Sunday Feb 14, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Maandamano ya kumpokea Nundu yafutwa

21st May 2012
Print
Comments
Aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Omary Nundu

Jashi la Polisi Mkoa wa Tanga limezuia maandamano ya kumpokea aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Omary Nundu, yaliyokuwa yameandaliwa na wananchi wa Jiji la Tanga kwa ajili ya kumpokea mbunge wao kutokana na sababu za kiusalama.

Nundu ambaye ni Mbunge wa Tanga Mjini (CCM) ilikuwa apokelewe na wananchi katika eneo la kiwanda cha kuzalisha unga cha Pembe Flour Mill baada ya kuwasili kutoka nchini Afrika Kusini ambako alikwenda baada ya kumalizika kwa mkutano wa saba wa Bunge.
 
Mbunge huyo baada ya kutemwa katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri lililotangazwa hivi karibu na Rais Jakaya Kikwete alisafiri kwenda nje Dubai na Afrika Kusini.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Mussa Malambo, akizungumza na NIPASHE kwa simu alisema hatua hiyo imechukuliwa na jeshi hilo kutokana na taarifa za kiusalama kuwa huenda kungeweza kutokea vurugu wakati wa maandamano hayo.

“Unajua mbunge ni kiongozi kama kukitokea vurugu halafu akapata madhara itakuwa ni tatizo, kwa hiyo tumewaomba wananchi waliokuwa wameandaa maandamano hayo wayasitishe wakajipange upya maana wanaweza wakajipenyeza hata watu ambao siyo wazuri wakaleta madhara kwa mbunge,” alisema Malambo.

Malambo alisema hofu ya usalama katika maandamano hayo inatokana na kwamba walioyaomba kuyaratibu ni wananchi wa kawaida na kwamba kama yangekuwa yameratibiwa na chama isingekuwa tatizo.

Juzi akizungumza na waandishi wa habari mjini Tanga, Mwenyekiti wa maandamano hayo, Ahmedi Keya, alisema lengo la maandamano hayo ni kumfariji mbunge huyo baada ya kuondolewa kwenye uwaziri.

“Hatupingi maamuzi ya Rais wala yaliyotokea bungeni bali tunampokea kama mbunge wetu ambaye tumemchagua na kuna mambo ambayo ameahidi kwa maslahi ya Tanga sasa tusipomfariji anaweza kujisikia vibaya na asitekeleze yale aliyoyaahidi,” alisema Keya.

Hata hivyo katika mkutano huo waandishi wa habari walionyesha kushangazwa na kushirikishwa mapokezi ya Nundu wakati mbunge huyo tangu amepata uwaziri hajawahi kuwashirikisha kwenye jambo lolote.

Kwa upande wake Katibu wa maandamano hayo, Rashid Blaa, alikiri mbunge kutelekeza makundi mbalimbali wakiwemo waandishi wa habari kwa kile alichokieleza kwamba kunatokana na watu wake wa karibu aliokuwa nao kumuongoza vibaya.

Mei 4, mwaka hu Rais Jakaya Kikwete, alilifanyia mabadiliko Baraza la Mawaziri na kuwatema mawaziri sita, akiwemo Nundu, baada ya kuguswa na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) na taarifa za wenyeviti wa kamati za Bunge za Hesabu za Serikali (PAC), Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na Ardhi, Maliasili na Mazingira.

Nundu anatuhumiwa kuingia mchakato wa kumpata mzabuni wa kujenga gati namba 12 na 13 katika Bandari ya Dar es Salaam.

Mbali na Nundu mawaziri wengine waliotemwa kutokana na ripoti hizo ni waliokuwa Waziri wa Fedha, Mustafa Mukulo, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda.

Naidu mawaziri walioachwa ni Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Lucy Nkya na Athumani Mfutakamba wa Uchukuzi.

Baadhi ya mawaziri hao walituhumiwa kuhusika moja kwa moja kwa katika matumizi mabaya ya fedha za umma na wengine walishindwa kusimamia wizara zao na kuisababishia serikali hasara ya mamilioni ya fedha.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment