Friday Apr 29, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Shibuda anapokuwa kikwazo kwa Chadema!

23rd May 2012
Print
Comments

Mbunge  wa Maswa Magharibi, John Shibuda, ameibua malumbano ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambacho yeye ni mwanachama wake.

Ameibuka katikati ya harakati za kupiga vita ufisadi, ufisadi, rushwa, matumizi mabaya ya ofisi na rasilimali za umma, akatangaza nia ya kutaka kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Niweke wazi kwamba mimi ni mmoja wa waliomuunga mkono Shibuda, kwa kigezo kwamba kila raia ana haki na uhuru wa kuelezea hisia zake, ili mradi havunji sheria za nchi.

Shibuda ameitumia haki hiyo kuelezea hisia zake, nia yake, matamanio yake, nia na utashi wa kutaka kuwania urais. Baadhi ya viongozi wa Chadema wakamjia juu.

Ni ukweli ulio wazi kwamba hivi sasa umma wa Watanzania una imani kubwa kwa Chadema, lakini si kweli kwamba kila aliye ndani ya chama hicho ni mwenye kuaminika na kuheshimika kwa jamii.

Wamo wahuni kama walivyo waadilifu ndani ya Chadema, wamo wenye hulka za wizi na ufisadi kama walivyo walio safi ndani ya chama hicho kinachopata nguvu zaidi kwa salaamu yake people’s power.

Kwa hiyo si kila aliye ndani ya Chadema, anaweza kuzungumza na kuaminika kwa kile anachokizungumza, hata kama ni ‘utumbo’ unaopaswa kupuuzwa na mtoto wa anayeanza darasa la kwanza baada ya kuhitimu mafunzo ya ya chekechea.

Wanaweza kujitokeza wehu wa kisiasa na wengine wenye sifa chafu zinazojidhihirisha kwa maneno na matendo yao, wakautumia ‘mgongo wa Chadema’ kuaminisha ama kuhalalisha matakwa yao mbele ya umma.

Wakati Chadema ikiwa mfano wa kimbilio kwa raia walio wengi, viongozi waliopewa dhamana ndani yake wanapaswa kutambua kwamba si kila hoja inastahili kujibiwa. Kunyamaza peke yake kunatoa fursa kwa umma kuzitafakari hoja dhaifu zinazotolewa na walio ndani ya chama hicho.

Ninakumbuka kuna wakati aliyekuwa Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Methodius Kilaini, aliulizwa kuhusu kauli ya kejeli ya Askofu wa kanisa moja la ‘kilokole’ lililopo maeneo ya Mwenge jijini Dar es Salaam.

Mhashamu Kilaini alisema, “kanisa Katoliki halimjibu kila mtu, muacheni huyo (akamtaja jina) afanye biashara zake na Kanisa Katoliki liendeleze utume na kazi lililotumwa na Mungu.”

Ninalikumbuka sana jibu la Mhashamu Kilaini na kwa mfano huo, Chadema inapaswa kusimamia mambo ambayo chama hicho kimetumwa na umma. Kujibu kila hoja, kumjibu kila mwanachama hata pale anapozungumza kwa ‘furahisha baraza’, ni kupoteza mwelekeo.

Sina maana ya kuufananisha mfano huo na hali ilivyojitokeza katika chama hicho kufuatia kauli ya Shibuda, lakini sioni msingi uliokifikisha chama hicho kuwa kwenye malumbano ya urais wa 2015.

Mtu anayezungumzia urais wa 2015 wakati taifa likiwa katika wimbi wa wizi wa mali, rasilimali na fedha za umma unaofanywa na baadhi ya waliopo kwenye utawala, ni kutaka kupoteza mwelekeo wa taifa. Chadema inajibu, inalumbana ili iweje?

Shibuda ni mwanasiasa mkongwe, anajua kuzicheza siasa za Tanzania, tangu akiwa CCM na sasa Chadema.

Sina kumbukumbu ya manufaa ya dhahiri yanayoweza kunisukuma kulitaja jina la Mbunge huyo kuwa amechangia kuleta mabadiliko, badala yake nina historia ya `purukushani za kisiasa’ zinazolenga kuibua malumbano ama mafarakano.

Unaporejea katika uhai wake wa uanachama wake ndani ya CCM, unaweza kumjua Shibuda ni mtu wa aina gani. Hata alipoibua hoja ya nia yake kutaka urais, huku akisema angekuwa anatokea mikoa ya kanda ya kaskazini (pengine) asingeguswa, anashangaza!

Hivi Chadema inapata wapi ujasiri wa kumjibu mwanachama wake mwenye dhamana ya ubunge, pale anapoibua hoja dhaifu kama ya kutaka umma uamini kuwa Chadema ni chama chenye ukabila?
Binafsi si mwanachama wa Chadema, sina kadi, skafu, fulana, kofia wala bendera ya chama hicho.

Ndivyo ilivyo kwa vyama vingine vya siasa nchini, kwa maana maadili ya kazi na utashi binafsi havijanifikisha huko.

Lakini ninatambua kuwa na ndugu, jamaa na marafiki walio katika Chadema. Mmoja wao ni Mbunge wa Viti Maalum, Esther Matiku. Wapo wengine kwenye orodha ndefu ya walio ndani ya Chadema kama ilivyo kwa vyama vingine vya siasa.

Ninapokuwa katikati yao, msingi mkubwa ni kujadili mustakabali wa taifa hili huku misimamo ya kiitikadi ikiwekwa kando. Unapozungumzua utaifa hakuna nafasi ya ukabila, udini ama rangi ya mtu. Mbunge anapata wapi nguvu ya ‘kulichomekea’ hilo katika nia yake ya kuutaka urais kupitia Chadema?

Dhana ya kutaka Chadema ionekane chama cha kikabila, imepitwa na wakati, haina mashiko, ni mufilisi na ina haki ya kuitwa ‘ya kishenzi’. Hoja za ‘kishenzi’ zimewahi kutolewa hata kukihusisha Chama cha Wananchi (CUF) kuwa cha kidini.

Miongoni mwa waliolieneza hilo wapo ndani ya serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar, wakisimamia misingi ya umoja wa kitaifa usiotoa fursa ya udini. Tunajifunza nini?

Kwa hali hiyo, sioni sababu ya msingi kwa Chadema kuingia katika malumbano yanayoasisiwa na kauli ya Shibuda, akijiridhisha kwa haki na uhuru wa kutoa maoni, pale alipozungumza, akatangaza nia kuwania urais mwaka 2015.

Yapo ya msingi yanapaswa kushughulikiwa na Chadema na vyama vingine vya siasa katika kufikia matarajio ya umma na si kujadili na kujibu kauli za kila anayefumbua kinywa na kunena, hata kama hagusi hisia za familia moja ndani ya mamilioni ya raia waliopo Tanzania.

Mashaka Mgeta ni Mwandishi wa Habari za Siasa wa NIPASHE. Anapatikana kwenye simu namba +255 754 691540, 0716635612 ama barua pepe;[email protected]

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles