinzi wa timu hizi wakiepuka pia kufanya makosa ya kizembe.

Kila la kheri wenyeji. Kila la kheri Simba, Mafunzo, Azam na mabingwa watetezi, Yanga.

 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment