Friday May 6, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Mfuko wa uchaguzi wa wanafunzi unapoteza vipaji

8th May 2012
Print
Comments

Ni wakati mwingine tena umefika wa kushuhudia mchujo wa wanafunzi wa sekondari, Kidato cha Sita, kupitia mitihani. Ni dhana ambayo kwa upande wangu imepitwa na wakati, na hata kama tunataka kuendelea nayo, ina kinzana na uhalisia wa mfumo wa elimu nchini.

Nikianza na la pili, niliwahi kusema kama kweli baraza la mitihani  linafanyakazi yake kwa kushirikiana na wadau wengine katika elimu ili kuhakikisha kuwa elimu inayotolewa inaelekea kuwafanya watahiniwa waanze katika msitari mmoja katika mbio za kuelekea kwenye mchujo.

Inawezekanaje wanafunzi wa shule za kata ambao hawana walimu kabisa, au shule ambazo hazina walimu na hawana miundo mbinu inayotakiwa kurahisisha kufanya masomo, wanakaa katika mtihani mmoja; ni sawa na kuwaingiza katika riadha wengine wakiwa mbele kwenye kona ya kwanza , na wengine wako kwenye msitari wa kuanzia.

Ni wazi walioko kwenye kona ya kwanza watashinda mashindano. Baraza la Mitihani linajua haya, lakini ati tunakuja kutoa takwimu za kushindwa na kushinda, kwa vigezo gani vya kisayansi vilivyotumika kuwashindanisha hawa?

Ninaona kama kwa sasa tunachofanya ni ili mradi kutimiza wajibu. Baraza la mitihani kwa kushirikiana na wadau wa elimu na hasa serikali kuu na serikali za wilaya (halmashauri) lazima wajenge mkakati wa kuhakikisha kuwa, kila mwanafunzi anapoingia kwenye mtihani anaingia katika mazingira sawa na mwenzake wa shule ingine.

Hili la mchujo ndilo linalonikera zaidi. Licha ya kutambua kuwa watu wana uwezo tofauti, lakini  kwa dhana ya mchujo sidhani kama mwalimu na mtaala unaweza kubadilika, ili mfumo wa ufundishaji uelekee katika kumfanya mwalimu kuwa mwezeshaji na msaidizi katika mchakato wa kujifunza wa mwanafunzi, badala ya kuwa mjuaji anayetafuta nani anaweza kufaulu na nani atafeli.

Na ugonjwa huu uko hadi vyuo vikuu; wanafunzi wanaishi kwa matokeo ya testi na kazi za nyumbani- course work assessment, na akijihakikishia kuwa amepata alama 40 basi anajua atafaulu.

Walimu hawajali kama wanafunzi wanaelewa, yeye anachojali ni kukusanya alama. Ndio maana tuna idadi kubwa ya wanafunzi wanaofaulu lakini ukimuuliza alielewa nini katika somo, hawezi kusema.

Kwanza hivi ufundishaji wetu ukoje; mwalimu na mwanafunzi ili waweze kufikia malengo ya kitaaluma, lazima wanaishi kama marafiki wa kumsaidia mwanafunzi kufaulu, na sio mwalimu anakuwa kisaidizi cha kuhakikisha wanafunzi wanakomoka, wanafeli.  Je, baraza la mitihani na taasisi ya elimu wanafuatilia ufundishaji ulivyo?.

Mwalimu anakaa mbele, wanafunzi wanamsikiliza, anamaliza na kuwaachia maswali, lakini hajui kama walimuelewa; kama ilivyo kwa wahubiri wanaohubiri kuhusu ufalme wa Mungu na kuacha dhambi. Lakini dhambi zinaendelea kutendeka, na idadi ya wanaohudhuria makanisani inapungua, kwa sababu kosa wanalolifanya ni kudhani waumini wana akili sawa, ufahamu sawa.

Mfumo wa elimu, na hasa ufundishaje unatakiwa uwe ule ambao mwalimu kwa wakati wote anakuwa akijua uwezo wa kila mwanafunzi, na kuwa kwa ufundishaji shirikishi huku mwalimu akiwa mwezeshaji zaidi, na sio mtoa maagizo, instructor, wanafunzi wanaweza sasa kufanya kazi za shule wakijua kuwa mwalimu wao yupo kwa ajili ya kuwasaidia kuwapanua mawazo, kuwaongoza namna ya kufanya vizuri zaidi kazi zao, na mwisho ni kuwa kitakachowasilishwa kwa mwalimu sio kile alichofanya mwanafunzi peke yake, bali ni matokeo ya mwalimu na mwanafunzi kushirikiana katika kumsaidia mwanafunzi kuelewa.

Dhana ya kuwa mwanafunzi ahangaike mwenyewe na mwalimu anamsubiri mwisho wa msitari kuona kama atafika sawa na wenzake au atakuwa nyuma yao, ili kumpatia alama; kwangu hii si dhana nzuri kwa kweli kielimu,  ni dhana potofu, haina tija kielimu na ndio inayoendeleza dhana ya mchujo, na kuwabakiza “makapi” huko mtaani.

Mwisho tujiulize, hivi ukishawachuja wanafunzi na matokeo ya mwisho ni mwanafunzi kupata sifuri, kwa wale ambao vita vimewatupa, wanakwenda wapi? Wanaishia kufanya nini? Tunajenga taifa la namna gani?

Na tutambue huyu ni mtoto, ana safari ndefu ya maisha, lakini mwalimu, serikali, yaani baraza la elimu, limeshamwambia kuwa amefeli, na kwa sababu hiyo anachukuliwa kama makapi, hafai tena, wazazi na yeye mwenyewe wanakata tamaa. Na anaweaza asiendelezwe, asijiendeleze, kwa vile amefeli. Tufutilie mbali dhana hii!


[email protected], 0766959349


SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles