Friday May 24, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Mapori yasiyoendelezwa yachangia migogoro ya ardhi Morogoro

19th February 2013
Print

Mkoa wa Morogoro ni mingoni mwa mikoa inayokabiliwa na  tatizo la  migogoro ya  ardhi ambayo mara kadhaa yamelipuka mapigano kati ya wafugaji na wakulima na kusababisha nyumba kuchomwa,watu kujeruhiwa na baadhi kufa.

Mkoa una  mashamba pori  220 ya vigogo ambayo hayaendelezwi huku serikali ikishindwa kuchukua hatua  za haraka  kulipatia ufumbuzi suala hilo.

Mashamba hayo yamekuwa chanzo cha migogoro na kikwanzo cha utekelezaji wa agizo la rais la kuufanya mkoa huo kuwa ghala la taifa la chakula.

Rais Jakaya Kikwete alipofanya ziara mkoani Mororo  alitoa agizo hilo la mkoa huo kuufanya kuwa ghala la chakula akiamini kuwa  una ardhi  na rutuba ya  kutosha kuzalisha chakula cha kukidhi mahitaji ya mkoa na  nchi.

Morogoro iliingizwa  kwenye  kundi la mikoa sita inayozalisha chakula kwa wingi nchini.
Mgawanyo mpya wa mikoa uliofanywa hivi karibuni umechangia  ongezeko la mikoa hiyo hadi kufikia mikoa saba.

Mikoa hiyo ni  Mbeya, Ruvuma, Rukwa, Njombe, Katavi, Iringa, Kigoma na Morogoro.
Ili kufikia kusudio hilo,  Morogoro iliweka mpango maalum ujulikanao kama Fanya Morogoro kuwa  Ghala la Taifa la Chakula (Famogata).

Hata hivyo, mpango huo umekuwa ukisuasua kutokana na changamoto nyingi ikiwemo  ardhi kubwa kumilikiwa  na vigogo wanaoshindwa kuiendeleza.
Kaimu Katibu tawala (Uchumi na fedha) mkoa wa Morogoro, Lamiki Noah, aliwaambia wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha na Uchumi iliyotembelea mkoa huo wa  Morogoro kuwa mashamba ya vigogo ambayo pia yanajulikana  kuwa ni mashamba pori yaliyoachwa bila kuendelezwa kwa miaka mingi yamekuwa kikwazo cha utekelezaji wa Famogata.

Morogoro ina  eneo la kilomita za mraba 73,039. Na  eneo la hekta 2,226,396 za ardhi zifaazo kwa kilimo sawa na asilimia 30.43 ya ardhi yote.

Kutokana na hali hiyo,  ikiwa ardhi ifaayo kwa kilimo itagawanywa kwa usawa kila mkazi wa Morogoro atapata mgao wa ekari 3.12 za ardhi hiyo.

Kutokana na eneo kubwa la ardhi hiyo kuchukuliwa na wawezekezaji na vigogo serikalini, kupanuka kwa makazi ya watu na ogezeko la kasi la idadi ya mifugo kumesababisha migogoro mingi kutokana na  uhaba wa ardhi.
Inakadiriwa kuwa mkoa wa Morogoro una zaidi ya ng’ombe 1,222,373 (Sensa 1988). Wataalam wanasema kuwa ng’ombe mmoja anahitaji ekari moja na robo kwa ajili ya malisho yake kwa mwaka.

Kutokana na mahitaji  makubwa ya mahitaji ya  ardhi  ya  malisho ya mifugo, kilimo na makazi  kumekuwa kunaibuka migogoro mingi  hasa  baina ya wakulima na wafugaji kwa upande mmoja na wananchi na wawekezaji kwa upande mwingine.

Migogoro hiyo imeshamiri  zaidi katika wilaya za Kilosa, Kilombero, Mvomero, Morogoro na Ulanga. Wakulima na wafugaji hugombea ardhi ndogo iliyopo.

Kuwepo kwa mashamba pori zaidi  ya 220 ya vigogo umekuwa ukizua vurugu kwa sababu  wananchi wengi hukosa ardhi kwa ajili ya kilimo hulazimika kuyavamia mashamba hayo yaliyodumu kwa  muda mrefu bila kuendelezwa ili yatumike kuzalisha chakula kwa ajili ya  kukidhi mahitaji yao.

Katika siku za hivi karibuni  kaya zaidi ya 50 za wakazi wa kitongoji cha  Mateteni kata ya Mbigiri wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro walijikuta wakipata hifadhi kwenye  mahema baada ya nyumba zao kuvunjwa kwa tingatinga na watu waliodai kuwa ni madalali wa mahakama waliotumwa na aliyekuwa katibu mkuu kiongozi wa utawala wa awamu ya kwanza, Thimos Apio.

Tukio hilo lilikuja  baada ya familia hizo  awali kukumbwa na mafuriko na uongozi wa mkoa wa Morogoro kuamua  wahamishiwe  katika eneo la mwinuko lilipo shamba la ( Apiyo) ili kujistiri kwa muda wakati serikali ikifanya jitihada za kuwatafutia eneo jingine la kudumu.

Uvunjaji huo usiozingatia utu umesababisha familia kuishi kwenye mahema yaliyotolewa na aliye kuwa mkuu wa wilaya hiyo, Halima Dendego, baada ya kupata taarifa za tukio hilo.

 Mahema hayo yanayotoa hifadhi  dhidi ya mvua na jua, lakini hayana  staha kwa sababu  baadhi ya familia zinalazimika kuishi katika hema moja pasipo kujali jinsi na mahusiano yao.
Licha ya  Apiyo, pia wapo  viongozi wengi  wanaotajwa  kumiliki mashamba makubwa  mkoani Morogoro wakiwemo, marais wastaafu , Ali Hassan Mwinyi na  Benjamin Mkapa.
 
Wengine ni mawaziri wakuu Fredrick Sumaye na  John Malecela, mawaziri, wabunge na
baadhi ya viongozi  wa serikali.
Mashamba yanayomilikiwa na vigogo hao yametajwa kuchangia  migogoro ya ardhi isiyoisha katika mkoa wa Morogoro, hasa kwa sababu  idadi kuwa ya wananchi hawana  maeneo ya kulima hali inayowalazimu kuyavamia mashamba ya vigogo hao hususan yasiyoendelezwa.


Hali katika kijiji cha Kikundi tarafa ya Mkuyuni  inatatiza kutokana na kukithiri kwa mgogoro wa muda mrefu wa ardhi kutokana na hatua ya wananchi wa kijiji hicho kupinga kampuni ya Morogoro Agro-Enterprises ya mhadhiri wa Chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Prof. Martin Shem kuwaondoa kwa nguvu kutoka katika shamba la Kidago lenye ukubwa wa hekta 1080 linalodaiwa kuwa analimiliki.|

Shamba hilo limekuwa linalimwa na  wananchi hao  kwa miaka mingi.
Hali hiyo imesababisha familia zaidi ya 300 zilizokuwa zikilitumia shamba hilo kwa zaidi ya miaka 30 kutaabika kwa kukosa eneo la kulima, huku wakiambulia kupigwa na walinzi wa kampuni hiyo na kufunguliwa kesi za mara kwa mara na mmiliki huyo. Wananchi wamekuwa wakilalamikia sana hatua hiyo.|

Mkoa  baada ya kubaini  kiini cha migogoro mingi ya ardhi uliamua kubainisha mashamba yote yasiyoendelezwa yaliyobakia kama mashamba pori kwa muda mrefu ili kumwomba rais mwenye dhamana ya ardhi kwa mujibu wa sheria  kubadilisha matumizi ya mashamba hayo.

Hata hivyo, Rais Jakaya Kikwete  wakati akizungumza na waandishi wa habari  Ikulu
jijini Dar es Salaam alisisitiza kuwa hatakuwa tayari kubadilisha matumizi ya ardhi yoyote iliyomilikiwa kihalali hadi atakapopewa sababu za kuridhisha za kubadilisha matumizi hayo.
Kwa upande wake  mkuu wa wilaya ya Morogoro Said Amanzi akizungumza katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) kilichofanyika mwishoni mwa mwaka jana alisema kuwa rais ametaka orodha ya mashamba yaliyodumu muda mrefu bila ya kuyaendeleza  na kuyatathimini  upya kabla ya kupeleka tenda kwa rais.

Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Joel Bendera, akitoa msimamo wake kuhusu migogoro ya ardhi katika mkoa wake alisema kuwa, anakusudia kuitisha kikao cha wadau wote ili kwa pamoja watafute ufumbuzi wa migogoro hiyo na kwamba hiyo ndiyo njia pekee itakayosaidia kupunguza madhara yatokanayo na migogoro hiyo.
“Sipendi kufanya mambo nusunusu.Nimemaliza  tatizo la ujenzi wa vyumba vya madarasa na watoto wote waliofaulu watakwenda shule. Baada ya  sasa nguvu nazielekeza kwenye migogoro ya ardhi. Nataka kukutana na  wadau ili kutafuta  chanzo na suluhisho la migogoro hiyo,” alisema Bendera.
 

SOURCE: NIPASHE