Friday May 6, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Mengi atunukiwa tuzo mbili za kimataifa

30th April 2012
Print
Comments
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman (kushoto), akimkabidhi Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, tuzo ya mafanikio ya mwaka 2010-2011,inayotolewa na mashirika binafsi ya Umoja wa Mataifa, (UN-NGOs), katika hafla ya shukrani iliyoandaliwa kwa pamoja na Umoja wa Mataifa Ofisi ya Tanzania na Global 2000(2011) International.

Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, ametunukiwa tuzo ya dunia ya uongozi kutokana na mchango wake kwa jamii katika jitihada za kuondoa umaskini na kusaidia makundi mbalimbali ya wasiojiweza.

Alitunikiwa tuzo ya mafanikio ya mwaka 2010-2011, inayotolewa na mashirika binafsi ya Umoja wa Mataifa, (UN-NGOs), katika hafla ya shukrani iliyoandaliwa kwa pamoja na Umoja wa Mataifa ofisi ya Tanzania na Global 2000(2011) International. Pia alitunukiwa tuzo ya  Uongozi na Utu inayotolewa na Global 2000(2010). Mengi anakuwa mwafrika wa kwanza kutunukiwa tuzo hiyo.

Hafla hiyo iliyofanyika Jumamosi, ilihudhuriwa na watu mbalimbali mashuhuri wakiwemo, viongozi wa dini na baadhi ya mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao nchini.

Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini, Alberic Kacou, alisema Dk. Mengi amekuwa si msaada tu kwa Watanzania bali kwa watu wengi duniani na kuongeza kuwa tuzo mbalimbali alizowahi kupata kama ile ya Martin Luther King aliyopewa na Marekani ni mifano michache tu inayodhihirisha kwamba ni mtu mpenda watu na ambaye amejitoa kusaidia jamii.

Alisema kamati ya tuzo ya Nobel Laureates imemteua Dk. Mengi kuwa miongoni mwa watu saba watakaopewa tuzo ya Business for Peace ya mwaka 2012.

“Mengi amesaidia watu wengi hapa Tanzania, lakini amevuka mipaka na kwenda kusaidia hata watu wa nje ya nchi, mengi amefanya mengi na anastahili tuzo hii ya 2010 United Nation globali Leadeship,” alisema.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda Nchini (CTI), Felix Mosha, alisema licha ya kwamba tuzo hiyo amepewa Dk. Mengi, lakini imekuwa heshima kubwa kwa watanzania wote.

Alimwelezea Dk. Mengi kuwa ni mtu ambaye anatumia sehemu kubwa ya mali yake kusaidia wenye shida na wakati wote amekuwa akiwaisitizia wenye uwezo kusaidia watu wa makundi yasiyo na uwezo kama walemavu.

Naye Katibu mstaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Balozi Juma Mwapachu, alisema walikutana kwa mara ya kwanza na Mengi mwaka 1980 na akawa mshauri wake mzuri katika mambo mengi.

Alisema Dk. Mengi amekuwa mtu asiyekata tamaa na anayependa kukabiliana na changamoto yoyote anayokumbana nayo na kwamba hiyo ndiyo imemfikisha hapo alipo.

“Mengi amekuwa siku zote akitumia sehemu ya utajiri wake kusaidia wenye shida, ni mtu wa kutekeleza kile anachoamini na amefika hapo alipo kwa kujiamini na kwa kufanyakazi kwa bidii,” alisema Balozi Mwapachu.
Akielezea namna anavyomfahamu baba yake, mtoto wa kiume wa Reginald Mengi, Abdiel Mengi, alisema:

“Mzee Mengi ni baba yangu, rafiki yangu na pia ni bosi wangu, ni mjasiriamali anayejali watu wenye shida na nawashukuru sana watu wote waliomsaidia baba yangu katika mambo mengi pamoja na familia ya makampuni ya IPP,” alisema.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Dk. Mengi, alisema si watu wengi wanajua shida wanazopata watu wanaoishi katika umaskini.

Alisema watu maskini ndio wanajua shida wanazopata katika maisha yao ya umaskini. “Ajuaye kikamilifu mateso wanayopata maskini kutokana na umaskini wao ni Yule ambaye ameishi na kushuhudia maisha hayo, na ninaamini kwamba wengi wa matajiri barani Afrika ikiwemo Tanzania wamepitia maisha hayo,” alisema.

Alisema umaskini unawanyima maskini haki nyingi na hawaelewi haki zao za msingi, wananyimwa haki za kushiriki kikamilifu katika kujenga taifa na wananyimwa haki na fursa sawa katika kufaidi matunda ya maendeleo ya taifa lao.

Dk. Mengi alisema maskini hasa wanawake ambao ndio nguzo ya uchumi wa vijijini na watunzaji wa familia wanafanyakazi sana hata kuliko ambavyo walio na hali nzuri kiuchumi wanavyoweza kufikiria.

“Natoa wito kwa matajiri na wafanyabiashara kujenga utamaduni wa kuwapa na kuwagawia utajiri wao watu maskini, watu walio kwenye hali ngumu za maisha na watu wenye ulemavu, njia za kufanya hivyo ziko nyingi,” alisema Dk. Mengi.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles