Thursday May 23, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Azam, Simba, Jamhuri zitavuna zilivyopanda

16th February 2013
Print
Maoni ya katuni

Timu tatu za Azam, Simba na Jamhuri ya Zanzibar zinacheza mechi za kwanza za michuano ya Afrika kati ya leo na kesho ambazo kwa namna ya ajabu tena mwaka huu zote zitaanzia nyumbani.

Azam leo inacheza na Al Nasir Juba ya Sudan Kusini katika mchezo wa Kombe la Shirikisho kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Jamhuri itacheza na St. Georges ya Ethiopia katika Ligi ya Klabu Bingwa kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba kesho.

Mabingwa wa Bara Simba na wazoefu wa michuano ya kimataifa watacheza pia kesho na Recreativo do Libolo ya Angola kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika pambano la Ligi ya Klabu Bingwa Afrika.

Tungependa, Nipashe, kuzitakia heri timu hizi katika michezo yake ya wiki-endi ya klabu ya Afrika ili zitoke viwanjani na matokeo mazuri. Zote.

Lakini, tunafahamu Nipashe, mpira wa sasa ni sayansi na mwanasayansi anayefanikiwa ni yule ambaye amefanya maandalizi mazuri maabara kabla ya kuingia kwenye 'mtihani' ulio mbele yake.

Hivyo pamoja na kupenda Azam, Jamhuri na Simba zizifunge timu za Sudan Kusini, Ethiopia na Angola na kujiweka katika mazingira ya kusonga mbele, tunajua kuwa ni maandalizi ya timu zetu kwa ajili ya mechi za leo na zile za marudiano baada ya wiki mbili, ndiyo yatakayoaumua ni nini zitavuna.

Tunafahamu kuwa Azam ilifanya ziara za mazoezi JK Kongo na Kenya na imekuwa ikifanya vizuri kwenye mechi za duru la pili la ligi kuu ya Bara.

Kama Azam, Simba nayo ilikwenda Oman ambako iliweka kambi ya wiki mbili ambayo haijaleta furaha ya kutosha kwa mashabiki wake baada ya kutoka sare mbili mfululizo na timu mbili za JKT.

Kuna habari chache sana zinazoelezea maandalizi ya Jamhuri lakini tuna hakika kuwa ilikuwa ikijiandaa vizuri hapa hapa.

Je, ziara ya nchi mbili za jirani ya Azam ambayo imekuwa timu pekee kushinda mechi zake zote tatu za mzunguko wa pili iliwawezesha wachezaji wake kuwa katika mazingira ya kuibuka na ushindi dhidi ya Al Nasir Juba leo?

Ndilo swali ambalo tunaweza kujiuliza, Nipashe, hasa ukizingatia ugeni wa Azam katika michuano ya klabu ya Afrika.

Faraja pekee ambayo tunapata, Nipashe, ni kuwa kutokana na upya wa Sudan Kusini hii pia ni mara ya kwanza kwa Al Nasri kucheza katika michuano hiyo hivyo ni msuli na akili za wachezaji wa Stewart Hall wakati wa maandalizi tu vinavyoweza kuwafanya Watanzania waamke kesho asubuhi wakiwa na matumaini mapya katika anga ya soka ya Afrika.

St George ni timu ambayo imekuwa ikishiriki mara kwa mara michuano ya klabu ya Afrika lakini kwa bahati nzuri, pia ni moja ya washiriki wa mara kwa mara wa Kombe la Kagame la klabu bingwa ya Afrika Mashariki na Kati hivyo kutokuwa katika nafasi ya kuwashangaza mabingwa wa zamani wa Zanzibar Jamhuri.

Lakini Jamhuri ilifanya maandalizi ya kutosha ya kimya kimya ya kuwa katika nafasi ya kupeperusha vizuri bendera ya Zanzibar kwenye Ligi ya Klabu Bingwa Afrika?
Sare mbili mfululizo zinaweza kuwa zimekatisha tamaa ya ushindi mashabiki wengi wa Simba ambao walitaraji kuona matunda ya timu yao kuishi kwa wiki mbili Oman ni 'dozi' mfululizo kwa timu pinzani kwenye ligi kuu ya Bara.

Lakini inapochukuliwa kuwa sare hizo ni dhidi ya timu za JKT ambazo zina sifa ya ukakamavu na maandalizi ya umakini kwenye makambi ya jeshi la kujenga taifa, ambacho Nipashe na mashabiki wa Simba tuna wasiwasi nacho ni kama mafunzo ya Uarabuni yalikuwa mazuri na yalipokelewa vya kutosha kuwezesha timu hiyo 'kuituliza' Libolo.

Kama mafunzo na mapokeo yaliyotolewa JK Kongo, hapa hapa na Oman yalikuwa mazuri vya kutosha timu zetu zitang'ara zikitupa karata za kwanza za michezo ya kwanza ya michuano ya klabu ya Afrika mwaka huu na tungependa iwe hivyo, Nipashe.


 
   
   
 








 

SOURCE: NIPASHE