Sunday May 26, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Mgogoro kuchinja usipopatiwa ufumbuzi, wanadini watagawana miji, mitaa!

17th February 2013
Print

Tangu kuibuka kwa mgogoro wa haki ya kuchinja kitoweo kati ya waumini wa dini ya Kiislamu na Kikristo, mkoani Geita, hivi karibuni, nimekuwa nikijiuliza maswali mengi, ambayo hadi sasa sijapata majibu yake!

Swali la kwanza ni hili. Hivi vitabu vya Biblia Takatifu inayoaminiwa na Wakristo na Kur’an Tukufu inayoaminiwa na Waislamu kuwa ndivyo mwongozo sahihi wa maisha yao ya kila siku, vimeanza kushuka mwaka huu, tena mkoani Geita?

Swali la pili. Kama hoja ni kuwa kuna kanuni au amri katika maandiko matakatifu ya vitabu hivyo kuwa wanadini wa upande mmoja wasile nyama iliyochinjwa na wanadini wa upande mwingine, mbona jambo hilo halikuwahi kusemwa toka zamani?

Swali la tatu. Kwanini mgogoro huo, ambao umesababisha kifo, majeruhi na upotevu wa mali zenye thamani ya mamilioni ya shilingi, utokee hivi sasa?

Swali langu hilo linaungwa mkono na kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, aliyoitoa Alhamisi wiki hii, mkoani Geita.

Kwamba anashangazwa na matukio hayo kutokea hivi sasa kwa kuwa hapo awali, haukuwapo kwa Watanzania utamaduni na chuki na vurugu.

Kwa kutopata majibu ya maswali hayo, ndipo ninapoona kuwa kuna haja na ulazima wa kufanyika uchunguzi wa uhakika na wa kina ili kubaini nini hasa kiini cha mgogoro huo.

Je, ni kuchinja au kuna kitu gani kilichojificha nyuma ya mgogoro huo kidini baina ya Waislamu na Wakristo nchini?

Kama kuna mtu, ambaye yuko nyuma anasokota kamba ya mgogoro huo, ajulikane na achukuliwe hatua za kisheria.

Kwani kuna hatari kubwa mbeleni kama mgogoro huo hautapatiwa ufumbuzi unaostahili na wa kudumu.

Nimejaribu kufuatilia kwa karibu hoja zinazotolewa katika kuhalalisha mgogoro huo.

Hoja kubwa kati ya zote ni kwamba, ni haramu kula nyama iliyochinjwa na wanadini wa upande mmoja kwa kuwa Mungu alinayetajwa na wanadini hao, hatambuliwi na wanadini wa upande mwingine.

Kama hoja ni hiyo, kwa uzoefu wangu, suala hilo haliishii tu katika kuchinja ng’ombe, mbuzi au kondoo kwa ajili ya kitoweo kinacholiwa na watu wa dini zote (Waislamu na Wakristo).

Suala hilo hutendwa na wafuasi wa dini zote kwa kila jambo wanalofanya katika maisha yao ya kila siku.

Huanza mambo yao kwa kutamka au kuashiria jina la Mungu wanayemwamini.

Kwa mfano, kama ni dereva wa basi la kwenda mikoani au daladala, huanza kuwasha gari hilo kwa kutamka au kuashiria jina la Mungu anayemwamini.

Kama ni hoteli, basi mmiliki atafungua asubuhi hoteli yake kwa kutamka au kuashiria jina la Mungu anayemwamini.

Na kama ni sokoni au dukani, muuza matunda na vyakula ataanza shughuli zake kwa kutamka au kuashiria jina la Mungu anayemwamini.

Sasa kama hoja ya mgogoro huo ni kuwa wanadini wa upande mmoja wanachinja kwa kutamka au kuashiria jina la Mungu, ambaye wanadini wa upande mwingine hawamtambui, itabidi wasiishie kwenye kutaka wawe na mabucha yao tu.

Katika kulaani vurugu zilizotokea, Waziri Nchimbi alitahadharisha kuwa kama suala hilo litafumbiwa macho linaweza kulipasua taifa vipande vipande.

Litapasua vipi taifa? Itabidi kila wanadini wawe na mabasi ya peke yao kwenda mikoani, daladala zao, hoteli zao, masoko yao na maduka yao.

Katika utaratibu huo mpya, itabidi sasa msafiri wa dini fulani akifika Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo (UBT) au kabla ya kupanda daladala aulize,

Je, dereva ni Muislamu au Mkristo ili asije akapanda basi lililowashwa kwa jina la Mungu asiyemtambua!

Kiuhalisia, utaratibu huo utakuwa mgumu sana.

Kwa hiyo, nchi ikifika hapo, itabidi sasa kila watu wawe na mabasi yao, maduka yao, hoteli zao nakadhalika.

Ili hilo liwezekane na watu wasibughudhiane, itabidi pia watu wagawane miji na mitaa!

Swali, ni je, watu wanaokuja na hoja kwamba, hawawezi kula nyama iliyochinjwa na watu wasiokuwa wa dini yao, hapa ndipo wanapotaka kuifikisha nchi?

Bado naendelea kutafakari jambo hilo, huku nikiendelea pia kusubiri kupata majibu ya maswali yangu hayo juu.

Nikitafakari jambo hilo na kusubiri kupata majibu ya maswali hayo, ningependa kutumia fursa hii kumpongeza Waziri Nchimbi kwa hatua yake nzuri ya kumteua Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi (SACP), Hezron Kigondo.

Kwamba ataongoza uchunguzi kubaini watu waliohusika na vurugu za mgogoro huo, ili kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria.

Waziri Nchimbi alichukua hatua hiyo katika ziara yake mkoani Geita, wiki hii. Ni matarajio ya Watanzania kwamba, ziara hiyo ya Waziri Nchimbi na ile ya Waziri Mkuu,

Mizengo Pinda, iliyotarajiwa kufanyika jana mkoani humo, zitatoa majibu ya maswali hayo, ikiwa ni pamoja na kuupatia mgogoro huo ufumbuzi wa uhakika na wa kudumu.

Muhibu Said ni Mwandishi wa Habari wa NIPASHE. Anapatikana kupitia simu namba 0717055551,0688055551, 0777055551 ama baruapepe: muhibu72@yahoo.co.uk

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI