

.jpg)
Nchi yoyote duniani kuwa na bandari yake ni bahati kubwa kwa sababu ni moja ya rasilimali kubwa sana ambayo ikitumika vizuri ina uwezo wa kuinyanyua kiuchumi kwa kuwa ni moja ya chanzo cha kuaminika cha mapato, kinachotakiwa ili unufaikaji huo utokee ni usimamizi mzuri na uwajibikaji.
Yapo mataifa ambayo ustawi wake unategemea zaidi bandari tu, kwa Tanzania bandari ya Dar es Salaam ingestahili kuwa moja ya vyanzo vikubwa vya mapato kwa ajili ya kukuza uchumi wa taifa hili, bandari hii ina sifa nyingi za kuwa kitovu kikuu cha usafirishaji wa mizigo kwenda na kutoka ughaibuni kwa nchi zote za Afrika Mashariki na Kati.
Kwa bahati mbaya sana hali ya mambo ilivyo katika bandari hii inatia aibu na kuchefuchefu, wizi wa mizigo umekuwa ni utamaduni bandarini. Katika safu hii tumekwisha kuandika mara nyingi juu ya wizi wa mizigo ya wateja katika bandari hii.
Ni nadra sana mtu kuagiza gari lake baada ya kudunduliza fedha zake litoke bandarini likiwa salama bila kunyofolewa vifaa mbali mbali kama redio, vitasa vya milango, jeki, tairi la akiba, vifaa vya kupandisha vioo, kutaja kwa uchache tu. Umekuwa ni kama utamaduni!
Ingawa kuna maelezo ambayo hata hivyo hayana uzito yanayotolewa na Mamlaka ya Bandari (TPA) kwamba udokozi wa vifaa hivyo hufanywa kwenye meli kabla mzigo hiyo haijafika bandarini, matukio ya kila wakati ya wizi unaoripotiwa bandarini hapo yanafanya fikra za kawaida kuhitimisha kuwa wizi ni jadi katika bandari hii.
Jana gazeti hili katika ukurasa wake wa tatu kulikuwa na habari iliyobeba kichwa kisemacho: Vigogo bandarini wadaiwa kuiba kontena la madini. Hii ni habari mbaya kwa watendaji wote wa bandari kwa maana ni katika kipindi kisichozidi miezi sita tu matukio makubwa ya wizi wa mali zenye thamani ya mabilioni ya fedha uliripotiwa tena kutokea chini ya mamlaka hiyo.
Vitendo vya wizi katika Bandari hii vinaendelea kushika kasi na kuisababishia serikali kukosa mapato yake kutokana na baadhi ya nchi na kampuni binafsi zilizokuwa zikiitumia kuamua kuikimbia kutokana na hasara wanayopata ya kuibwa kwa mizigo yao.
Katika tukio la hivi karibuni kabisa, kontena lenye madini aina ya tantalite yenye thamani ya zaidi ya Dola za Marekani milioni 10 sawa na Sh. bilioni 16, limeibwa. Habari zinasema kuwa madini hayo yanapatikana katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Rwanda na Burudi pekee na yamekuwa yakisafirishwa kutoka katika nchi hizo kupeleka nje kupitia Bandari ya Dar es Salaam.
Kutokana na wizi huo ambao Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wameandika katika nyaraka zao kuwa una thamani ya Dola za Marekani 22,000 sawa na Sh. milioni 35.2 umesababisha Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, kuagiza maofisa waliohusika wakamatwe na kufunguliwa mashitaka. Wizi huu siyo wa bahati mbaya, siyo wa mara ya kwanza, ni mfululizo wa uharamia wa kujipatia mali kwa njia ambazo siyo halali, lakini madhara yake yamekuwa ni makubwa mno kwa taifa kwa ujumla wake.
Kwa mfano, Waziri wa Uchukuzi akielezea hali hiyo kwenye mkutano wa waandishi wa habari juzi, alisema wazi kuwa kwa miezi minne serikali imekuwa ikipokea malalamiko kutoka serikali ya Rwanda kuhusu kuwako kwa mtandao wa wezi wa madini hayo katika Bandari ya Dar es Salaam.
Ni jambo la bahati mbaya kwamba badala ya Bandari hii kuwa mkombozi wa taifa hili kwa kusisimua sekta nyingine kama za usafirishaji na uchukuzi na kuvutia biashara kutoka mataifa mengine jirani kama Zambia, Malawi, DRC, Rwanda, Burundi na Uganda, inakimbiwa kutokana na mambo mawili makubwa; moja ambalo ni la kipekee wizi, la pili ufanisi duni wa kazi.
Haya ni mambo ambayo kimsingi hayakubaliki katika taifa masikini kama Tanzania linalohitaji kila nyenzo kuwakomboa watu wake kutoka katika lindi la umaskini. Tunajua kwa sasa kuna timuatimua kubwa sana imepita TPA, wapo walioachishwa kazi, wapo ambao wamepelekwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa hatua zaidi za kisheria, lakini pia wapo ambao uchunguzi wa utendaji wao uko kwenye uchunguzi; haya yakiendelea bado wizi unaendelea kufanyika bandarani.
Ni kwa kutambua aibu na hasara ambayo tunaipata kama taifa kwamba vitendo viovu vya wachache ndani ya shirika hilo vinatukwaza.Tungependa kuona udhibiti ukiongezeka katika bandari hii ili kweli iwe chanzo kikubwa cha mapato ya serikali ambayo yatasaidia kupiga vita umasikini wa nchi hii.