

.jpg)
Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imetupilia mbali maombi ya wagombea uongozi katika shirikisho hilo na bodi ya ligi (TPL) ya kupitia upya maamuzi iliyoyatoa juu ya rufani zao na kuwataka wahusika kwenda kwenye Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS).
Baada ya kamati hiyo kutangaza kuwaengua baadhi ya wagombea katika kinyang’anyiro hicho Jumatatu ya wiki iliyopita, rais wa TFF anayeondoka madarakani, Leodegar Tenga aliwaambia waandishi wa habari kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuwa walioenguliwa wanayo fursa ya kuiomba kamati ya rufani ya uchaguzi ya TFF kupitia upya maamuzi yaliyotolewa dhidi yao kabla hawajaenda FIFA na baadaye CAS.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za makao makuu ya TFF zilizopo Karume, Dar es Salaam jana, mwenyekiti wa kamati hiyo, Idd Mtiginjola alisema kamati yake haiko tayari kupitia upya maamuzi yake kwa sababu hakuna utaratibu huo kwenye katiba ya TFF na kanuni za uchaguzi za shirikisho hilo.
“Tenga ni rais wa TFF, si mwanasheria. Kamati hii inaongozwa na wanasheria. Sisi tuna taaluma zetu. Hatuwezi kupitia upya maamuzi tuliyoyatoa kwa sababu hakuna kipengele ndani ya katiba ya TFF na kanuni za uchaguzi za TFF zinazoturuhusu kufanya hivyo,” alisema Mtiginjola.
Alisema kuwa kamati yake ilikutana jana asubuhi na kujiridhisha na suala hilo lililoibuliwa na rais Tenga, lakini haikuona kifungu chochote cha kanuni za TFF kinachoiruhusu kuridhia maombi ya wagombeaji hao, hivyo yeye na wajumbe wengine wawili wa kamati hiyo, Kamanda Mohamed Mpinga na Francis Kabwe, waliamua kuyatupilia mbali maombi hayo.
Aidha, Mtiginjola alisema kuwa maamuzi yaliyofanywa na kamati yake dhidi ya wagombea waliofikishwa mbele yao yamefuata misingi ya kisheria na kwamba hakuna ‘unazi’ wowote ulitotumika.
“Ni kweli niliwahi kufanya kazi kwenye mahakama moja na Jumanne Nyamlani (mgombea pekee urais TFF), lakini mimi na yeye tulikuwa waajiriwa wa serikali. Mahakama ile haikuwa ya Nyamlani au yangu. Mbona hata Michael Wambura nimesoma naye Mzumbe na ni rafiki yangu?” Alihoji Mtiginjola.
“Watanzania waelewe kwamba hakuna urafiki wala undugu katika maamuzi ya kamati hii, ni kanuni tu. Hatuangalii mtu hapa,” aliongeza Mtiginjola huku akiwaonyesha waandishi wa habari saini ya Agape Fue kwenye barua ya pingamizi dhidi ya Jamal Malinzi lililozua gumzo nchini.
MALINZI ANENA
Akizungumza na NIPASHE jijini Dar es Salaam jana, Malinzi alisema amesikitishwa na maamuzi ya kamati hiyo na kwamba leo ataweka wazi hatua atakazochukua.
“Nimepata taarifa hizo za kusikitisha lakini kwa leo (jana) naomba nisizungumze chochote. Kesho (leo) nitawaeleza hatua inayofuata baada ya maamuzi hayo,” alisema Malinzi ambaye pia ni mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoani Kagera (KRFA).
‘TENGA AJIUZULU’
Katika hatua nyingine, mgombea wa nafasi ya makamu wa rais wa TFF, Michael Wambura aliliambia gazeti hili jana kuwa rais Tenga anapaswa kuachia ngazi ama kuifuta kamati ya Mtiginjola.
“Tenga alisema Jumamosi kuwa kuna hatua tatu zinapaswa kufuatwa ikiwamo ya kuiomba kamati ya rufani ya uchaguzi ya TFF kupitia upya maamuzi yake. Leo (jana) kamati hiyo inasema utaratibu huo haupo. Kwa maana hiyo Tenga aliwadanganya Watanzania, ajiuzulu,” alisema Wambura.
“Kama utaratibu huo haupo, Tenga anapaswa kuwajibika kwa kuachia ngazi. Na kama utaratibu huo upo, aitishwe haraka mkutano wa kamati yake ya utendaji iivunje kamati ya rufaa ya uchaguzi ya TFF. Mambo gani haya?” Alihoji Wambura.