


.jpg)
Siku chache baada ya bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kukwama kwa kukosekana kwa nusu ya wabunge bungeni, Spika wa Bunge, Anne Makinda, amesema orodha ya kujisajili itapita mara mbili kwa siku.
Kwa mujibu wa kanuni za kudumu za Bunge, ili kufanya maamuzi ya hoja, idadi ya wabunge inatakiwa kuwa isiyopungua nusu ya jumla yao.
Hata hivyo, Jumamosi wakati idadi ya wabunge walipokaa kama kamati kwa ajili ya kupitisha bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula, na Ushirika hakufika 176 na hivyo Naibu Spika, Job Ndugai kulazimika kuahirisha Bunge hadi jana ilipopitishwa.
Makinda aliyasema hayo jana muda mfupi kabla ya kuahirishwa kipindi cha asubuhi, hali ambayo inatafsiriwa inalenga kudhibiti wabunge watoro.
“Sasa sisi tutaanza kuji-register(kujiorodhesha), mchana na jioni, nikisema hivyo mnajua wenyewe maana yake,” alisema Makinda.
Hata hivyo, suala la baadhi ya wabunge kutofuatilia kwa makini mijadala ya Bunge, kulianza kuonekana mara tu baada ya Kambi ya Upinzani Bungeni kumaliza kusoma maoni yake kuhusu makadirio ya matumizi na mapato ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.
Hali hiyo ilitokana na Spika Makinda kuruhusu mchangiaji wa kwanza wa hotuba hiyo, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mchungaji Getruda Rwakatare, ambapo baadhi ya wabunge walianza kunong’ona kuwa muda umekwisha.
Baada ya Spika Makinda kuisikia minong’ono hiyo, “inaashiria kuwa hamkuwepo bungeni.”
Hata hivyo, hakuendelea kufafanua na kumruhusu Rwakatare kuanza kuchangia hotuba hiyo.
Ijumaa wiki hii, mara baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, kuomba kutenguliwa kwa kanuni, Ndugai alitangaza ratiba mpya ya kuanza na kumaliza vikao ili kuwapa nafasi wabunge wa dini ya Kiislamu kupata nafasi ya kushiriki kikamilifu katika Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Katika ratiba hiyo wabunge wataanza vikao saa 3.00 asubuhi hadi saa 7.15 badala ya saa 7.00 mchana na kisha kurejea tena saa 10.00 jioni badala ya saa 11.00 jioni na kutoka saa 12.00 badala ya saa 1.45 jioni.