

Wiki hii imekuwa ya kumbukumbu kubwa kitaifa, ambapo hatua za mwanzo za kugawa vitambulisho vya u-taifa kwa kila Mtanzania zilianza kwa kitambulisho cha kwanza nchini kukabidhiwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Kikwete akifuatiwa na viongozi wengine waandamizi wakiwamo mawais wawili wastaafu Mzee Ali Hassan Mwinyi na Benjamin William Mkapa.
Sherehe za kukabidhiwa vitambulisho vya u-taifa kama zilivyoshuhudiwa jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa wiki hii, zikifuatiwa na baadhi ya watendaji wa taasisi mbalimbali na wabunge ni ishara kuwa pazia la kuvigawa vitambulisho kwa wananchi wote nchini limefunguliwa rasmi kwa zoezi ambalo litakuwa endelevu.
Kimsingi, inatarajiwa kuwa wale wengine wanaoishi nchini kwa vibali maalum wakiwa si raia wa nchi hii pia watapewa vitambulisho maalum vinavyowatofautisha na wananchi wengine ambao ni raia wazawa.
Ni dhahiri kuwa sasa tunashuhudia hatua nyingine kubwa ya maendeleo kabla ya kuingia katika sherehe za miaka 52 ya Uhuru wa nchi yetu. Kutokuwapo kwa vitambulisho hivi kulichangia changamoto kadhaa ikiwemo wananchi kukosa viambatanisho muhimu vya kuwatambulisha, uhakiki wa taarifa za uraia, uhakiki wa taarifa za makazi, upungufu wa vifaa na Rasilimali watu.
Isitoshe, vitambulisho hivyo vitakuwa ushahidi mkubwa katika masuala yanayohusu haki na uwajibikaji katika nyanja mbalimbali za kidemokrasia ikiwa ni pamoja na haki ya kushiriki kupiga kura.
Mafanikio ya kuvipata vitambulisho hivyo yamepitia mchakato mkubwa ikiwa ni pamoja na serikali kuwekea mkakati na dhamira ya dhati ya kuhakikisha vinapatikana kwa muda uliopangwa ingawa ni kwa gharama kubwa.
Yote yamewezekana kutokana na mipango mizuri pamoja na uongozi thabiti wa Mkurugenzi Mkuu wa Vitambulisho (NIDA) Bwana Dickson Maimu ambaye alijitoa kwa juhudi na maarifa akisaidiana na timu yake wakati wa kutekeleza jukumu hilo muhimu kitaifa.Tunawapongeza sana.
Zoezi la utayarishaji wa vitambulisho lazima lilihusisha taasisi nyingi pamoja na wadau wengine katika sehemu za kazi, pamoja na wananchi wote ili kuhakikisha kuwa hakuna mwananchi aliyeachwa, kazi ambayo si nyepesi. Na tunaamini kuwa kwa msaada wa serikali zoezi hilo la kuwapatia watu wote nchini vitambulisho litafanikiwa.
Rais katika uzinduzi wa vitambulisho hivyo aliahidi serikali kuisaidia NIDA ili kabla ya uchaguzi wa mwaka 2015 watu wote wawe na vitambulisho vya Taifa vitakavyotumika katika uchaguzi huo.
Ni imani yetu kwamba vitambulisho hivyo havitatolewa kwa watu wasiotakiwa kama alivyoagiza Rais Kikwete na kwamba watakaokiuka sheria ya usajili wa vitambulisho hivyo wachukuliwe hatua za kisheria.
Zoezi hilo pia limesaidia kupata idadi halisi ya Watanzania ambapo takwimu zake zitasaidia kuwepo kwa jedwali la kumbukumbu za kila wakati likionyesha taarifa za mwelekeo wa uchumi kwa Watanzania waliosajiliwa na kuingizwa kwenye mgao wa vitambulisho vya taifa.
Kadhalika vitambulisho hivyo vitawasaidia sana wananchi kuwatambulisha wakati wa kuwekeana mikataba ya kijasiriamali pamoja na kupatiwa mikopo ya benki.
Serikali kwa upande wake itanufaika na mradi huu wa vitambulisho vya taifa kutokana na ukweli kuwa hata idadi ya walipa kodi watafahamika kirahisi na pia itakuwa rahisi kuwafuatilia wengine ambao kwa njia moja au nyingine wanaweza kuwa wanakwepa kuwajibika katika tozo mbalimbali za serikali.
Tunaamini kuwa wananchi wanafahamu umuhimu wa kutunza vitambulisho watakavyopewa zoezi likikamilika. Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein aliweka bayana hivi karibuni wakati wa kukabidhiwa vitambulisho kwa baadhi ya viongozi waandamizi wa serikali kuwa vitambulisho vya taifa ni haki ya kila Mtanzania, na kwamba ni utambulisho halali wa kumjua mwananchi halisi mzaliwa wa Tanzania.
Ni wajibu wa mamlaka zote zikisaidiana na NIDA kuwaelimisha wananchi sura halisi ya vitambulisho vya taifa ilivyo kusudi iwe rahisi kuvitofautisha na vingine vya udanganyifu endapo vitajitokeza. Wananchi wote kkwa upande wao wanapaswa kuwa wazalendo kwa kutoa taarifa zao kwa uaminifu na kutoa ushirikiano ili kurahisisha zoezi hilo.
Tunategemea pia kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, inaweza kufanya kazi kwa karibu na NIDA ili kuweka tathmini nzuri itakayopunguza gharama wakati wa chaguzi mbalimbali zinapofanyika.