



Katika mfumo wa utawala ambao umelala au kudumaa, linapotokea jambo moja kubwa kufanyika kwa nadra hakika furaha ya wananchi haipimiki.
Hii ndiyo furaha ambayo ameletea umma Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, baada ya kutangaza kuwasimamisha kazi maofisa waandamizi wanne wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) na askari wanyamapori 28 ili kupisha uchunguzi wa mauaji ya faru katika mbuga ya Serengeti.
Tumesema kuwa ni furaha kwa hatua kama hizo kuchukuliwa siyo kwa kuwa tunawatakia mabaya watuhumiwa wa sakata hilo, ila kama taifa tunaanza kupata ahueni kwamba inawezekana misingi ya utawala bora ikatekelezwa kwa sababu siyo siha njema kiutawala kuchunguza watu wangali wamekalia viti vyao.
Hatua ya Kagasheki inaamsha imani ya wananchi kwa uongozi wake katika wizara ambayo inaaminika yenyewe tu ina uwezo wa kusaidia serikali kupata mapato ya kuendesha shughuli zake bila kutembeza bakuli kwa wahisani, aghalabu wakitoa misaada kiduchu tena kwa masimango mengi.
Kwa maana hiyo inapotokea basi habari kama hizi zinaibuka kutoka ofisi ya serikali kwamba kiongozi mmoja mwenye dhamana na wizara amekasirishwa na utendaji wa ovyo wa waliochini yake na kuamua kuchukua hatua, walau za kuwaweka pembeni wahusika ili kupisha uchunguzi, ni vema na haki kabisa kumpongeza kiongozi huyo.
Ndiyo maana tunamwambia Kagasheki kuwa kwa kasi hii aliyoanza nayo inawezekana kabisa akaleta mabadiliko makubwa katika wizara hii.
Tunampongeza na kumpa moyo.
Suala la wanayamapori limekuwa ni gumzo kubwa katika nchi hii kwa miaka mingi, tangu sakata la Loliondo, ugawaji wa vitalu vya uwindaji, uuzaji wa wanayama hai nje ya nchi, lakini pia biashara kubwa ya nyara za taifa hasa meno ya tembo.
Tanzania inanuka huko nje juu ya uwezo na utayari wake wa kukomesha biashara haramu ya pembe za tembo. Taifa hili linatajwa ama kuwa chanzo cha pembe haramu kwenda barani Asia au kuwa njia ya kupitisha pembe hizo kutoka mataifa mengine kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambako vita ya wenyewe kwa wenyewe haiachi serikali kuu kuimarisha ulinzi katika hifadhi zake.
Kuna biashara ya magogo. Hili limepigiwa kelele kubwa miaka na miaka; heka na heka za misitu zinateketezwa kwa watu kukata miti ili kupasua mbao.
Mfano mmojawapo ni janga ambalo linaandama misitu kuzunguka Mlima Kilimanjaro huku wasimamizi wakuu wa rasilimali hizo wakibeua kwa shibe inayotokana na biashara haramu.
Mapema mwaka huu tuliandika mfululizo wa habari na makala kuhusu uharamia dhidi ya maliasili katika Mlima Kilimanjaro, ukataji wa miti ya asili kwa ajili ya mbao, wanavijiji walionyesha madhara makubwa ya biashara hiyo ambayo askari wa Tanapa wamekataa kuikomesha kwa kuwa wamekuwa sehemu ya uhalifu kwa kuwa wananufaika nao.
Tunataja mambo haya kama njia ya kumfungua macho Waziri Kagasheki kuwa wizara yake ni janga kwa taifa kwa vizazi vya sasa na vijavyo; kwa kipindi cha miaka saba ya utawala wa Rais Kikwete, wizara hii imekaliwa na mawaziri wanne, ni wastani wa mwaka mmoja na nusu kwa kila waziri.
Hata makatibu wakuu mambo yamekuwa hivyo pia, wamepita wanne. Mabadiliko ya viongozi wakuu wa wizara kwa kasi hii siyo ya kawaida, yana siri ndani yake. Siri hii siyo nyingine ila ni ukweli kuwa kuna madudu mengi, kila anayeondoka anaondoka na sababu au kisingizio chake.
Hii ni wizara pekee katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ilipata kuwa na wakurugenzi waliorushiana makonde na wabunge wakionyesha kiburi na jeuri ya pesa walizopata kwa uharamia dhidi ya nyara za taifa hivyo kukataa kuhojiwa, lakini pia ni wizara ambayo imeshuhudia mkurugenzi akitunishiana misuli na waziri wake na kumuonya kuwa alimkuta na atamwacha.
Tunasema haya yote kumkumbusha Waziri Kagasheki upana wa mawanda ya wizara na uoza ambao umeigubika; ni wizara inayosimamia utajiri wa taifa hili; ni wizara ambayo hakika itaendelea kutajwa kuandamwa na kutajwa kwa sababu maandiko yanasema mti wenye matunda ndiyo unaorushiwa mawe.
Wizara hii imejaa matunda kila kona.
Pamoja na haya yote tunampa pole Waziri Kagasheki kwa kuthubutu, tunamtia moyo kwamba umma uko nyuma yake kwa kuwa ulitamani siku nyingi hatua kama hizi zichukuliwe, kwamba eti wanauawa faru lakini wahusika hawashtuki wala kutoa taarifa kwa wizara, huku ni kuficha madhambi jambo ambalo halikubaliki.
La msingi ni kwa waziri kuwa na msimamo, kutenda haki na kusimamia sheria bila kupepesa macho, kwa kasi na mwenendo wa namna hiyo atabadili taswira ya Wizara ya Maliasili na Utalii kutoka uchafu uliopindukia kuwa kioo na nyota ya taifa ing’aayo. Kanyaga Kagasheki.