Wednesday May 22, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Kigi Makasi kumbadili Maftah Simba

21st July 2012
Print
Comments
Kocha wa klabu ya Simba, Milovan Cirkovic

Kocha wa klabu ya Simba, Milovan Cirkovic, amesema Kigi Makasi, winga aliyesajiliwa kutoka kwa mahasimu wao Yanga ataziba pengo la beki namba tatu Amir Maftah ambaye ni majeruhi wa kidole cha mguu kwenye mchezo wa leo wa Kundi A la Kombe la Kagame dhidi ya klabu ya Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya kufanya marekebisho kwenye kikosi chake.

Akizungumza na Nipashe jana, Cirkovic alisema atamkosa Maftah aliyeumia kidole kwenye mchezo uliopita, lakini huenda mchezaji wake mpya aliyesajiliwa kutoka Yanga, Kigi Makasi akaziba nafasi hiyo akicheza kama beki wa pembeni.

Winga Kigi amewahi kucheza beki tatu, pembeni, akiwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 23, chini ya Jamhuri Kiwhelu.

Endapo Makasi hatokuwa katika nafasi ya kuanza mchezo huo, alisema Cirkovic, atamtupia Haruna Shamte kazi ya kuziba pengo hilo.

Simba na Vita kila moja ina pointi tatu na ingawa zimeshaingia robo-fainali kufuatia Ports ya Djibout kufungwa 3-1 jana na URA inayoongoza Kundi A na kutolewa, zinawania heshima ya nafasi ya pili.

Milovan alisema timu yake haikucheza vizuri kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya URA ya Uganda lakini ilibadilika kwenye mchezo wa pili dhidi ya Ports ya Djibout ambapo Simba iliibuka na ushindi wa magoli 3-0.

"Hata kwenye mchezo dhidi ya Port bado sikuridhishwa na uchezaji hasa kwenye umaliziaji... lakini nimekaa na wachezaji mazoezini na naamini mchezo wa kesho (leo) utakuwa na mabadiliko makubwa,' alisema Cirkovic.

Aidha, alisema kuwa mchezo wa leo watacheza pasi ndefu huku timu ikibadilika kulingana na uchezaji wa wapinzani wao.

Alisema kuwa ameiona klabu hiyo ya Kongo kwenye mchezo wao dhidi ya URA ambapo walifungwa magoli 2-0 hivyo anajua nini cha kufanya kuibuka na ushindi.

Endapo Simba itashika nafasi ya pili kwenye kundi lake itakutana na mshindi wa kwanza wa Kundi C Atletico ya Burundi ambayo ilimaliza mechi zake ikiwa na pointi saba, moja juu ya Yanga.

Endapo itamaliza namba tatu, itakutana na yeyote kati ya Mafunzo ya Zanzibar, Tusker ama Azam zenye nafasi sawa kusonga mbele kutoka Kundi B.

 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment