


Kampuni ya utalii ya Leisure Tours na Holidays Limited, iliyokuwa imewasilisha mahakamani ombi la kutaka kuuza jengo la Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) ili kujilipa deni la dola za Marekani 716,259.52 (takriban Sh. bilioni 1.2), ambalo linadaiwa kwa kampuni hiyo tangu mwaka 2008 imetakiwa kufanya kwanza uthamini wa jengo hilo.
Amri ya Mahakama Kuu (Divisheni ya Biashara), ya Februari 11, mwaka huu ,iliyotolewa na Jaji Robert Makaramba, imezielekeza kampuni hizo kufanya tathmini ya thamani ya jengo la ATCL lililopo Mtaa wa Ohio katikakati ya jiji la Dar es Salaam.
“Walalamikaji wanatakiwa kuwasilisha thamani ya jengo hilo mahakamani leo kabla ya maamuzi mengine, ambayo yatatolewa Februari 25, mwaka huu,” ilieleza sehemu ya amri ya mahakama.
Kwa mujibu wa walalamikaji, deni hilo lilitokana na ukodishaji wa magari yaliyokuwa yanatoa huduma za ATCL.
Ilidaiwa Januari 16, 2008, ATCL ilikubali deni la dola za Marekani 313,759 na ikakubali kulilipa kwa awamu tatu kuanzia Februari hadi Aprili, 2008, lakini baadaye kampuni hiyo ya utalii iliandika barua kwa ATCL iliyodai deni ni dola za Marekani ni 321,016.
Machi 31, 2008, kwa mujibu wa mlalamikaji aliwasilisha hati za madai kwa ATCL kuwa deni lilikuwa limefikia dola za Marekani 367,097, ambalo ni pamoja na riba ya asilimia mbili ya madai ya awali.
Ilidaiwa ATCL ilijibu kwa barua pepe Machi 30, 2008 ikieleza kwamba, haina uwezo wa kulipa deni hilo, ambalo lilikuwa limefikia dola za Marekani 418,305.
Kwa mujibu wa mlalamikaji, Machi 31, 2008, ATCL ilikubali deni hilo na kuahidi kulipa dola za Marekani 30,000 Juni 6, 2008 na dola za Marekani 5,000 kila wiki.
Ilidaiwa kwamba, kampuni hiyo ilikubali ombi la ATCL na kutaka riba ya asilimia 1.5 kila mwezi hadi malipo ya deni hilo yatakapomalizika.
Ilidaiwa kwamba ATCL haikuweza kutimiza ahadi yake na ndipo Juni 20, 2008 kampuni hizo zilipoiandikia tena barua pepe kudai malipo lakini ATCL haikuweza kulipa.