Sunday May 1, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Tuuenzi Muungano wa Tanzania

26th April 2012
Print
Comments
Maoni ya Katuni

Watanzania leo wanaadhimisha miaka 48 ya kuzaliwa kwa taifa lao, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambalo lilitokana na muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Zanzibar tarehe kama ya leo mwaka 1964. Ni kitambo kirefu, bado miaka miwili tu Muungano huu utimize nusu karne, yaani miaka 50.

Katika mfumo wa maisha ya binadamu miaka 48 si haba, ni kitambo kirefu, ni umri wa mtu mzima mwenye majukumu katika jamii na kwa hakika anatazamwa kama kiongozi wa kaya mwenye wajibu wa kutunza na kuikuza familia yake, lakini pia ni miongoni mwa vichwa vinavyohesabiwa katika kulijenga taifa lake kwa kutoa mchango wa maana.

Ni kwa hali hii tunasema kuwa Muungano umepiga hatua, iwe ya umri au hata yote ambayo yamefikiwa tangu kuasisi kwake mwaka 1964. Sisi kama sehemu ya jamii ya Watanzania kila tunapotazama nyuma tunaona tuna kila sababu ya kujipongeza kama taifa kwamba pamoja na changamoto zote ambazo tumekumbana nazo, bado tumebakia kama taifa moja linaloitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ndiyo maana tunachukua fursa hii kuwatakia Watanzania wote kila la heri katika maadhimisho ya miaka 48 ya Muungano.

Hata hivyo, pamoja na Muungano kuendelea kuwako kwa kipindi chote hiki, bado unakabiliwa na changamoto nyingi. Kuna hisia kutoka kila upande, yaani Zanzibar na Tanzania Bara juu ya faida zake na ni upande upi unanufaika zaidi na muundo uliopo.

Kumekuwa na maoni ya kubadilishwa kwa mfumo wa serikali mbili kuwa serikali tatu, wapo wanaoamini kuwa serikali ya Tanzania Bara inakula ndani ya hazina ya Serikali ya Muungano, kwa maana hiyo ni vema kungelikuwa na serikali tatu ili kutofautisha serikali hizi kwa urahisi zaidi.

Kwa upande wa Bara nao wamekuwa na hisia kwamba Zanzibar inanufaika zaidi kwa sababu, kwanza ina serikali yake yenyewe na pia inakuwa tena sehemu ya Serikali ya Muungano, mifano imetolewa mingi juu ya mfumo wa vyombo vya uwakilishi wa wananchi, kwamba kuna uwakilishi uliopindukia kwa upande wa Zanzibar.

Kwa kifupi kila upande umekuwa unahisi kuwa mwingine ama unafaidika zaidi, au unajipendelea au kupendelewa na kuhengwa mno; kama ni ndoa inavyoelekea kwa baadhi ya hisia za wananchi ni kwamba yupo mwanandoa mmoja ambaye kazi yake ni kulia na kung’ang’ania kupewa hiki na kile na vyote kadri atakavyo bila kujua kuwa pia kuwa ana wajibu wa kutimiza katika ndoa hiyo.

Si nia ya tahariri hii kuorodhesha kero au matatizo yote ya Muungano, ila tunataraji haya machache kukumbusha kuwa pamoja na hatua zilizopigwa tukiadhimsiha miaka 48 ya uhai wake, bado zipo changamoto za kweli zinazohitaji kutazamwa upya kwa nia ya kuufanya usonge tena mbele miaka mingine 48 ijayo kwa ajili ya ustawi wa watu wake.

Tunatoa rai hii kwa sababu wanaounda mifumo kama hii ya Muungano ni wanadamu, na inatazamiwa kuwa mifumo hii ni lazima itazamwe kila wakati kama inakidhi mahitaji ya nyakati na matarajio ya kizazi husika. Ni kujidanganya pengine kuahatarisha Muungano wenyewe kama kero hizi hazitatazamwa kwa maana ya kuzitatua ili kujenga mustakabali wake mwema na ustawi wa watu wake sawia.

Sasa hivi taifa kinaingia katika mchakato wa kutengeneza katiba mpya. Tume ya kufanya kazi hiyo imekwisha kuteuliwa, kazi inaaza rasmi Mei mosi mwaka huu, yaani wiki ijayo tu. Ni matarajio yetu kuwa pamoja na mambo mengine ambayo yatazungumzwa katika kutafuta maoni ya wananchi kuhusu katiba yao, suala la Muungano litapewa nafasi ya kutosha.

Tunawachagiza wananchi wote watakaopata fursa ya kutoa maoni yao, wasisite kusema kile wanachotaka kuwepo katika muundo na uendeshaji wa Muungano huu, kwa kuwa ni kwa kuzungumza tu binadamu anafanikiwa kutatua matatizo yake hasa yanapokuwa yamejiegemeza katika mfumo wa kukinzana.

Tunawachagiza wananchi wazungumze kwa sababu tunaamini Muungano huu ni muhumu kwa watu wetu, faida za kuwako kwake ni kubwa zaidi kuliko kutokuwako, lakini ni vizuri zaidi kuwako huko kusaidiwe na kutatua kero zilizopo, ziwe za kimuundo, kimfumo au mazoea tu. Kila kitu kizungumzwe ili hatimaye tufikie makubaliano mema ya ustawi wa taifa letu na watu wake. Ni kwa jinsi hii tunarejea tena kauli yetu ya kuutakia Muungano huu maisha marefu zaidi na kuwapongeza wananchi wote kwa maadhimisho haya adhimu.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles