


.jpg)
Shirikisho la riadha la kimataifa (IAAF) limewathibitisha wanariadha wawili wengine kutoka Tanzania, Faustine Mussa na Mohamed Msindoki, kuwa wamefuzu kushiriki kwenye michezo ya Olimpiki ya London 2012 itakayofanyika kuanzia Julai 27.
Mussa amefuzu kushiriki michuano hiyo baada ya kushiriki mashindano ya riadha ya mbio za Marathon nchini Poland Machi 29, wakati Msindoki amefuzu baada ya kushiriki mashindano kama hayo nchini Ujerumani Mei 6 mwaka huu.
Awali wanariadha hao walitangazwa na chama cha riadha nchini (RT) kuwa wamefuzu, hawakuweza kujiunga na wenzao kambini kutokana na kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) kusubiri taarifa ya uthibitisho kutoka IAAF.
Akizungumza na NIPASHE jana, katibu wa TOC, Filbert Bayi, alisema tayari wamepata uthibitisho kupitia barua pepe iliyowasilishwa na IAAF kuwa wakimbiaji hao wamefuzu.
Alisema Tanzania imefarajika sana kuongeza idadi ya washiriki wa Olimpiki ambapo pamoja na wapo pia Samson Ramadhan na Faustine Mussa wanaokimbia marathon na Zakia Mrisho (mita 5,000), wakati katika ngumi yupo Seleman Kidunda na kwa upande wa waogeleaji ni Magdalena Moshi.
Bayi alisema pia kwa upande wa mchezo wa kuogelea wameongezewa nafasi moja ya muogeleaji mmoja wa kiume.