Tuesday May 21, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Wazungu wasiwe sababu ya machafuko Kenya

13th February 2013
Print

Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kutamka, wakati wa harakati za kutafuta Uhuru, kwamba kama Tanganyika (sasa Tanzania) haitakuwa kuwa kama Afrika yote haijakuwa huru. Fikra hiyo inaishi hata sasa.

 
Nimekumbuka nukuu ya Mwalimu Nyerere kipindi hiki ambacho nchi jirani na Tanzania, Kenya, inatarajia kufanya Uchaguzi Mkuu wake Machi 4, mwaka huu, kiasi cha majuma matatu kuanzia sasa.
 
Uchaguzi Mkuu wa Kenya ambayo kama ilivyo Tanzania, ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), utafanyika huku kukiwa na kumbukumbu ya vurugu, fujo na mauaji vilivyotokea baada ya uchaguzi kama huo, uliofanyika 2007 na kumuingiza ‘kibabe’ madarakani, Rais Mwai Kibaki.
 
Vurugu za Kenya hazikuishia ndani ya mipaka ya taifa hilo lenye nguvu kubwa kiuchumi kwa ukanda wa Afrika Mashariki, bali kwa nchi jirani ikiwemo Tanzania. Kwa maana hiyo, usalama wa Kenya ni usalama wa ukanda wa Afrika Mashariki kama ilivyo vurugu, fujo na athari zozote za kijamii kutokea, lazima ziiathiri Tanzania na nchi nyingine za EAC.
 
Kwa maana hiyo, amani na utulivu nchini Kenya ni jukumu la kila mdau katika EAC, kwamba kwa nafasi ya pekee, Wakenya wanapaswa kupewa fursa inayokidhi misingi na matakwa ya haki na demokrasia, kufanya uamuzi sahihi kuhusu Rais, mbunge, seneta, gavana, mwawakilishi wa wanawake na diwani wanaotaka, kupitia kura sita watakazozipiga siku hiyo.
 
Hatua hiyo pekee inayopaswa kutekelezwa kwa mujibu wa Katiba na sheria zinazohusiana na uchaguzi nchini humo, Kenya na Wakenya watabaki kuwa salama, wenye amani, utulivu na umoja wa kitaifa, pasipo kuingiliwa na matakwa ya mataifa ya nje.
 
Lakini hali ya hewa imeanza kuchafuka, baada ya mataifa kadhaa hasa ya Magharibi, kutoa matamko yenye kuashiria kwamba, yanatoa maelekezo ya kiongozi gani anayepaswa kuchaguliwa hususani katika nafasi ya Urais, vinginevyo ‘wakatishia’ kukata misaasa yao.
 
Nchi za Magharibi ni washirika wa karibu na muhimu katika masuala ya maendeleo barani Afrika ikiwemo Kenya, lakini namna wanavyotaka kuzitawala nchi za bara hili kupitia ‘kuwaweka madarakani’ viongozi wanaowataka, hakupaswi kukubalika, si kwa kizazi hiki pekee, bali milele na milele.
 
Nchi za Magharibi zimejikita kutumia misaada kama sehemu ya kutimiza matakwa yao, wakifanya hivyo zaidi kutokana na udhaifu wa watawala waliopo, kushindwa kubuni, kusimamia na kutekeleza matumizi sahihi ya rasilimali zilizopo, badala yake kuendelea kuwa ‘omba omba’ wenye kuwapigia magoti, ili mkono uende kinywani.
 
Hivi karibuni, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Johnnie Carson, alikaririwa akitoa onyo dhidi ya Wakenya, kwamba hawapaswi kuwachagua viongozi wenye mwelekeo wa moja ya Miungano ya kisiasa (ikitafsiriwa kuwa Jubilee). Kwa maana rahisi wanataka Rais atokane na Muungano wenye ushindani wa karibu na Jubilee ambao pasipo shaka ni Cord, iliyomsimamisha Raila Odinga maarufu kama Bwana Tinga.
 
Si Carson pekee aliyekaririwa akitoa karipio hilo, Ufaransa pia imekaririwa ikionyesha msimamo kama huo, lengo likidaiwa kuwatisha Wakenya, kwamba kama wakimchagua Uhuru Kenyatta (wa Jubilee) anayewania na mgombea mwenza, William Ruto, basi kuna uwezekano taifa hilo likakatiwa misaada ama kuisusia nchi hiyo!
 
Binafsi sina maslahi yoyote na Kenya isipokuwa katika uhalisia wa udugu, kwamba ndani ya EAC na Umoja wa Afrika (AU) kwa ujumla, tumo ndani ya vyombo hivyo.
 
Kenya ni majirani, Wakenya ni ndugu kutokana na muingiliano uliopo kiasi cha kusababisha wengine kuoa ama kuolewa, hivyo kuijenga familia yenye watu wenye asili ya nchi hizo mbili, wakawa wamoja.
 
Pia, ndani ya siasa za muingiliano, athari zozote za kisiasa, kijamii na kiuchumi zikiikabili Kenya, Tanzania na mataifa mengine ya EAC ama AU, hayawezi kubaki salama. Lazima yataathirika.
 
Kwa maana hiyo, inawezekana mtu binafsi kama Mashaka Mgeta, ama taasisi kama serikali za Magharibi, zisimhitaji mmoja ama wagombea kadhaa nchini Kenya, lakini Wakenya wakamuona ama kuwaona wanawafaa, hivyo kuwapigia kura ya ndiyo, yaani wanatosha.
 
Nikiwa rafiki wa Kenya na Wakenya, sipaswi kuwapinga, sipaswi kuwashinikiza, sipaswi kupanga na kushiriki njama za aina yoyote zitakazoivuruga nchi hiyo na raia wake. Kwa kufanya hivyo siwezi kuwa na haki ya kuitwa rafiki wa Kenya ma Wakenya, bali adui wao.
 
Ninachopaswa kukifanya katika ubinafsi ama nikiwa taasisi kama serikali za nje, ni ‘kufa kiume’ na kubadili mfumo na fikra zangu, kwamba kwa namna iwayo yote, Kenya na Wakenya ni bora kuliko matakwa na nguvu inayonishawishi kuathiri uamuzi na chaguo la Wakenya walio wengi.
 
Wapo wanaotumia kigezo dhaifu cha kesi kama zile zilizopo Mahakama ya Makosa ya Jinai (ICC) kule Hague, Uholanzi, kwamba inatosha kuwafanya wagombea, Kenyatta na Ruto kutochaguliwa! Ni ufinyu wa fikra na mawazo mgando yasiyolitakia bara la Afrika amani na utulivu wa kudumu.
 
Kwa maana Kenya ni Taifa lenye mifumo ya kisheria, inayoelezea bayana sifa za mtu anayepaswa kushiriki mchakato wowote wa kijamii, ikiwemo kuwania Urais. Iweje atokee asiyekuwa miongoni mwa Wakenya walioibuni, kuipitisha na kuitekeleza mifumo hiyo, awabague raia hao kwa kigezo hicho ambacho hata hivyo, bado kinaibua mjadala ikiwa kina maslahi kwa Waafrika ama wazungu wenye nia na mikakati ya kuendelea ‘kuitawala’ Afrika?
 
Matamko tofauti yanayotolewa na nchi za Magharibu ambayo raia wake wanajulikana kama  Wazungu, yanapaswa kutokuwa sababu ya kuibuka kwa machafuko nchini Kenya.  
 
Wanaweza kushauri katika mtazamo wa kushinikiza, wanaweza kufanikisha kupitia mbinu tofauti, lakini Kenya ikichafuka, hawatakuwa waathirika, wao na kizazi chao. Vurugu zikitokea wakiwa sehemu ya sababu zake, watatangaziwa kuondoka kuziepuka ghasia.
 
Wataondoka Nairobi, Mombasa, Kisumu, Eldoret, Turkana, Machakos, Vihiga, Sabatia, Kitale, Malindi na kwingineko kokote, wasionekane katika ardhi, warudi makwao. Kizazi cha waafrika wa Kenya ndicho kitakachokuwa waathirika wa kwanza.
 
Tusiombe Kenya ifikie ama kurejea katika hali hiyo na njia pekee ya kuinusuru ni kuwaacha Wakenya wafanye uamuzi sahihi ulio huru katika kuwachagua viongozi wanaowataka. Basi!
 
Mashaka Mgeta ni Mhariri wa Makala wa NIPASHE Jumamosi na Nipashe Jumapili. Anapatikana kupitia simu namba +6255 754 691540 ama barua pepe: mgeta2000@yahoo.com.
 
 
 
    
 
SOURCE: NIPASHE