

Uwazi ni moja ya sifa zilizo kuu kwa tawala za kidemokrasia na zinazojali haki za binadamu. Uwazi ni miongoni mwa viashiria vya utawala unaokubalika kwa umma, ukatekeleza majukumu yake kwa niaba ya umma, ukiwa ni sehemu ya umma.
Uwazi unagusa maeneo mengi, kubwa zaidi yakiwa ni katika kujadili na kufanya uamuzi kwa masuala kama bajeti za nchi, kanuni, michakato ya manunuzi na matumizi ya rasilimali za umma.
Mambo mengine yanayochagizwa uwazi katika jamii ni kufanikisha vita ya rushwa na aina nyingine za ufisadi zinazoligubika taifa.
Kwa ujumla wake na mengine mengi yanayoweza kutajwa, yasitoshe katika eneo la safu hii, utawala unawajibika kwa umma, ukakubalika kwa umma, kwa sababu unatenda kwa kadri ya mahitaji ya umma.
Tofauti ya hapo, utawala na mifumo inayoongza nchi, ikishindwa kutekeleza japo hayo yenye kuashiria nia njema kwa nchi na watu wake, inakosa mamlaka ya kimaadili katika kuumiliki na kuuongoza umma.
Badala ya kutenda hivyo, utawala na mifumo yake utajikita kuhakikisha kuwa raia hawajui utendaji na uendeshaji wa nchi yao.
Utawala wa namna hiyo na mifumo yake utahakikisha raia hawapati taarifa sahihi zinazowahusu na kuhusu mustakabali wa nchi yao.
Inapofikia hatua hiyo, mtawala ataweka mbele maslahi ya chama cha siasa anachotoka, akizikumbatia vyombo vinavyotambulika katika mfumo wa utawala, huku akiukandamiza umma mpana.
Hali hiyo iliwezekana nyakati kama za Adolf Hitler alipoitawala Ujerumani na kujiongezea madaraka ya udhibiti wa kidikteta mwaka 1933.
Lakini kwa nyakati hizo zinazokabiliwa na mageuzi makubwa ya kiuchumi, kisiasa na kijamii, ambayo yanachochewa na utandawazi unaifanya dunia kuwa mfano wa kijiji, ni vigumu udikteta huo kutokea.
Kinachoshangaza, wapo baadhi ya viongozi, wenye zinazowaelekeza ‘mwaka 47’, kwamba pamoja na kuwa na macho, ni kama hawaoni, wana masikio, wanajifanya hawasikii. Wapo kama hawapo.
Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, ametoa kauli yenye fikra isiyoishi katika ulimwengu wa sasa, akipendekeza Bunge liteke haki ya Watanzania wanaokadiriwa kuwa zaidi ya milioni 44, wasipate taarifa sahihi.
Akionekana mfano wa Mfalme anayeitawala nchi na kudumu madarakani mpaka kifo chake, Dk. Kashilila, akatamka azma ya ofisi ya Bunge, kutaka kusitisha matangazo ya moja kwa moja kupitia runinga kutokea bungeni.
Kwamba kufanya hivyo, Bunge linaloendeshwa kwa kodi za wananchi, ‘liteke’ haki ya msingi ya raia kupata taarifa, isipokuwa zile ‘zinazochakachuliwa’, ziufikie umma!
Hapo ni dhahiri kwamba taifa linaelekea kukosa sifa ya kujiendesha kwa njia ya uwazi, linapoteza hadhi ya kusimamia misingi ya demokrasia, haki na amani.
Taifa lenye mifumo ndani ya utawala wake, inapojipambanua kwa nia dhaifu ya kupora haki ya umma kupata taarifa sasa, linaelekea kuwa ‘mfu’ kifikra. Haliziishi fikra zilizo hai zinazoendana na wakati.
Kwamba raia wake wasipate taarifa hasa zinazohusu mijadili na maamuzi kwa masuala kama bajeti za nchi, kanuni, michakato ya manunuzi, rushwa, ufisadi na matumizi ya rasilimali za umma!
Kama ningekuwa Dk. Kashilila, nisingediriki hata kwa sekunde moja, kufungua kinywa change ili nitoe wazo lenye athari hasi kwa nchi ambayo, hata nitakapo kufa, kizazi change kitabaki na kuishi katika ardhi ya Tanzania.
Iwe ni kwa mamlaka, shinikizo ama vinginevyo, kama ningekuwa Dk Kashilila, nisingeruhu dhamira yangu iwe kichocheo cha kuingia kwenye kumbukumbu chafu ya nchi, ile inayosifika duniani kwa utawala bora, demokrasia, haki na amani.
Kwamba itokee wakati wowote na mahali popote, jina langu, kama ningekuwa Dk. Kashililah, lingetajwa kwamba niliasisi kwa kutangaza wazo la kutaka kupora haki za binadamu, kupitia kuufanya umma usipate taarifa sahihi kutoka kwa wawakilishi wao bungeni, isipokuwa mpaka ‘zichakachuliwe.’
Ningeona fedheha, ningejisuta ndani ya nafsi yangu kama ningekuwa Dk. Kashililah, kwamba iwe ni kwa familia, kijiweni, kikao cha familia, nyumba ya starehe ama mbele ya waandishi wa habari kama alivyofanya, ningepata ujasiri wa kulitamka hilo.
Badala yake, ningejifunua kupata hekima, busara na maarifa kutambua kwamba Tanzania ni eneo la nchi ambalo halitapita, hata dunia itakapokamilika.
Kwa hali hiyo, kama ningekuwa Dk Kashililah, ningeiona Tanzania ni yenye maana sana kuliko kiti cha Ukatibu wa Bunge, kilichonipa fursa ya kutoa tamko lisilostahili, kutangaza azma yenye taswira ya kupora haki za raia! Sababu inayotolewa na ofisi ya Bunge kupitia kwa Dk Kashililah, kwamba udhibiti wa matangazo ya ‘live’ bungeni utasaidia kuwadhibiti wabunge wakorofi, haiingii akilini, kwamba imetoka kwa wasomi waliofuzu na kupewa dhamana ya kuliongoza Bunge.
Hivi ina maana viongozi hao hawajui kwamba kuna kanuni zinazowaongoza, zile zinazopaswa kusimamiwa kwa haki na usawa wenye kukidhi maslahi ya umma?
Hawajui kwamba udhaifu unaotokea bungeni huku kukiwa na kanuni ‘lukuki’ zenye kufaa na zisizofaa, kunatokana na udhaifu wa kiuongozi, hivyo moja ya njia ya kulinusuru hilo ni ujasiri wa kuwaachia wenye uwezo kukiongoza chombo hicho?
Kwa maana haiwezekani ofisi ya Bunge, kukusanya fikra, akili, mawazo, hekima na busara za Watanzania wote, na kusema ‘zinatekwa’ na wabunge kupitia upinzani, wale `wanaopakaziwa’ kashfa ya kuwa vinara wa vurugu bungeni.
Watanzania wanatambua ovu na njema kwa yanayotokea bungeni. Wanahukumu kwa kadri ya utendaji wa kila anayehusika na kwa hali hiyo, kila Mbunge ‘atabeba msalaba wake’
Kwa hatua iliyofikiwa na ofisi ya Bunge kupitia kwa Dk Kashililah, ninashawishika kuwapigia simu Spika Anne Makinda na Naibu wake, Job Ndugai. Nitawapigia kuwatahadharisha kwamba wasiipeleke Tanzania isipostahili kuwepo, bali waiche hapo walipoikuta kabla hawajazitwaa nafasi hizo zenye kupita, bali nchi itabaki na vizazi vyake.
Mashaka Mgeta ni Mhariri wa Makala wa gazeti. Anapatikana kupitia simu namba +255 754 691540 ama barua pepe; mgeta2000@yahoo.com.