Wednesday Jun 19, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Mahausigeli waandaliwe mafunzo kabla ya kuajiriwa

15th July 2012
Print
Comments

Mpenzi msomaji, utakumbuka kwamba wiki iliyopita tulizungumzia ujumbe wa msomaji wetu mmoja aliyelalamika kuwa mumewe alitimka na hausigeli kisha kumwachia watoto.

Wapo baadhi ya wasomaji wengine waliochangia maoni juu ya jambo hilo kama itakavyofuata hapa chini. Lakini pia nitakueleza msomaji wangu mbinu chafu zinazotumiwa na baadhi ya watu wanaowauza mahausigeli hao wakidai ni wazuri, waaminifu kumbe ni mradi wa aina yake. Sikia maoni haya kwanza toka kwa wasomaji;

“Hausigeli wengine wanawafundisha watoto sarakasi ya ngono, wengine wamekimbia kwao ili wasiolewe kwa lazima, wengine wamekimbia shuleni, wengine wanafanyishwa kazi za laana kama kufua nguo za ndani za mabosi wao, wengine wamebebeshwa mimba za lazima na kuwafukuza nyumbani.Ili kulipiza wanafanya vituko.

Ni vema iwekwe bayana kwamba Serikali na sheria vinataka nini. Ni vema sheria ikatamka kuwa iwepo mikataba ya ajira kwa mahausigeli. Mikataba hii isimamiwe na Serikali za Mitaa na kila ofisi ya Mtaa iwe na kumbukumbu ya hausigeli husika.

Iainishe bayana kwa hausigeli fulani ni mtoto wa mtu fulani anayefanya kazi kiutumwa kwa mshahara kidogo.

Hausigeli wengi wanasafirishwa kama vifurushi kwa maana ya kutojua wanakokwenda kufanya kazi ipi. Hakuna tofauti na mtumwa aliyetoka Ujiji kwenda Amerika ila tu kwa sasa ni mtoto mdogo kinyume na sheria ya ajira.

Na mwisho nikupongeze kwa uanaharakati wa haki sawa. Naomba uungane nani kutetea tabaka la kinyonge linalofanya malipizi ya kunyonywa, kudharauliwa na hatimaye umauti uko mbele yao kwa uasi wa lazima(By Eliah wa Njombe)”. Hivyo ndivyo anavyomaliza msomaji wetu huyu katika ujumbe 3 kupitia simu ya kiganjani.

….Mwingine anasema: Hawa mahausigeli wetu wakati mwingine wanabadilika kutokana na mazingira. Mfano, kama tunawanyanyasa katika kazi na katika posho yao(mshahara wao). Lingine ni kwamba hawa mahausigeli wamezoea ukatili kwa sababu wanatoa mimba wakiwa mikoani kwa hiyo mtu wa sampuli hii kuua kwake ni jambo dogo( naitwa Asanial Idd wa Mlola, Tanga).

Naam. Baada ya makala ile yupo mama mmoja tulisoma wote elimu ya sekondari alibainisha mbinu chafu wanayofanya baadhi ya watu na hasa kinamama ambao hukusanya wasichana wa kazi huko mikoani na kuwaleta mijini ili kuwatumia kama njia ya kujipatia kipato.

Huku akijitolea mfano, anasema kuwa aliwahi kuletewa msichana wa kazi lakini baada ya wiki mbili akasema kazi hawezi na hivyo kulazimika kumjulisha mwanamke aliyemletea kuja kumchukua.

Lakini hata hivyo mwajiri huyu akawa tayari amepata hasara kwa sababu baada ya kuletwa kwa mama huyo, mama huyu rafiki yangu alitakiwa kutoa sh.25,000 kwa ajili ya kumwagiza hausigeli huyo kutoka mikoani, jambo ambalo alizitoa.

Kumbe wasichana hao wa kazi tayari walishakusanywa toka mikoani na kuhifadhiwa kwa mama huyo anayepokea fedha za nauli. Anachofanya mama huyo ni kuwakusanya na kuwatunza huku akiwatafutia mahali pa kufanyia kazi.

Pia huwafundisha mbinu hiyo chafu kwamba wakiulizwa wametokea wapi wataje vijiji wavijuavyo huko mikoani ili wasitofautiane na mama yao huyo mlezi. Kumbe wasichana hao wengine ni wale madada poa wanaonyatia mabuzi mitaani usiku kisha mchana wanajifanya mapole.

Mama huyu rafiki yangu anasema binti yule aliyeletewa awali aliona anafanya kazi vema japo kwa usimamizi wa karibu lakini baada ya wiki akaanza kubadilika. Alikuwa na nguo mbili kuu kuu, yuko rafu ijapokuwa nywele zinaonyesha zilikuwa zikienda saluni kabla ila alijifanya rafu asigundulike.

Alidai elimu yake ni ya msingi na kwamba hajui mahali popote eneo lile la Mbezi Beach. Siku moja alifika baba mmoja dukani kwa mama huyu rafiki yangu na alipomkuta akaanza kumchangamkia. Yule baba akasema anamfahamu lakini bibie akakana kumtambua akidai kamfananisha.

Baba yule alipoondoka, binti akaulizwa anamfahamuje baba yule wakati alidai hamjui mtu pale Mbezi lakini akazidi kudai kamfananisha. Binti akaanza vituko mara afinye mtoto, mara aunguze mboga, mara ugali mbichi, ili mradi maudhi atimuliwe.

Wiki ya pili mama rafiki yangu akaona visa vinazidi akamuita mama aliyemleta aje amchukue kabla hajamwitia polisi kwa uharibifu. Yule mama kuja akajifanya kumgombeza na kumwambia lazima aendelee na kazi lakini binti akasema akilazimishwa kufanya kazi atatoroka. Ndipo mama yule akalazimika kuondoka naye na kumuomba radhi rafiki yangu.

Kumbe ule ulikuwa ni mchezo unaofanywa na baadhi ya kinamama na pia kinababa kuzungusha wafanyakazi wa majumbani kwenye familia lakini wanawarubuni baada ya muda wanatoroka au wanafukuzwa kisha kurejea tena kwa waliowaleta na kwenda kwingine.

Hapa wanachuma fedha kwani kila wanakowapeleka huwa wanadaiwa nauli ambazo hazirudishwi. Huu ni wizi wa mchana.

Na ndio maana wasichana wengi wanaoajiriwa majumbani mwa watu huwa wana historia mbovu, hivyo uchunguzi yakinifu wahitajika kabla ya kuwaajiri kama makala yangu ya awali kuhusu mahausigeli hawa ilivyojieleza. Tuwachunguze kabla ya kuwaajiri kwani wengine ni mamluki(askari wa kukodiwa)!

Suala la usafirishaji wa binadamu tumelisikia. Hata Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi uliopita aligusia jambo hilo akihusisha raia wa nje wakiwemo Ethiopita ambao waligunduliwa wamekufa porini wakisafirishwa isivyo halali kupitia nchini kwetu kuvushwa kwenda nchi za Kusini mwa Afrika.

Usafirishaji wa binadamu wa aina hii hauna tofauti na huu niliozungumzia wa watu kutoa wasichana vijijini na kuwaleta mijini kuja kuwatafutia kazi za majumbani, wengine kuwaajiri kwenye madanguro ya siri, wengine wakiyaita geto, wengine gesti bubu na kadhalika.

Je, wasichana waliopatikana kutoka maeneo hayo, watakuwa watumishi wazuri majumbani mwetu? Hawana maadili, ni wakatili, wengine kutokana na kutumikishwa kazi za suluba kabla ya kuingizwa majumbani mwetu. Tuwachunguze.

Ni wakati sasa zijitokeze asasi za kusimamia kundi hili kama wenzetu Kenya wanavyofanya kwa muda mrefu sasa. Kule zipo shule au vituo kwa ajili ya kuwapatia mafunzo ya malezi majumbani ambako baada ya kuhitimu hutafutiwa kazi.

Na huko wanakoajiriwa huwafuatilia kuhakikisha kuwa mafunzo yale yamekuwa na tija kwao na familia wanasifanyia kazi. Inawezekana hata hapa kwetu. Kama siyo asasi basi Idara ya Ustawi wa Jamii ianzishe mafunzo hayo ili wapatikane watumishi wazuri wa majumbani mwetu badala ya sasa kila mtu hujitafutia ili mradi amepata, lakini baadhi wanaacha vilio na hasara nyingi kwa wanaowaajiri.

Mpenzi msomaji, kwa leo nimechangia vya kutosha na kama nawe unalo la ziada kuhusu hili la mahausigeli, uko huru kuleta maoni kabla sijafunga pazia tuingie katika jambo lingine. Na ukiwa tayari, kuwa huru kutuma ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 774268581(usipige), au barua pepe; fwingia@gmail.com

Kumbuka kama hutapenda jina au simu yako itajwe gazetini tamka hivyo na hilo litaheshimiwa.

Wasalaam.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment