Sunday May 1, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Watoto wakeketwa wakiwa wachanga

6th May 2012
Print
Comments

Baadhi ya watu wanaondekeza mila potofu ya ukeketaji wa watoto wa kike katika Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, sasa wanakeketa watoto wao wakiwa wachanga kati ya umri wa mwezi mmoja au miwili kwa kuogopa kugundulika na kuchukuliwa kuchukuliwa hatua.

Mtoto akishazaliwa husubiriwa atimize umri wa mwezi mmoja au miwili ndipo hufanyiwa ukeketaji na akishafikia umri wa usichana huingizwa kwenye ngoma ya unyago ambayo hutoa mafunzo ya kuishi na mume.

Utafiti uliofanywa na NIPASHE kwa kushirikiana na Chama cha Wanahabari Wanawake (Tamwa), katika kata tatu za wilaya hiyo, umebaini hayo baada ya mahojiano na wakazi wa maeneo hayo.

Kata zilizofanyiwa utafiti huo ni Ruvu, Mwembe na Maole, ambapo wakazi wake ni jamii ya wafugaji (Wamasai) na Wapare.

“Sasa hivi huwezi kukuta sherehe za ukeketaji, watu wanafanya kwa siri sana wanakeketa watoto wakiwa wachanga kuanzia mwezi mmoja,” alisema Mwenyekiti wa Kijiji cha Darajani, Kata ya Ruvu, wilayani humo, Tatu Mkumbwa.

Alisema watu wanaoendeleza mila hiyo ya ukeketaji, huwafuata mangariba na kuwaomba wawakekete watoto wao wakiamini kuwa mtoto asipotahiriwa hawezi kuolewa anapofikia umri wa utu uzima.

Mwenyekiti huyo alisema kufanyika kwa siri kwa vitendo hivyo kunatokana na viongozi wa kiserikali na taasisi zisizo za kiserikali kutoa elimu kuhusu madhara ya ukeketaji na kuonywa kuwa watu watakaopatikana kufanya mila hiyo watakamatwa na kuchukuliwa hatua.

Alisema baadhi ya watu hulazimika kuwafanyia watoto wao ukeketaji kwa vile katika jamii imeshajengeka kuwa mtoto wa kike ambaye hajakeketwa hata akifikia umri wa miaka 30 ataonekana mdogo mbele ya wasichana wenzake waliofanyiwa mila hiyo.

“Kutokana na imani waliyonayo baadhi ya wasichana wakishakua na kujikuta hawajakeketwa wanalilia wafanyiwe kwa mawazo kuwa hawatapata wachumba wa kuwaoa,” alisema.

Kwa mujibu wa Afisa Tabibu Mwandamizi wa zahanati ya Maole katika Kata ya Maole Kijiji cha Mheza, zahanati hiyo imeshapokea wanawake kadhaa wanaokwenda kujifungua wakiwa wamefanyiwa ukeketaji.

“Hatujawahi kuletewa mtoto au msichana aliyepata madhara yanayotokana na ukeketaji lakini wanapokuja kujifungua ndio huwa tunawagundua kuwa wamekeketwa,” alisema.

Madhara ya ukeketaji yanaweza kusababisha mwanamke kupata maumivu makali wakati wa kujifungua kutokana na njia kuwa ndogo na kusababisha kutokwa na damu nyingi jambo linaloweza kumsababishia kifo.

Aidha mtu anapofanyiwa ukeketaji kama vyombo vilivyotumika havikuwa salama, anaweza kupata maambukizi ya magonjwa kama ya Ukimwi.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles