Wednesday Jun 19, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Gazeti la MwanaHalisi lafungiwa

31st July 2012
Print
Comments
Mhariri Mtendaji wa gazeti la MwanaHalisi, Saed Kubenea

Serikali imelifungia kwa muda usiojulikana gazeti la MwanaHalisi kwa melezo kwamba limekuwa na mwenendo wa kuandika habari na makala za uchochezi.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Fabian Rugaimukamu, alisema Serikali imelifungia gazeti hilo kuanzia jana.

Aidha, Rugaimukamu alisema katika matoleo ya hivi karibuni, gazeti la MwanaHalisi toleo namba 302 la Julai 11 hadi 18 na  toleo namba 303 la Julai 18 hadi 24, na toleo namba 304 la Julai 25 hadi Agosti Mosi, mwaka huu, pamoja na matoleo yaliyotangulia, yamekuwa yakichapisha habari na makala zenye kueneza na kujenga hofu kwa jamii.

Alisema Mhariri wa gazeti hilo, aliitwa na kuonywa mara nyingi, lakini alikataa kukiri kuwa maudhui ya makala zake hazina tija kwa jamii na pia hazifuati weledi na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari.

“Mhariri huyu katika utetezi wake amekuwa akinukuu kifungu cha 18 cha Katiba ya nchi ambacho kinatoa uhuru wa kutoa maoni na kwa makusudi kutonukuu kifungu cha 30 cha katiba hiyo kinachoweka ukomo wa wa uhuru,” alisema Rugaimukamu.

Alisema Serikali imechukua uamuzi huo kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, kifungu (25) (i), kwa mujibu wa Tangazo la Serikali namba 258 na kuchapishwa na Gazeti la Serikali na kutolewa jijini Dar es Salaam Julai 27, mwaka huu.

Aidha, Serikali imewataka wamiliki, wahariri na wanahabari kuzingatia sheria, uzalendo, weledi na maadili ya taaluma ya waandishi wa habari katika kutekeleza wajibu wa kuhabarisha, kuelimisha na kutoa burudani kwa wananchi.

“Kama ilivyoelezwa bungeni wakati wa kuwasilisha Bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo hivi karibuni, waandishi na watangazaji wa habari wanatakiwa kuhakikisha habari wanazoziandika na vipindi wanavyoviandaa vinazingatia taaluma na kuweka mbele maslahi ya Taifa,” alisema Rugaimukamu.

Alisema kuanzia sasa Serikali haitasita kuchukua hatua dhidi ya vyombo vya habari ambavyo kwa makusudi vitatoa taarifa za uchochezi na kuhatarisha amani na utulivu wa nchi.

Kwa upande wake, Mhariri Mtendaji wa gazeti hilo, Saed Kubenea, alisema kwamba amesikitishwa na kitendo cha kufungiwa kwa gazeti lake kwa kuwa hakupewa na nafasi ya kusikikilizwa.

“Kama gazeti la MwanaHalisi lilikuwa linatuhumiwa kuandika habari za uchochezi, ni mhimili upi ambao ulipaswa hasa kusema kwamba linaandika habari za uchochezi kati serikali na mahakama?,” Alihoji Kubenea na kuongeza kuwa atatoa taarifa rasmi leo.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment