Sunday May 26, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Barua kwa waheshimiwa wa Takukuru-2

19th February 2013
Print

Ukurusa huu mpya wa barua hii ni mwendelezo  na hitimisho la barua niliyoanza kuiandika wiki iliyopita kuhusu  taasisi hiyo  kutokuwa na uwezekano wa  kuidhibiti tabia ya ufisadi, achilia mbali kuiondoa kabisa . Naona ni kama  jambo lisilowezekana.

 
Ndugu wananchi wenzangu, ninashukuru kuwa hata Mkurugenzi wa Takukuru, baada ya barua yangu wiki iliyopita, alikiri kuwa wanasiasa wamekuwa ni kikwazo, achilia mbali watendaji wenzake vingunge katika ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali.
 
Niliandika kuwa wanasiasa wamekuwa ni kikwazo, lakini Mkurugenzi wa Takukuru ametaja wazi kuwa wanasiasa wamekuwa na mbinu za kuhalalisha ufisadi, na hasa rushwa, kwa kuremba remba maneno na kuiita takrima, hahahaha! Nilikwambia, lakini mheshimiwa Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru  nakumbuka walishatunga sheria ya Takrima kuipatia rushwa uhalali wa kisheria. Lakini  tunashukuru  wajanja wakaja kuifuta.
 
Lakini  Mheshimiwa, nikiendelea  pale nilipoachia kuhusu viongozi. Nilizungumza  wafanyakazi katika idara nyeti kuwa na miradi halali ya kibiashara lakini uwezekano wa kutumia mbinu zisizo halali kuziendesha biashara hizo ni mkubwa. 
 
Nikaonyesha hofu kuwa uwezekano wa sisi watato wa vigogo kukamatwa na Takukuru, polisi au Idara za usalama wa taifa unaweza kuwa ni sifuri kabisa. Natoa mfano hapa katikati kulikuwa na hekaheka ya Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (NEMC)  kutaka kuvunja nyumba ya Mama, mchungaji, Dk. Getrude Lwakatare, kwa kuijenga ufukweni kinyume na sheria ya utunzaji wa pwani zetu. 
 
Awali niliwaunga mkono NEMC,  lakini baada ya kusafiri mkoa fulani wa pwani huko kusini nikashuhudia baa moja imejengwa pembeni ya ufukwe. Na  nyumba ya ghorofa nayo inaibukia hapo kando ya baa hii ambayo kila sikukuu ikifika watu wanajazana na uchafu unaenda baharini, ati hiyo ghorofa mpya itakuwa night club, ufukweni mwa bahari, mita hamsini sidhani zinavuka. 
 
Nikajiuliza mbona hapa nikikaa kwenye seng’enge maji ya bahari yakitaka kuja kutembelea nchi kavu yananigusa kwenye ndala zangu kila wimbi linapopiga.  Nikila mchemsho nikataka kusukutua ushombo wa chakula natemea kwenye bahari;  mbona huyu yuko karibu zaidi na bahari kuliko hata Mama Lwakatare.
 
 Inakuwaje hakamatwi, haulizwi, vipi tena. Na nasikia mtu huyu amejenga pembeni ya ikulu ndogo ya Mheshimiwa Rais mkoani hapo, na hili nalo tulidhani kuwa si vyema likawa kwani tunampenda rais wetu.  Akifika hapo akae kwa amani na utulivu, sasa vuguvugu la walevi na kelele za magari zikimkera atafikiriaje matatizo ya wanaogambania shingo za wanyama, wanaotaka kuchoma nyumba za wenzao, wanaotaka kula chakula maana Kilimo Kwanza kimefeli. 
 
Nikaambiwa kuwa Takukuru hawawezi bwana kumkamata kibopa huyo, maana ni mtoto wa wenyewe. Na wafanyakazi wa Takukuru ni watoto wa wakulima wanaojifanya wanaipenda sana nchi hii na watu wake. Wajaribu kumkamata mtoto huyu wa wenyewe, kesho yake wao na mkurugenzi watarudishwa vijijini kuchuma maboga, sasa na njaa hii itakuwaje.
 
Ndugu wa Takukuru, kama nilivyosema wiki iliyopita katika waraka wa awali  achilia mbali wakubwa wenyewe na mambo yao huko juu; tunaona pia watoto wa wakubwa wanaanzisha biashara hii, biashara ile, na hakuna anayeweza kuwakamata. Maana, kama nilivyosema pia, utatukamataje sisi watoto wa baba aliyewaajiri ninyi wote wa Takukuru. 
 
Matokeo ya yote hayo ni kuendelea kutumia nyavu za matundu madogo, maana hamuwezi kuendesha meli zinazotumia kokoro na nyavu kubwa kunasa papa, nyangumi na wengine ambao sisi wananchi tunawahitaji hasa ili tuweze kuhalalisha matumizi ya kodi zetu.
 
Hivi inakuwaje lakini, mheshimwa mkurugenzi, unapoona kuwa rushwa imekuwa sasa sehemu ya maisha. Kila mwananchi akipeleka mgonjwa wake hospitali anaondoka na fedha  ya kumuona daktari na ya kumlipia bakshishi nesi; kila polisi anapokukamata hataki mwende kituoni, ila ufungue pochi; kila msichana anapoenda kazini au kwenda kuomba kazi, anakwenda na kondomu maana anajua ataombwa rushwa ya ngono, tena sio mbali na ofisi, humo humo ofisini mwa mtoa na muidhinisha ajira. Lazima awe na kondomu. 
 
Ashakum si matusi wasomaji, lakini nazungumzia kitu ambacho nakijua kinatendeka na wananchi sasa tunaona usipofanya hivyo huwezi kupata kile ambacho ni haki yako na halali yako, lakini tunachokisema ni kuwa, kila mbuzi atakula kwa urefu wa kamba yake.
 
Kwa hiyo ninyi wa Takukuru mkija kunikamata, mkavuta kitu kidogo, na mimi mwalimu nikiombwa kuvujisha mtihani, naomba kitu kidogo, na daktari akimvusha foleni mgonjwa anayempenda kwa ahadi ya kitu kidogo, wote tunakula kwa urefu wa kamba zetu, sisi wote ni mbuzi. 
 
Rushwa sasa ni mfumo, ni itikadi, imeingia na kujikita katika akili na tabia zetu, sio kitu kigeni, na kwa kweli tunawashangaa nyie watu wa Takukuru kuendelea kula kodi zetu kudhibiti kitu ambacho sisi tumeamua kuwa ni sehemu ya maisha.
 
Naomba niishie hapo, Wasalaam Aleikhum
Ckayoka28@yahoo.com, 0766959349
 
SOURCE: NIPASHE