


.jpg)
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), limewaomba Watanzania kujihadhari na tabia ya udini inayoanza kujitokeza nchini ili kuliepusha Taifa katika machafuko ya wenyewe kwa wenyewe.
Ombi hilo limetolewa juzi na Askofu Mkuu wa KKKT, Dk. Alex Malasusa, wakati akifungua mkutano mkuu wa Sinodi ya 12, wa Kanisa hilo, Dayosisi ya kati mjini Singida, kwenye hotuba iliyotolewa kwa niaba yake na Askofu Paul Akyoo, wa Dayosisi ya Meru ya Mkoani Arusha.
Alisema kuwa, Watanzania wamekuwa wakiishi kama ndugu mmoja, kwa kudumisha amani na upendo kabla hata ya uhuru na muungano, huku kila mmoja akiabudu dini anayoona inamfaa kulingana na imani yake.
Dk. Malasusa amesema ili kuepuka machafuko yanayoweza kuikumba nchi, Watanzania wanapaswa kuachana na udini na wajifunze athari hizo kutoka kwa majirani zake na nchi nyingine zinazokabiliwa na machafuko, ikiwemo Nigeria na Somalia.
Aidha Dk. Malasusa ameiasa jamii kujitahidi katika kuhifadhi mazingira kwenye maeneo yao, ili pamoja na kunufaika na mazao yatokanayo na misitu, pia kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, yanayotishia dunia hivi sasa.
Kwa upande wake, Askofu Eliuphoo Sima wa KKKT-Dayosisi ya Kati, ambaye anamaliza kipindi cha miaka sita ya uongozi wake, alitoa wito kwa jamii kuwajibika ipasavyo kazini, kwa ajili ya kujikomboa kiuchumi na kiroho.
Alisema kuwa, mkazo na msingi mkuu wa kanisa hilo ni elimu, hivyo waumini wake wanayo kazi kubwa kuhakikishwa wanashiriki kikamilifu katika kukamilisha ujenzi wa chuo kikuu, kinachotarajiwa kuanza kazi hivi karibuni.