

.jpg)
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Mkoani Singida, Manju Salumu Msambya, ameilalamikia Hazina kuwa ndiyo kikwazo kikubwa cha kutolipwa mishahara yake ya miezi miwili anayoidai serikali.
Msambya alitoa shutuma hizo kwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi (Tamisemi), Kassimu Majaliwa, kwenye kikao maalum kilichoandaliwa kwa watendaji wa Idara ya Elimu na kufanyika mwishoni mwa wiki kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida.
Aidha, Mkuu wa wilaya hiyo mpya alibainisha kuwa kwa zaidi ya miezi tisa sasa amekuwa akidai mishahara yake hiyo bila mafanikio huku akiwa ameshawasilisha Hazina nyaraka zote muhimu zinazotakiwa.
Kwa mujibu wa Msambya ambaye katika kikao hicho alikuwa amekaimu nafasi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, licha ya kudai mishahara ya Mei na Juni, mwaka jana, lakini ameshangazwa na watendaji wa Hazina kumlipa mishahara mingine yote ya kuanzia Julai,2012 hadi sasa.
Msambwa alisema kuwa madai yake ya mishahara hiyo yalishawasilishwa pia kwa Katibu Tawala wa Mkoa huo, lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa kutatua tatizo lake.
“Waswahili wamesema ukimwona Jumbe basi usisahau kuwasilisha matatizo yako yote....kwa hali hii Mheshimiwa Naibu Waziri wa Tamisemi, naomba nawe unifikishie kilio changu hiki kwa wahusika huko juu,” alisema huku akimwangalia Naibu Waziri wa Tamisemi.
“Mimi tangu nilipoteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Mkuu wa wilaya ya Ikungi, mishahara yangu ya mwezi Mei na Juni, mwaka jana bado sijalipwa mpaka leo, lakini utashangaa kuona sina madai ya mishahara mingine ya miezi ya mbele,” alifafanua.
Katika kikao hicho ambacho kililenga kuwakutanisha watendaji wa sekta ya elimu Mkoa wa Singida na Naibu Waziri wa Tamisemi, Msambya alimwomba Naibu Waziri huyo kufikisha ujumbe huo Tamisemi ili wafanye mawasiliano na Hazina.
Katika hatua nyingine, Msambya alimweleza pia Naibu Waziri Majaliwa kwamba yeye amekuwa kikwazo cha utekelezaji wa shughuli za afisa elimu wa wilaya ya Singida kutokana na kulihodhi gari lake alilokuwa akilitumia kwenye ufuatiliaji wa shughuli za idara hiyo. “Kwa kweli Mheshimiwa Naibu Waziri umesema magari ya elimu yasikae ofisini bali yaende vijijini, lakini sasa mimi nimemkwamisha afisa elimu wangu wa wilaya kutokana na kulihodhi gari lake maana mimi bado sijapata gari la kufanyiakazi zangu,”alisisitiza huku akimwangalia Afisa Elimu wa Wilaya akiangua kicheko.
Msambya alimwomba Naibu Waziri Majaliwa kuiona hali hiyo ambayo alisema inaweza kuathiri utendaji wa afisa elimu wa wilaya hiyo na hivyo ingekuwa vyema serikali ikachukua hatua za makusudi na za haraka ofisi hiyo kupewa gari.