Saturday Feb 6, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Rufaa ya Lyon mechi ya Azam, Mtibwa leo

2nd May 2012
Print
Comments

Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) inatarajia kukutana leo saa 8:00 mchana kujadili rufaa iliyowasilishwa kwao na klabu ya African Lyon ambayo inapinga maamuzi yaliyotolewa na Kamati ya Ligi juu ya mchezo wa Ligi Kuu ya Bara kati ya Azam na Mtibwa Sugar ambao ulivunjika hivi karibuni.

Kamati ya Ligi baada ya kupitia ripoti ya refa wa mchezo huo na kamisaa iliamua kuipa Azam ushindi wa pointi 3 na magoli 3 huku ikiamuru Mtibwa ilipe faini ya Sh. 500,000 na kunyimwa mapato ya mchezo huo na pia ikimuondoa refa, Rashid Msangi kwenye orodha ya waamuzi wa ligi hiyo.

Barua ya African Lyon ya Aprili 29 mwaka huu kwenda kwa Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi,  inasema kwamba wanapinga timu yao kucheza mechi ya ligi dhidi ya Mtibwa ambayo wao wanaamini haistahili kuendelea kuwepo kwenye ligi.

Barua hiyo iliyosainiwa na Mwenyekiti wao, Rahim Kangezi, inasema kuwa Kamati ya Ligi na Mashindano ilipindisha maamuzi yake kwa kutoa maamuzi ya kutatanisha na yasiyozingatia kanuni.

Kangezi katika barua yake ya rufaa alitaja sababu ni kuwa Kamati ya Ligi na Mashindano haikufuata kanuni namba 22 (1) inayoelezea wazi adhabu kwa timu inayovuruga mchezo na badala yake ikatumia kanuni ya 22 (3) inayozungumzia muda ambao refa atasubiri kabla ya kumaliza mechi ambao ni kati ya dakika moja hadi 15 ili kuyumbisha maamuzi.

Lyon pia wanapinga Kamati kutumia kipengele cha kanuni namba 5 na 6 na kueleza kuwa ilipaswa timu hiyo ishushwe daraja na kutekeleza kanuni hiyo ya 22.

"Kamati ilipotosha na kuyumbisha kanuni kwa maslahi binafsi," ilisema sehemu ya barua ya Lyon.

Vile vile Lyon iliwatuhumu wajumbe watano wa Kamati hiyo walioshiriki kutoa maamuzi waliangalia maslahi ya timu zao ambapo aliwataja Mwenyekiti, Wallace Karia anayetoka Mtibwa, Said Mohammed (Azam), Geofrey Nyange 'Kaburu' (Simba), Yahaya Ahmed (Mtibwa Sugar) na Damas Ndumbaro ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Simba.

Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, alisema kuwa tayari shirikisho hilo limejiandaa kuwasilisha hoja zake katika kamati hiyo.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment