Jengo la CCM wilaya ya Masasi mkoani Mtwara na pikipiki vikiwa vimeteketea baada ya vurugu na uharibifu wa mali uliotokea hivi karibuni
Mgogoro wa gesi umesababisha wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, ikiingia katika kipindi kigumu baada ya mji huo kukumbwa na vurugu zilizosababisha vifo na uharibifu wa majengo na mali za serikali na viongozi.
Ghasia hizo zilizotokea Januari 26 mwaka huu, zimeacha ‘makovu’ katika mji huo, kutokana baadhi ya maeneo yake kubaki na magofu ya nyumba na mabaki ya magari, vyote vikiwa vimetekea kwa moto.
Katika vurumai hizo, watu saba wamethibitishwa kufa na mali za watu kuchomwa moto ikiwamo nyumba za wabunge wawili kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mariam Kasembe na Anna Abdallah.
Pia ofisi ya CCM wilaya ya Masasi, majengo ya mahakama, magari 14 na ofisi za halmashauri zilichomwa moto.
TUKIO LILIVYOTOKEA
Inasadikiwa kwamba hakuna mkazi wa Masasi anayeweza kujitokeza hadharani kukueleza chanzo halisi za vurugu zilizosabisha hasara hiyo, lakini inaaminika kuwa zilihusiana na mgogoro wa gesi unaoendelea kufukuta katika mikoa ya kusini, hususani Mtwara na Lindi.
Vyanzo mbalimbali ndani ya Masasi vinazielezea vurugu hizo kutokuwa na nafasi kubwa ya kuhusishwa na masuala ya gesi, kwa sababu eneo haliguswi na hoja ya gesi kutokana na umbali uliopo kati yake na mjini Mtwara.
Abdallah Kaisi, ni mkazi wa Masasi anasema Januari 26, mwaka huu, alishuhudia vurugu ambazo hata hivyo, anasema hazikuwa ishara yoyote ikiwemo maandamano ya washukiwa wa uhalifu huo.
Badala yake, palikuwa na msafara wa pikipiki maarufu kama bodaboda na bajaji, uliohitimishwa katika kituo cha polisi, hali iliyowafanya baadhi ya wakazi wa eneo hilo kwenda kujua sababu ya kuwepo tukio hilo.
"Kama watu wanasema palikuwa na maandamano ya wananchi si kweli, mimi nilikuwa mmoja wa tuliokwenda kituoni pale baada ya kuona msafara mrefu wa pikipiki na bajaji ziliishia kituo cha polisi,"anasema Kaisi.
Anasema kituoni hapo, palikuwa na ‘kurushiana’ maneno kati ya askari polisi na madereva wa bajaji na bodaboda.
Mkazi mwingine, Mohamed Mrope anayemiliki bajaji, anasema madereva wa pikipiki na bajaji waliandamana wakiwa na madai halali, ingawa baadaye kuna baadhi ya watu ‘walioliteka’ tukio hilo na kuingiza ajenda zenye nia ovu.
Anasema lengo la madereva hao ilikuwa kupinga hatua ya polisi kumkamata dereva mwenzao, kwa kosa la kukutwa akikokota pikipiki yake katika barabara kuu.
Hata hivyo, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Masasi, Benueld Salamu anapingana na madai ya waandamanaji hao akieleza siku hiyo hapakuwepo dereva wa bodaboda aliyekamatwa.
"Siku ya tukio hatukumkamata mtu yoyote anayehusiana na pikipiki, hata walipokuja pale kituoni tuliwaambia hivyo, hawakutuelewa badala yake vurugu zilianza na kusababisha kuwepo hali mbaya zaidi," anasema Salamu.
MPANGO WA VURUGU
Vyanzo vinaeleza kuwepo mpango maalum uliowekwa na wanasiasa katika kuhakikisha wanapata nguvu zaidi kupitia ajenda ya gesi, ambapo imeelezwa kwa siku tatu kabla ya tukio hilo, walikutana kwenye hoteli moja mjini humo kujadili suala hilo.
Imeelezwa katika mkutano huo uliokuwa ukiwashirikisha baadhi ya viongozi wa vyama vya kisiasa, uliungwa mkono na moja wa Mbunge mmoja kupitia CCM anayewakilisha moja ya majimbo ya uchaguzi mkoani humo.
“Lengo la kikao hicho ambacho taarifa zake zinafanyiwa kazi kwa karibu na vyombo vya dola, ilikuwa kueneza mgogoro wa gesi ili kujenga taswira kuwa mkoa wote haukubaliani na suala hilo,” akasema.
Taarifa nyingine zinaeleza kuwa mkutano huo ulifanyika kwa siku tatu na ulihudhuriwa na watu kutoka sehemu mbalimbali ikiwemo Newala na Nachingwea.
Hata hivyo, haijulikana ni kwa namna gani maazimio ya mkutano huo yaliingizwa ama kuhusishwa na maandamano ya madereva wa bajaji na bodaboda.
YAFANANISHWA NA MILIPUKO BALOZI ZA MAREKANI
Kwa mujibu wa watu walioshuhudia matukio ya kuchomwa nyumba za wabunge wawili kupitia CCM, yalitekelezwa katika hali inayoashiria kupangwa, kama ilivyotokea katika milipuko ya balozi za Marekani jijini Dar es Salaam na Nairobi nchini Kenya.
Katibu wa Mbunge wa Masasi, Francis Charles anasema siku ya tukio, palikuwa na mkanganyiko wa mahali palipostahili kupewa msaada wa kuzima moto, kwa vile ilibainika nyumba zote zilichomwa moto na kutekekea katika muda mmoja.
Anasema kabla ya tukio hilo, madereva wa bodaboda walifika kwenye nyumba ya mbunge Mariam Kasembe wakihitaji msaada wake (Mbunge), kwa kile walichoeleza kuchoshwa na vitendo vya unyanyasaji wanavyofanyiwa na polisi wakati wakiwa kazini.
Anasema baada ya kutoa malalamiko hayo, mume wa Mbunge huyo, Mzee Omar Lada, alikubali kuwasaidia kwa kwenda kituo cha polisi ili kufahamu matatizo yao.
Hata hivyo, anasema wakati Mzee Lada akiwa kituoni hapo, kundi moja la watu waliingia kwenye nyumba hiyo na kuamuru watu wote kutoka ndani, wakieleza lengo lao kuwa ni kuchukua mali zao.
Charles anaeleza baadhi ya vitu ndani, walichukua mfuko wa takataka waliokuwa wamebeba wakatupia ndani ya nyumba pamoja na sehemu yalipoegeshwa matrekta mawili na gari moja aina ya Landcruiser, kisha kumwagia petroli waliyokuwa wamebeba katika kidumu kisha kuwasha moto.
Anaeleza wakati takataka hizo zikiwaka, kulitokea milipuko kama ya baruti na kusababisha moto kusambaa kwa kasi na kuteketeza nyumba na mali zote.
Anasema wakati nyumba hiyo ikilipuliwa kwa moto, majengo mengine yalianza kuungua moto katika muda huo na kusababisha wananchi wapate hofu na kuanza kukimbia hovyo kuokoa maisha yao.
"Hakuna aliyeweza kuja kutusaidi, wakati nawasiliana na mzee kumueleza nyumba inaungua moto ghafla nilishtukia moshi ukitoka ofisi za CCM, halmashauri na maeneo ya mama Anna," Charles anasema.
MBINU ZA KIJESHI ILITUMIKA
Imebainika kuwa mbinu iliyotumika katika vurugu za Masasi zilizosababisha uharibifu huo ni kama zile zinazofanywa na wanajeshi katika uvamizi, hivyo kusababisha uwezekano wa kuwepo ushauri wa kitaalamu wa jeshi katika kutimiza mpango huo.
Afisa upelelezi kutoka Makao Makuu ya Polisi, Isaya Mngulu anathibitisha kuwa kulikuwa na mpango maalum ulioratibiwa na watu maalum, kwa sababu katika siku ya tukio walionekana watu wamevalia kofia maalum ya kuzuia sura zisitambulike.
"Kuna watu walionekana wamevaa kininja siku ya tukio, kama kungekuwa na maandamano ya kawaida kusingekuwa na maandalizi kama yale," anasema Mngulu.