Tuesday May 3, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

CUF chataka utaratibu wa stakabadhi ghalani ufutwe

20th April 2012
Print
Comments
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu wanachama wa chama hicho mkoani Lindi kutolipwa fedha za korosho. (PICHA: OMAR FUNGO)

Chama Cha Wananchi (CUF), kimeitaka serikali kuachana na mpango wa stakabadhi ghalani, kwa  madai umeshindwa kuleta tija kwa wakulima, na badala yake imekuwa chanzo cha migogoro na matatizo kwa wakulima.

Aidha, chama hicho kimemtaka Rais Jakaya Kikwete kumwajibisha Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba, Hasna Mwilima, kwa kushindwa kuwajibika.

Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, alitoa wito huo wakati  akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, kuhusu vurugu zilizotokea hivi karibuni wilayani Tandahimba, baada ya wananchi kuandamana ili kuishinikiza serikali iwalipe madai yao ya malipo ya korosho.

“CUF ililazimika kuandaa maandamano ya amani yaliyoelekea kwa Mkuu wa wilaya ili kuishinikiza serikali iwalipe wakulima malipo yao, lakini mkuu wa wilaya hakutoa majibu mazuri akisema  yeye hahusiki” alisema Lipumba.

Prof Lipumba, alisema jambo hilo ndilo lililowafanya wananchi kuamua kuweka vizuizi kwenye barabara ya kwenda Mtwara ili kuishinikiza serikali iwalipe, kwani huu ni wakati wa kuweka mbolea ya salfa kwenye mikorosho yao.

“Wakulima walilipwa Sh. 850 na walielezwa kuwa watalipwa fedha nyingine Sh. 350 kwa kilo, lakini hadi leo (jana)  imekuwa ni kitendawili, ni vizuri serikali ikakiri kosa na kutafuta njia muafaka kwa kuwaruhusu wafanyabiashara wenye uwezo wanunue korosho kulingana na bei ya soko la dunia” alisema.

Akizungumzia tukio la juzi, Profesa Lipumba, alisema ilitolewa taarifa kuwa kuna moto kwenye Ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Tandahimba ambayo ipo karibu na soko, ambapo wananchi walijitokeza na kwenda kutoa msaada wa kuuzima moto huo.

Alisema lakini badala yake wananchi hao wakaanza kupigwa virungu na polisi, huku moto ukiendelea kuwaka na kuteketeza vibanda vya wafanyabiashara na hasa vya wanachama wa CUF na cha kushangaza kibanda cha OCD hakikuungua hata kidogo, jambo lililoleta mtazamo tofauti.

Aidha CUF kimetaka uchunguzi wa kina ufanyike na wale wote watakaobainika kuhusika wachukuliwe hatua.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles