


.jpg)
Asilimia 72 ya dawa za binadamu zinazotumika nchini, zinaagizwa nje, huku baadhi yake zikiwa hazifai kwa matumizi.
Rais Jakaya Kikwete alisema hayo jana kwenye hotuba yake ya kuzindua wiki ya wafamasia jijini Dar es Salaam.
Kwenye hotuba hiyo iliyosomwa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi, Rais Kikwete alisema utegemezi wa dawa za binadamu unatokana na idadi ya viwanda sita vilivyopo nchini kutokidhi mahitaji yaliyopo.
Hata hivyo, Rais Kikwete alisema pamoja na utegemezi huo, serikali imejidhatiti kutoa kipaumbele hususan kwa zabuni za usambazaji dawa kwa mashirika na taasisi za umma, kupewa viwanda vya ndani.
Lakini Rais Kikwete ripoti ya Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) inayoonyesha kati ya asilimia 25 na 30 ya dawa zinazotumika nchini ni duni ama bandia hazitoi taswira nzuri kwa vile madhara yake ni makubwa kwa jamii.
Alisema serikali imejipanga kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya ufamasia, ikiwemo kuwepo kwa sera ya dawa, kuongeza vivutio kwa wawekezaji wa viwanda vya dawa, udhibiti wa dawa bandia na kupunguza kodi.
Rais Kikwete alisema kudhibiti dawa bandia kunahitaji ushirikiano wa taasisi mbalimbali za kitaifa, kikanda na kimataifa.
Rais wa Chama cha Wafamasia (PST), Elizabeth Shekalaghe, alisema pamoja na mambo mengine, umuhimu wa kada upo katika kuielimisha jamii kuhusu matumizi sahihi ya dawa, jambo litakaloepusha hatari kwa binadamu.
Shekalaghe alisema matumizi yasiyo sahihi ya dawa yanaweza kusababisha madhara kwa binadamu ikiwemo kupata ulemavu na wakati mwingine kifo.
Alisema takwimu zinaonyesha kuwepo ongezeko kubwa la matumizi ya dawa nchini, hivyo kupanua wigo wa uelewa wa watu kuhusu matumizi hayo ni jambo lisiloepukika.
Pia Shekalaghe alisema pamoja na matumizi sahihi ipo haja ya kutilia mkazo ubora wa vifaa vya tiba na kuzingatia maadili mema yanayoiongoza kada hiyo.
Kwa mujibu wa Shekalaghe, tasnia ya famasia inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo ukosefu wa fursa za kujiendeleza kitaaluma, ukosefu wa idara ya dawa katika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, mazingira duni ya kazi na mishahara duni.
Mwenyekiti wa PST, Dk Romuald Mbwasi alisema dawa ni mhimili muhimu kwenye tiba, hivyo suala la matumizi sahihi na taratibu zinazopaswa kuzingatiwa ni muhimu zikatekelezwa kwa vitendo.
akitoa mchango binafsi, Dk Mwinyi alisema changamoto ya ukosefu wa idara ya famasia katika wizara ya afya na ustawi wa jamii imezungumzwa muda mrefu, sasa umefika wakati wa utekelezaji wake.
“Sioni sababu ya kuendelea kuitaja changamoto ya ukosefu wa idara ya dawa pale wizara, sasa mimi niwahakikishie kwamba hilo litafanyiwa kazi ndani ya muda mfupi ujao,” alisema.
Kwa upande, Mlezi wa PST, Dk Reginald Mengi, alishukuru ushirikiano uliopo kati ya serikali na chama hicho na kusema unathaminiwa na wafamasia nchini.
Dk Mengi alisema kwa vile serikali kupitia kwa Rais Kikwete imeelezea kuzitambua changamoto zinazowakabili wafamasia nchini, kada hiyo imepata matumaini ya kuwepo suluhu kwa vile pamoja na kuzungumzwa mara kwa mara, utekelezaji wake ulikuwa hafifu.
Pia Dk Mengi, akihojiwa na waandishi wa habari baada ya hafla hiyo, alisema pamoja na mambo mengine, kuna haja ya kuwepo sheria kali zinazodhibiti uingizaji wa dawa bandia, ikibidi kuhusisha kosa hilo na makosa ya mauaji.
“Kuingiza dawa bandia maana yake ni kusababisha vifo kwa watu wasiokuwa na hatia, hili linaweza kuwekwa kwenye orodha ya makosa ya mauaji,” alisema.
Dk Mengi alisema inashangaza kuona dawa bandia zinatoka kwenye mataifa ambayo ndani yake, yanaongozwa na sheria kali na utaratibu usiotoa mwanya wa kuwepo matumizi ya dawa bandia.
“Kama ndani ya nchi ambazo zinatengeneza dawa bandia hauwezi kuwapata wakitumia dawa hizo, kwa nini zipenye na kuingizwa kwenye nchi masikini ikiwemo Tanzania,” alihoji.