Unyama uliofanywa Zanzibar wa kumuua kwa kumpiga risasi tatu Padri wa Kanisa Katoliki akiwa njiani kwenda kuendesha misa juzi Jumapili asubuhi, umetikisa nchi na kuacha simanzi kubwa, lakini kikubwa zaidi swali kubwa likiwa halina majibu kwamba taifa hili kwa sasa linakwenda wapi kutokana na mivutano ya kiimani kuanza kushika kasi.
Matukio ya kushambulia viongozi wa dini hayajawahi kuwa utamaduni wa nchi hii tangu uhuru, ni sasa tu yameanza kuibuka matukio ya kutikisa mambo ya imani katika nchi hii tena kwa kasi na kiwango cha kutisha;
kwamba ndani ya kipindi kisichozidi miezi miwili viongozi wawili wa kiroho wameshambuliwa kwa risasi, mwaka jana mwishoni Padri Ambrose Mkenda alijeruhiwa kwa risasi mjini Zanzibar akirejea nyumbani kwake, juzi Padri Evaristus Mushi aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa njiani kwenda kanisani.
Kwa mujibu wa habari ambazo zimeandikwa na vyombo vya habari jana, matukio haya mawili yanafanana kwa karibu sana. Kwanza, walioshambuliwa ni viongozi wa kidini tena wote Wakatoliki, lakini pia staili ya ushambuliaji inafafana kwani kama ilivyokuwa kwenye tukio la awali, hili la pili washambuliaji pia walikuwa wamepanda pikipiki aina ya Vespa. Baada ya tukio walikimbia bila kupora chochote.
Kwa kawaida watu wanaotenda uhalifu kama huu wa Zanzibar wanakuwa na malengo mahususi, siyo wezi wanosaka mali. Majambazi hushambulia watu kwa silaha za aina mbalimbali ili kupora; anayeshambulia na kukimbia bila kuchukua chochote malengo yake ni makubwa na ya mkakati mahususi zaidi kuliko jambazi anayesaka mali kwa nguvu.
Ni kwa kutazama hali hii tunashindwa kujua kiini cha unyama huu ni nini hasa. Kwa hakika siyo kupora au kujipatia mali yoyote ya waliojeruhiwa na kuuawa, kwa sababu ingelikuwa hivyo basi mapadri hawa wangelikuwa wameporwa chochote.
Nia ni nje kabisa ya kupora. Tunasikitishwa na kuhuzunishwa na mauaji haya. Tunachukua fursa hii kuwapa pole wote walioguswa na mauaji haya mabaya ambayo yameharibu kabisa taswira ya taifa hili ambalo limejenga historia ya kipekee kwa watu wake kuvumiliana licha ya tofauti za kiimani miongoni mwa jamii. Tunasikitishwa kwamba historia hii ambayo imejengwa na kuwa utamaduni wetu kama taifa sasa inakanyagwa tu na watu wenye nia mbaya ya kupanda uhasama wa kidini nchini.
Tumesikia na kuona vyombo vya usalama vikijiapiza kwamba vitawasaka wote waliohusika na unyama huu, pia tumemsikia mkuu wa nchi akiahidi kwamba atatumia hata wataalam kutoka nje wenye ujuzi na weledi wa kubobea katika kuchunguza matukio ya kiuhalifu kama haya ili kuwasaka wote waliohusika na mauaji haya, tunasema yote ni mema, lakini jambo moja la msingi ni wananchi waone kweli hatua zikichukuliwa na wahusika kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba ndani ya nchi hii kuna watu wameanza kuonyesha kila aina ya dalili za kuchoka amani, wanafanya vituko vya kila aina kuonyesha kuwa wamechoka amani, hawa wamo wenye mamlaka ya kusimamia usalama wa wananchi, lakini pia wamo raia wa kawaida tu ambao kwa kulewa amani wanadhani wanaweza tu kujifanyia watakalo hata kama ni uchochezi, akili na mawazo yao ni kujenga fitina ndani ya jamii tena fitina za kiimani.
Hawa wanajulikana na wanafanya mambo haya wazi wazi, lakini hawafanywi lolote mpaka yatupate ya kutupata kama taifa ndipo tunaanza kukimbizana.
Bila kutaka kuingia katika mtego wa kunyoosheana vidole kwa sasa, tunaomba kuikumbusha jamii kwa ujumla wake kwamba sisi ni Waafrika kama Waafrika wengine wowote wa bara la Afrika; tusije kujidanganya kwamba eti sisi Tanzania tuna amani na kwa maana hiyo tunaweza tu kubweteka na kuacha vitendo vya kutuvuruga vikipaliliwa hadi kuota mizizi kiasi cha kuanza kuwaandama kwa mauaji viongozi wa dini. Hakika uvumilivu huu una mwisho, hakuna binadamu ambaye hachokozeki.
Kila binadamu ana machungu yake, yakimfika mahali naye hujibu mapigo, tunaomba sana sana wenye dhima ya kusimamia usalama wa nchi hii na wenye mamlaka ya umma wasiruhusu taifa hili lifikishwe huko. Tunaomba watu wote wenye mwelekeo wa kuchochea chuki, ghasia na mauaji kama haya tunayoshuhudia Zanzibar wadhibitiwe kwa mkono wa nguvu ya kutosha wa dola.
Tulifikiri kwamba baada ya tukio la mwaka jana Desemba la shambulizi dhidi ya Padri Mkenda vyombo vya usalama vingefanya kazi yake sawasawa, havikufanya hivyo; tunadhani baada ya damu na kifo kutokea tena walau sasa tutajifunza kutokana na makosa yetu wenyewe kwa kuhakikisha kwamba wahusika wote na makundi yao yote wanaopanga ushenzi kama huu uliotokea Zanzibar wanakomeshwa milele.
Tunataka hali hiyo iwakute kwa sababu tunataka Tanzania iendelee na utamaduni wake wa watu wake kuishi kwa kuheshimiana na kuvumiliana licha ya tofauti za kidini. Dola ifanye kazi yake sawasawa.