

Majirani wa jengo la ghorofa lililoporomoka eneo la Kijitonyama katika Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, wamelazimika kuyakimbia makazi yao kwa kuhofia jengo hilo kuporomoka zaidi.
Hatua hiyo imefuatia baada ya jengo hilo lenye ghorofa nne, kuegemea katika baadhi ya nyumba za jirani eneo hilo.
Akizungumza na NIPASHE, mmoja wa majirani na jengo hilo, Gospat Raphael, alisema inapofika usiku hawalali ndani na badala yake hulala nyumba ya wageni iliyopo karibu na eneo hilo.
Alisema wamefikia uamuzi huo baada ya sehemu kubwa ya ghorofa hilo kuegemea katika nyumba wanayoishi.
Alisema Manispaa waliwaahidi kufika kulimalizia kulidondosha ghorofa hilo lakini mpaka jana hawakufika, hivyo wanahofia ghorofa hilo linaweza kudondoka wakati wowote.
Alisema wakati wa mchana, hulazimika kushinda nje na wanapotaka kuingia ndani, hufanya hivyo kwa tahadhari kubwa kwa kuhofia usalama wa maisha yao.
Ghorofa hilo liliporomoka Jumapili iliyopita na kusababisha kifo cha mtoto na mtu mmoja kujeruhiwa.
Jengo hilo liliporomoka baada ya nguzo za jengo hilo kutitia.