Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani
Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani, ameingilia kati mgogoro wa muda mrefu wa shamba la zaidi ya hekari 1,056 na kutishia kutoweka hali ya amani na utulivu baina ya wakazi wa kijiji cha Makorora kata ya Mashewa wilayani Korogwe na kampuni ya Katani kwa kuamua kugharamia upimaji wa mipaka ya shamba hilo.
Ngonyani ametoa ahadi hiyo baada ya wananchi wa kijiji hicho kutishia kuchukua sheria mkononi kwa madai ya kunyang’anywa ardhi yao na kampuni ya Katani.
“Ndugu zangu nawaomba msifike huko mnakotaka kufika….amani na utulivu ni vitu vya msingi sana ambavyo kwa sasa tunavihitaji kwa gharama zetu zote hapa nchini…hivyo gharama hiyo ya upimaji wa mipaka nitaiingia ili tu kila mmoja apate haki yake kisheria” alisema Mbunge huyo.
Awali wakizungumza kwa jazba katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Shule ya Msingi Makorora, wananchi hao walisema kitendo cha kampuni ya Katani kuchukua hekari 1,056 ambazo wamekuwa wakizitumia kwa shughuli za kilimo na makazi ni kuwatia umaskini ikizingatiwa wengi wao wanaendesha maisha yao kwa kutegemea kilimo.
“Sisi tunasikitishwa sana na kitendo hiki na tumechoka kwa sababu tunapuuzwa, kati ya maeneo yaliyochukuliwa hekari 336 ni za asili na hekari 720 ni za bega kwa bega idadi ambayo inafikia jumla ya hekari 1,056 ambazo ndiyo zilizochukuliwa na Katani ni haki kweli wakati watoto wetu wanaenda shule na kupata chakula kutokana na kilimo katika eneo hili hili”, alihoji Abdi Sechonge mkazi wa kijiji hicho .
Naye Abdi Rashed Sechonge akizungumza mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Mrisho Gambo, Ngonyani na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya, alisema hawako tayari kulifumbia macho suala hilo kwa kile alichoeleza maeneo hayo ni mali ya wananchi wa kijiji hicho.
Kwa upande wake, Gambo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa wilaya aliwataka wananchi hao kuwa na subira wakati serikali ikitafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hilo.
“Naomba muwe na subira wakati mimi na kamati yangu ya ulinzi na usalama ya wilaya tukitafuta ufumbuzi wa kudumu wa suala hili ikiwamo hatua za upimaji upya wa mipaka ya eneo hili…ndugu zetu wa Katani wapo hapa nao wameridhia uamuzi huu wa upimaji hivyo tusubiri tu majibu yatapatikana” alisema.