Naibu Waziri wa Ujenzi Gerson Lwenge
Serikali imesema ni vyema mfumo wa kibenki ukatumika katika maeneo ya ukusanyaji wa mapato kwenye mizani za barabara nchini na kuwa na utaratibu wa kuwabadilisha wafanyakazi wa maeneo hayo ili kukomesha tabia ya wizi na vitendo vya rushwa vinavyoendelea katika maeneo hayo.
Naibu Waziri wa Ujenzi Gerson Lwenge alitoa agizo hilo jana wakati akifunga mkutano wa baraza la wafanyakazi wa wizara hiyo uliomalizika mjini hapa.
Alisema mfumo wa kibenki ukitumika vyema katika kukusanya mapato kwenye mizani badala ya ukusanyaji wa fedha taslimu unaotumika sasa utasaidia kuzuia wizi na vitendo vya rushwa vinavyodhalilisha wizara hiyo kwa sasa.
“Mtu anakuwa amekusanya Sh. milioni 5 anazo mkononi anaziangalia huku mfukoni mwake pengine hana hata hela, si anashawishika kuiba jamani’’ alisema Lwenge.
Alisema ili kuepusha vitendo vya rushwa kuna haja ya kuwahamisha wafanyakazi mara kwa mara badala ya kuwacha wakakaa muda mrefu katika eneo moja jambo linalowafanya kujenga mazoea na wateja.
Alisema serikali inajitahidi kudhibiti uharibifu wa barabara kwa kuweka kiwango maalumu cha uzito unatakiwa kupita katika barabara lakini watu wa aina hiyo wasio waaminifu wanatumia mianya hiyo kuwaruhusu na hivyo kuharibu barabara.