


Timu ya taifa ya soka ya wanawake, Twiga Stars, juzi ilibanwa mbavu na Kombaini ya vijana wa umri chini ya miaka 17 ya mkoa wa Dodoma kwa sare ya bila kufungana katika mchezo wa kirafiki uliofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani humo.
Akizungumza na gazeti hili, Meneja wa Twiga Stars, Furaha Francis, alisema kuwa katika mchezo huo kila upande ulionekana kuwa makini na kila mchezaji alifuata maelekezo ya kocha wao.
Meneja huyo alisema kuwa wakiwa Dodoma timu ilipokelewa vizuri na jana asubuhi walianza safari ya kuelekea jijini Mwanza kucheza mechi nyingine ya kirafiki na baadaye watarejea Dar es Salaam kuja kuikabili Zimbabwe Jumamosi.
Naye Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema jana kuwa Zimbabwe iliwasili nchini jana ikiwa na msafara wa watu 25.
Wambura alisema Twiga Stars inacheza mechi hiyo ya kirafiki ya kimataifa Jumamosi ili kujiandaa na mchezo wake dhidi ya Ethiopia utakayofanyika jijini Addis Ababa Mei 26 na baadaye kurejeana hapa nchini baada ya wiki mbili.
Twiga Stars iliyoko chini ya kocha Boniface Mkwasa ilianza vyema harakati za kusaka nafasi ya kushiriki fainali hizo za Afrika kwa mara ya pili baada ya kuifunga Namibia jumla ya magoli 7-2 wakati Ethiopia wao waliiondoa Misri.
Fainali hizo za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake mwaka huu zitafanyika nchini Equatorial Guinea.