Saturday May 18, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Mawaziri wa JK walivyosulubiwa

22nd April 2012
Print
Comments
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda

Hasira za wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) zilionekana wakati wa kujadili na kufikia uamuzi wa kuwawajibisha mawaziri wanaotuhumiwa kuihujumu serikali juzi.

Kwenye ukumbi wa Pius Msekwa uliopo ndani ya eneo la Bunge mjini Dodoma, wabunge hao walikuwa na ujumbe mmoja, kung’atuka kwa mawaziri nane wa serikali ya Rais Jakaya Kikwete.

Vyanzo tofauti vya NIPASHE Jumapili kutoka ndani ya kikao hicho kinachoelezwa kufanyika kwa muda usiozidi saa moja, wabunge hao walikusanyika wakati ambapo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alikuwa upande mwingine akiwahoji mawaziri watuhumiwa.

“Wabunge wote walionyesha kuchukizwa na utendaji wa mawaziri waliotuhumiwa na hapakuwa na hali ya furaha ukumbini,” kilieleza chanzo chetu.

Hata hivyo, Pinda ambaye pia ni Mwenyekiti wa wabunge kupitia CCM, aliwasili ukumbini baada ya kuwahoji ‘watuhumiwa’ ambapo alitoa taarifa kwa wabunge hao.

“Wakati akiingia ukumbini Pinda naye hakuonekana kuwa mwenye furaha, lakini alikuwa imara katika kuzungumza na kutoa taarifa,” alisema mmoja wa wabunge ambaye kama walivyokuwa wenzake, hakutaka kutajwa jina lake gazetini.

Alisema Pinda aliwajulisha wabunge kwamba katika kikao chake na mawaziri watuhumiwa, aliwataka wajichunguze, wajitafakari na kuchukua hatua.

“Pinda alitujulisha kwamba aliwaambia kujiangalia kuwa jamii inawachukuliaje, wabunge wanawaonaje, mamlaka iliyowateua inawaonaje, Mungu anawaonaje na wao binafsi wanajionaje katika utendaji wako wa kazi,” kilieleza chanzo hicho.

Wakati Pinda akitoa taarifa hiyo, inaelezwa kuwa mawaziri watuhumiwa walikuwa wamenywea na kwamba hawakupata mwanya wa kujibu hoja zilizotolewa.

"Hawakuweza kujibu lolote katika kikao hicho, hivi niambie wewe utuhumiwe na wabunge wote, utajibu nini hapo…ukweli ni kwamba walikuwa katika hali ya majonzi," alisema mbunge huyo.

Pia wakati wabunge hao wakichangia huku takribani wote wakishinikiza wajiuzulu, mbunge mmoja kutoka jimbo la visiwani Zanzibar alijitokeza kuwatetea mawaziri hao.

“Lakini ilikuwa kama amejipalia mkaa kwa maana alishambuliwa sana, ikabidi abaki kimya,” kilieleza chanzo chetu kingine.

Aidha, alisema kuna mbunge mmoja ambaye anatokea Zanzibar alijaribu kutaka kuwatetea mawaziri hao na kujikuta katika wakati mgumu kwani wabunge walianza kumshambulia na kutamani hata kumtukana.

Kwa upande wake, mbunge mwingine wa CCM ambaye alikuwa katika kikao hicho, alisema taarifa dhidi ya mawaziri hao ambao wametajwa katika vyombo vya habari ni kweli wameandika barua ya kujiuzulu.

Alisema wabunge waliokuwa katika kikao hicho walifurahia taarifa za kuwa mawaziri hao wameandika barua kujiuzulu.

Yupo Waziri mmoja miongoni mwao anayetuhumiwa kwa ufisadi ikiwemo ununuzi wa nyumba iliyogharimu Dola 700,000 za Marekani huku `akimwaga’ misaada yenye thamani ya mamilioni ya fedha jimboni kwake.

“Waziri kama huyo anapata wapi hela zote hizo kwa kipindi cha muda mfupi, binafsi huwa ninatafuta hata Shilingi milioni tano tu kwa shughuli za maendeleo ninazikosa,” alisema.

Alisema kwa sasa hali ilivyo Waziri Mkuu hawezi kujiuzulu kwa kuwa tayari mawaziri waliotajwa wameshaandika barua za kutaka kujiuzulu.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa pamoja na azma ya kujizulu kwa mawaziri hao, kikao cha wabunge wa CCM kilitoa maazimio kadhaa kwa kila mtuhumiwa.

Maazimio hayo yamo katika mfumo unaowataja mawaziri kwa majina na vyeo vyao, tuhuma zinazowakabili na hatua zinazostahili kuchukuliwa.

CCM YAWAUNGA MKONO WABUNGE WAKE

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa upande wake kimeunga mkono na kuwapongeza wabunge wake kwa hatua ya kuwakosoa mawaziri wa serikali ya chama hicho.

Katibu wa Itikadi na Uenenzi wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Nape Nnauye, ametoa taarifa hiyo kwenye mtandao wa kijamii wa kielektroniki na kusema lazima yafanyike maamuzi magumu na akawaomba wananchi kuunga mkono na kukiamini chama hicho.

Alisema binafsi alishtushwa na taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), Kamati ya Kamati ya Hesabu Mashirika ya Umma (POAC), Kamati ya Hesabu ya Serikali (PAC) na ile ya Serikali za Mitaa, zikionyesha kuna udhaifu wa utendaji na kusababisha kuwepo kwa matumizi mabaya ya fedha za umma.

Alisema imeonyesha kuwepo ufisadi na matumizi ya hovyo katika mamlaka, taasisi na halmashauri mbalimbali, kitu ambacho hakikubaliki na kuwataka wote waliohusika wafikishwe katika vyombo vya sheria.

“Kuibuliwa kwa ufisadi huo imemfanya kujiuliza mambo mengi lakini kutokana na kuwa mwana-CCM anayeamini imani ya chama chake pamoja na kufuata kikamilifua kiapo cha chama chake hatakuwa na hofu kwa kusema ukweli na kukemea vitendo vya kutoa na kupokea rushwa,” alisema.

MAIGE ALIPULIWA

Kamati ndogo ya Maliasili na Utalii, imemshutumu Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige kwa madai ya kugawa vitalu vya uwindaji kiholela na imemshauri ajiuzulu.

Kamati hiyo ndogo iliundwa kuchunguza kashfa ya kusafirisha wanyama hai kama Twiga nje ya nchi na ilitarajia kutoa ripoti yake bungeni kesho.

Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Peter Msigwa, alisema uchunguzi walioufanya ulibaini kuwa kampuni tatu zisizokuwa na sifa zilipewa vitalu kinyume cha sheria.

Alisema kuna makampuni sita yalipewa vitalu ingawa hayajawahi kuwasilisha maombi ya kutaka vitalu hivyo. Alisema kamati ndogo ya maliasili na utalii imependekeza serikali imwajibishe Waziri Maige kwa kashfa hiyo.

Alisema kampuni 19 zipokonywe vitalu vya utalii kwa kuwa zilipewa bila kuwa na sifa stahili za kufanya shughuli hiyo.

“Hii ni Wizara nyeti, sekta hii ya maliasili na utalii inachangia asilimia 17 ya pato la taifa hivyo kamati inashauri iangaliwe vizuri na watu wasifanye mambo kiholela,” alisema.

Alisema baadhi ya watu walimshutumu kuwa alihongwa safari ya kwenda Las Vegas Marekani jambo ambalo alilikanusha vikali.

“Siwezi kuhongwa safari, mimi nimesafiri sana hata kabla ya kuwa Mbunge, nimetembea sana duniani hii kashfa ya kuhongwa safari imeniudhi sana,” alisema Msigwa.

Alisema ni kweli alikwenda Las Vegas Marekani lakini safari hiyo ilitokana na yeye (Msigwa), kupendekezwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda.

Alisema safari hiyo ilikuwa ikihusu kongamano kubwa la kimataifa lililokuwa likihusu masuala ya maliasili na utalii na alikwenda kwa kuwa alikuwa mdau wa sekta hiyo.

“Spika aliniteua nikaenda ingawa gharama zote zililipwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, lakini kuna watu walisema kuwa nimehongwa safari na waziri ili nifiche ripoti si kweli hata kidogo,” alisema.

Habari hii imeandikwa na Beatrice Shayo, Dar es Salaam na Joseph Mwendapole, Dodoma

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment