Friday May 6, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Ma-DC wasigeuze ofisi vijiwe vya `kupiga mabomu` au dili za kimjini

13th May 2012
Print
Comments

Ni dhahiri uamuzi wa Rais Jakaya Kikwete wa kuteua wakuu wapya wa wilaya (ma-DC), ni mfululizo wa mabadiliko anayoyafanya katika serikali yake, kufuatia kukithiri kwa hali mbaya ya kiutendaji ya watu aliowateua serikalini.

Ukweli huo unathibitishwa na hatua ya Rais Kikwete ya kulifanyia mabadiliko baraza lake la mawaziri Mei 4, mwaka huu. Katika mabadiliko hayo, mawaziri sita na naibu mawaziri wawili walitupwa nje ya Baraza la Mawaziri.

Mawaziri waliotemwa katika baraza la sasa ni pamoja na Mustafa Mkulo (Fedha), Dk. Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii) na William Ngeleja (Nishati na Madini).

Mawaziri wengine walioachwa ni Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii), Dk. Cyril Chami (Viwanda na Biashara) na Omar Nundu (Uchukuzi). Naibu mawaziri waliofyekwa ni Dk. Athumani Mfutakamba (Uchukuzi) na Dk. Lucy Nkya (Afya na Ustawi wa Jamii).

Mawaziri na naibu mawaziri hao walikumbwa na mkasa huo kufuatia tuhuma mbalimbali zinazowakabili katika maeneo waliyokuwa wakiyasimamia. Tuhuma zilifichuliwa na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na kamati tatu za kudumu za Bunge.

Kamati hizo ni pamoja na ile ya Hesabu za Serikali (PAC), ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) na ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).

Kwa sababu hizo basi, yapo mambo kadhaa, ambayo hapana shaka ma-DC, hususan wale wapya walioteuliwa, yafaa kuzingatia. Lengo likiwa kuepuka yasije yakawakuta yale yaliyowakuta viongozi wenzao waliokumbana na fagio hilo.

Mosi, ma-DC wasidhani kwamba, wameteuliwa ili kwenda maofisini kudumisha Chama Cha Mapinduzi (CCM). Hii inatokana na ukweli kwamba wengi wa walioteuliwa kwa namna moja au nyingine wanajulikana hata kwa kuku na ndege kuwa ni makada wazuri wa CCM.

Pili, wasidhani kwamba, kuteuliwa kwao ni zawadi au wamelipwa fadhila kwa utumishi wao mzuri na uliotukuka kwa CCM.

Tatu, wasidhani kwamba, uamuzi wa Rais Kikwete wa kuwateua umelenga kuwapoza baadhi yao machungu. Hayo ni yale ya kuanguka katika mbio zao za kuwania ubunge, udiwani na nafasi nyingine za kichama.

Naamini kuwa uamuzi wa Rais Kikwete wa kuwateua katika nafasi hizo, umekusudia kuleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo katika wilaya walizopelekwa.

Makusudio ya Rais Kikwete ni pamoja na kutaka wakasimamie ipasavyo maendeleo ya watu, rasilimali za nchi pamoja na matumizi yake ili zitumike vizuri kwa maslahi ya wananchi.

Makusudio mengine ya Rais Kikwete ni ili waende wakasimamie kwa haki matumizi mazuri ya fedha za serikali kama zilivyokusudiwa.

Naamini kuwa wananchi wengi wanaamini pasi na tone la shaka kwamba, ma-DC walioteuliwa watakuwa wameelewa kusudio la Rais Kikwete huko wilayani walikopelekwa kwamba ni kwenda kuchapa kazi na siyo kutembea na wananchi wanatarajia kuona uchapaji kazi wao na kuwaletea mabadiliko katika maendeleo yao.

Nasema hivyo, kwa sababu ushahidi na uzoefu unaonyesha kwamba, wapo wateuliwa wengi ambao wamekuwa na tabia ya kugeuza ofisi kuwa vijiwe vya ‘kupiga mabomu’ na dili za kimjini.

Hao ni wale ambao nafasi wanazozipata huzitumia kutanguliza zaidi ubinafsi na kudhulumu umma kupitia wizi, utapeli, vitisho na ubadhirifu.

Wanatumia nyadhifa walizozipata ‘kuwachomoa’ watu, hususan wafanyabiashara. Pia kwa kutumia nyadhifa zao kujinufaisha kibinafsi rasilimali za umma na kufanya kila aina ya ufisadi.

Wanachotakiwa kukifanya ma-DC ni kwenda kudhibiti ubadhirifu katika halmashauri, kuwasukuma watendaji wazembe na wala rushwa wilayani na kuwachukulia hatua pamoja na kusimamia kwa dhati maendeleo ya wilaya zao.

Wanapaswa kutambua kuwa hivi sasa wao ni watumishi wa umma ambao wameingia kwenye wajibu wa kuhudumia wananchi na sio kula nchi.

Nawatakia kheri tupu ma-DC wote, wakiwamo waliokuwa mabosi na washauri wangu na wana taaluma wote wenzangu katika tasnia ya habari, akiwamo Muhingo Rweyemamu (Handeni, mkoani Tanga) na Ahmed Kipozi (Bagamoyo, mkoani Pwani).

Naamini uteuzi wao ulistahili kutokana na imani kubwa iliyoonyeshwa kwao na Rais Kikwete hivyo sitarajii wamwangushe.

Mwenyezi Mugu awabariki sana. Wao na familia zao awape afya njema. Watekeleze wajibu wao kwa umma kwa uaminifu na uadilifu wote. Kila siku iwe nzuri na ya kheri kwao. Amin.

 

Muhibu Said ni mwandishi wa habari wa gazeti la NIPASHE. Simu: 0717055551 au 0755925656. Baruapepe: [email protected]

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles