Thursday May 5, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Malezi bora yatachangia watoto kujiepusha na wabakaji

22nd May 2012
Print
Comments

Miongoni mwa sababu zinazochangia ubakaji nchini ni ulevi wa pombe unaosababisha  magomvi kwa wazazi hata kuchangia watoto kukosa huduma.

Visa Iddi, 27 wa kijiji cha Bunju B, Kata ya Mabwepande, Dar es Salaam anasema kinachochangia ubakaji ni ulevi wa pombe na utumiaji wa madawa ya kulevya kwa vijana unaosababisha wazazi wasiwajibike kwenye familia zao.

Vitendo hivyo anasema kuwa, vingepungua kama wazazi wangetimiza wajibu wao katika familia na kama serikali ingefuatilia kwa makini  kuchunguza sehemu zinazofanywa ulevi kwa sababu vijana wanaharibika kutokana na ongezeko la  vitendo vya ubakaji.

Takwimu kutoka kituo cha polisi Wazo Hill - Kinondoni zinaonyesha kuwa vitendo vya ubakaji vinaongezeka. Matukio  yaliongezeka kutoka 71  mwaka 2010 hadi 88 mwaka 2011  kati yake   24 yalifikishwa mahakamani mwaka 2010 na 32 mwaka 2011.

Kesi 47 za ubakaji  zilifutwa  mwaka 2010 kwa  kukosa ushirikiano toka kwa walalamikaji.

Mwaka huu 2012  kituo  cha Wazo  kimepokea matukio 37 ya ubakaji ambapo ni  10 tu yamefikishwa  mahakamani na 27 yako kwenye upelelezi.

Mratibu wa kituo cha polisi Wazo Hill, Gwisael Pagi, (ASP-OCS), amesema wabakaji hawajutii makosa yao kwa sababu watuhumiwa wengi wanaokamatwa huwa wanaachiwa huru kutokana na upande wa mlalamikaji kutofika mahakamani wanapohitajika.

“Wanaotufikia tuwasaidie  tukishawakamata watuhumiwa wakirejea nyumbani hufanya vikao na kusuluhisha kindugu”,amesema polisi wa kituo cha Wazo Hili,  Halima Ibrahim  anayeshughulika na dawati la ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto.

Amesema kesi ya kubaka inahitaji ushahidi wa aliyebakwa na dakitari, na mara nyingi kesi ikishafikishwa mahakamani walalamikaji hawafiki kutoa ushahidi.

“Polisi unaweza kuandaa kesi vizuri na mwanasheria wako ili kesi iendelee, majibu yakatoka kuwa kesi iende mahakamani ukiipeleka baadae haitoi matunda kwa sababu wanaotakiwa kwenda kutoa ushahidi hawaendi” alilalamika.

Halima anasema, kuna  waliofungwa kwa  kubaka na wengine wameshindwa kuithibitishia mahakama na kuachiwa  huru.

Amewahimiza wazazi kukaa na watoto wao ili wawape elimu ya maisha bora na pia wananchi wahakikishe kuwa, inapotokea uhalifu wa ubakaji katika eneo lao washirikiane kwa umoja ili aliyebakwa haki yake iweze kupatikana mahakamani.

Halima amesisitiza kuwa mtu akibakwa anapaswa asioge wala kubadilisha nguo bali wananchi wamsaidie aende polisi kuchukua fomu ya PF3 kisha aende hospitali ya wilaya Mwananyamala kupatiwa matibabu na ushahidi wake kuchukuliwa na daktari.

Ameshauri  elimu  kuhusu jinsi ya  kupambana na ubakaji itolewe mashuleni na  kwenye makazi ili wananchi wajue mbinu za kuhakikisha kuwa wabakaji wanatiwa hatiani kisheria.

Kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti Makosa ya Kujamiiana ya mwaka 1998 mtu anayepatikana na kosa la kubaka anahukumiwa kifungo cha miaka isiyopungua 30 jela.  Na kubaka mtoto ni kifungo cha maisha jela.

Dakta Prisca Berege anayeshughulikia magonjwa ya watoto katika hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam, amethibitisha kuongezeka kwa vitendo vya ubakaji na kusema kuwa huwa anapokea kesi tatu kwa siku moja hospitalini hapo.

Amewaomba wazazi na walezi kuwalea watoto wao katika maadili mema na wawaelimishe kuhusu madhara ya kulewa ikiwa ni pamoja na kuwaandaa kwa ajili ya maisha yao ya baadaye.

Naye Dkt. Berege amesema, kuwalea watoto wao kwa ukaribu itasaidia mtoto kutoa taarifa kwa mzazi au hata kama kitendo kikitokea kwa mwenzao itakuwa rahisi kueleza wenzake ili hatua ziweze kuchukuliwa haraka.

Aidha katika jitihada za kupunguza vitendo vya ubakaji,  Gaudence Nyamwihura, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni amesema serikali imejipanga vema kuhakikisha mtuhumiwa wa ubakaji anachukuliwa hatua za kisheria.

Amewataka serikali za mitaa kuwaelekeza wanaofika kwao na kesi za ubakaji waende polisi ili mtuhumiwa akamatwe kwa hatua ya kwanza kisha apelekwe hospitali ndani ya masaa 72 ili aliyebakwa akapewe tiba ya kuzuia maambukizi ya VVU (PEP)

Pia amewashauri wazazi na walezi kuchukulia umuhimu malezi ya maadili mema kwa watoto wao ili wajiepushe na ulevi kwa sababu ndiyo unaochangia vitendo vya ubakaji.

Ameviomba vyombo vya habari na wadau wote nchini  waelimishe jamii kuhusu malezi yasiyochochea ulevi unaosabaisha mifarakano ya wazazi ikasababisha watoto kukosa huduma na kuwafanya wakimbilie mitaani.

Padre Adolph Majeta wa kanisa Katoliki Boko, kata ya Bunju jijini Dar es Salaam amesema “swala zima liko kwenye malezi ambayo yameharibika iwe ni nyumbani, mashuleni, chuoni hakuna malezi endelevu kwa vijana”.

Vitendo vya ukatili kama ubakaji  anasema vinavyosababishwa na ulevi miongoni mwa vijana wengi  nchini vinatokana na wao kujifunza  vitabu, kwenye internet, magazeti na Televisheni badala ya wazazi kuwaelimisha watoto watambue wajibu wao na wajitambue wao wenyewe.

Padre Majeta  amesema, vijana wengi wamekosa hofu ya Mungu wanaiga mambo ambayo hawayajui hivyo ameitaka jamii hasa wazazi warudi kwenye malezi wawaelimishe watoto wao kuhusu madhara ya ulevi.

Naye Sheikh na Imamu wa Msikiti wa Bunju A,  Shame Kombo Shame, Bunju amethibitisha kuwa ulevi ni miongoni mwa sababu za kutokea kwa migogoro nyumbani na kusababisha baadhi ya wanaume kukimbia familia zao wakidhani ni suluhisho la matatizo.

Imamu huyo amesema kuwa, baada ya mama kubaki peke yake nyumbani bila msaidizi watoto hukosa huduma muhimu na kutelekezwa na wengine hubakwa kwa sababu wanakuwa hawana ulinzi hata wa wazazi.

“Kwa waislamu mtu anayefanya tendo hilo adhabu zake huwa ni kutengwa na jamii pamoja na kuchomwa sindano ili asirudie.” 

Anasema sheria hiyo haijatumika hapa Tanzania kwa sababu ya kulinda haki za binadamu na ndiyo maana vitendo vinajirudia.

Sylvester Ntongya, Afisa Mtendaji, Kata ya Mbweni, amesema mwaka jana 2011 alipata kesi 2 za ubakaji, moja ilimhusisha mwalimu wa madrasa (Chuo), kumbaka mtoto, na nyingine mtu aliyemtorosha mtoto wa kiume akamtumia kwa vitendo vya kumlawiti.

“Tulimshauri aende polisi apate PF3 kisha ampeleke hospitali na alipokwenda kupimwa walikuta ni kweli ameharibiwa alikuwa ni mtoto wa miaka (10), kisha tukamwambia aende mahakamani hadi sasa kesi iko mahakama ya Kinondoni” Amesema  Ntongya.

Amesema kesi ya pili ni ya mama aliyeshitaki kuwa mwanae wa kiume alitoroshwa na mtu akapelekwa Zanzibar baadaye iligundulika kuwa jamaa alikuwa anamuingilia ki mwili, alimshauri akashitaki lakini hajui kama alienda kwa sababu hadi leo hawajamuona tena.

Ameshauri elimu itolewe kwa jamii ili wazazi au walezi wajue madhara ya vitendo hivyo na walinde watoto wao, na kama ikitokea mtu amefanya kitendo hicho apewe adhabu kali iwe fundisho kwa watu wengine.

Ntongya amesema kifungo cha miaka 30 jela inawezekana hakitoshi kwa sababu watu wanajua lakini bado wanafanya hivyo na kupendekeza  wanyongwe kabisa kwani kama mtu wa miaka 39 anambaka mtoto wa miaka 10 huyo anasema hana sababu ya kuishi kwenye jamii.

Sister Christina Ngalya, Muuguzi na Afisa Utawala wa Hospitali ya Mbweni jijini Dar es Salaam amesema hospitali yaoi mwezi wa nne mwaka 2012, ilipata kesi ya ubakaji ambayo mfanyakazi mwenzao (Hakumtaja jina) mke wake alibakwa.

“Tulifanya uchunguzi tukakuta ni kweli alikuwa amebakwa na ameumizwa. Tulimuanzishia matibabu kabla ya saa  72. Kwa sababu tuna kitengo cha Ukimwi, daktari anayehusika alitwambia hata kama vipimo havitaonyesha maambukizi lakini dawa hizo tumpatie kwa siku 28 au mwezi mzima” amesema Sister Ngalya.

Kibaya zaidi anasema ni kuwa mama huyo aliyebakwa alikuwa ni mjamzito wa mimba ya miezi sita ambapo mwanzoni alikuwa hasikii mapigo ya mtoto tumboni, lakini walipompima waliona mimba ilikuwa inaendelea vizuri hadi leo hajajifungua.

Ameiomba jamii iendelee kuelimishana  pia serikali iendelee kusisitiza watu wasichoke hasa wazazi wawaeleze watoto wao waepukane na watu kuwaeleza maneno yasiyofaa Symphoroza Gordian, Afisa Maendeleo ya Jamii, Kata ya Mbweni, anasema bado kuna tabia ya kulindana katika jamii ya watu wa Pwani kwenye kata yake kwani utakuta mtu ana tabia ya ubakaji lakini hata yule aliyejitolea kulifuatilia anaishia njiani.

Kwa upande wake anasema, alishawahi kupata kesi ya mtoto wa darasa la nne kubakwa baada ya siku chache mama yake akawa anataka kumuhamisha aliyebakwa, alimfuata mtendaji lakini hakumkuta na waligundua baada ya kumuuliza sababu ya kutaka kumhamisha mtoto.

Amesema kitakachosaidia ni elimu kupitia vyombo vya habari, makundi ya watu mbali mbali kama ya aki na mama na wanafunzi ili kuelimisha watu waachane na vitendo hivyo na wazazi pia wawe mstari wa mbele kuepusha watoto wao katika njia mbaya.

Symphoroza Gordian ameomba kila kata itumie wajumbe wake watendaji wakusanywe pamoja waelimishwe kwanza ili watakapokuwa kwenye kata zao waweze kufikisha elimu kwa wenzao.

Amesema kwenye serikali za mitaa kati ya wajumbe 8 kuna wanawake watatu katika kila kata waelimishwe na wakafundishe wenzao na kwa njia hiyo tutasaidia kupunguza ubakaji kama si kuutokomeza kabisa.

NB: Happiness Bagambi ni mwandishi wa habari kutoka Chama cha Wanahabari Wanawake nchini - TAMWA


SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles