Matokeo ya mtihani wa kidato cha nne ya mwaka 2012 yaliyotolewa na Baraza la Taifa la Mitihani (Necta) na kutangazwa juzi na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, yamedhihirisha kuwa kiwango cha elimu nchini kinazidi kuporomoka.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, asilimia 60 ya watahiniwa wamefeli. Wanafunzi waliofeli kwa maana ya kupata sifuri ni 240,903. Waliopata daraja la nne ni 103,227, waliopata daraja la tatu ni 15,426, waliopata daraja la pili ni 6,4,53 na waliopata daraja la kwanza ni 1,641.
Pamoja na kusema kuwa waliopata daraja la nne nao wamefaulu, huko ni kujidanganya kwa kuwa kiuhalisia kupata daraja la nne kwa miaka ya sasa ni sawa na kufeli kwa kuwa mhitimu wa aina hiyo ni nadra sana kupata nafasi ya ajira au nafasi ya masomo zaidi katika vyuo. Kimsingi, tunaweza kusema ukweli kwamba waliofeli ni daraja nne na daraja sifuri ambao jumla yao ni 344,230 kati ya 367,750, yaani asilimia 93.6 wamekwama.
Wadau kadhaa wametoa maoni yao kuhusiana na matokeo hayo mabaya hususan kwa upande wa shule za serikali wengi wao wakisema kuwa yamechangiwa na mfumo mbovu wa elimu nchini na kutowajali walimu kwa maana ya kuwapa maslahi mazuri. Wapo baadhi waliosema kuwa aibu hiyo imechangiwa na uhaba wa walimu na ukaguzi wa kina kutofanyika katika shule.
Wengine wamesema ni sababu ya mfumo mbovu wa elimu hususan mtaala ambao umesababisha elimu kuwa mahututi. Wakati wadau wa elimu wakibainisha sababu za wanafunzi wengi kufeli, akitangaza matokeo hayo, Dk. Kawambwa alitaja sababu ya kutofanya vizuri kwa shule nyingi hasa za vijijini kuwa ni kukosekana kabisa kwa walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati na upungufu wa walimu wa masomo mengine.
Aidha, alitaja sababu nyingine kuwa ni kukosekana kwa maabara kwa shule za mikondo ya sayansi na maktaba za kujisomea pamoja na upungufu mkubwa wa vitabu vya kiada na ziada katika baadhi ya shule.
Kadhalika, matokeo hayo yamebainisha kuwa shule za sekondari za serikali, zimefanya vibaya kwenye kundi la shule zenye watahiniwa 40 au zaidi, baada ya shule 18 kati ya 20 zilizofanya vizuri kuwa za binafsi.
Kwa ujumla, matokeo hayo yametuachia changamoto kubwa; kwamba sisi kama taifa tunapaswa kuketi chini na kujiuliza ni sababu zipi zimechangia hali hiyo na kupanga mikakati ya kukabiliana na aibu hiyo.
Hali inaonyesha kuwa serikali haiwezi kuendesha elimu peke yake hivyo ni jukumu la kila mmoja kuanzia watu binafsi, asasi na vyama vya siasa kutoa mchango wake kuokoa elimu yetu. Juzi, Dk. Kawambwa alitaja baadhi ya mikakati ya serikali katika kukabiliana na changamoto hizo kuwa ni kuajiri walimu kila mwaka ili kuondoa upungufu uliopo.
Mikakati mingine alisema ni ile ya kuboresha miundombimu iliyoko katika shule kwa kujenga nyumba za walimu, madarasa na maabara na kuendelea kutoa ruzuku ya Sh. 25,000 kwa kila mwanafunzi kwa mwaka, nusu yake ikitumika kununua vifaa vya kufundishia na kujifunzia. Aidha, alisema wizara itaendelea kuzishauri halmashauri kuweka mgawanyo mzuri wa walimu waliopo baina ya shule na shule na kuimarisha Idara ya Ukaguzi wa shule na kuwawezesha waratibu elimu kata na wakuu wa shule kufanya ukaguzi wa ndani katika shule za sekondari kwenye maeneo yao.
Hata hivyo, mwenendo mzima wa uendeshaji elimu nchini unaonyesha kuwa serikali imekuwa ikitamka mikakati ya kubiliana na changamoto hizo bila kuzitekeleza kwa kutoa kisingizio cha uhaba wa fedha.
Kwa mfano, mwaka juzi, idadi kubwa ya walimu waliopangiwa ajira katika halmashauri nchini walikutana na mateso baada ya kusota kwa miezi kadhaa bila kulipwa fedha za kujikimu, hali iliyosababisha wengi kuzikimbia ajira hizo.
Vilevile, mkakati wa kujenga nyumba za walimu katika maeneo ya vijijini sambamba na kuboresha mazingira ya shule hususan za kata umeshindikana kwa muda mrefu, hali inayosababisha walimu wengi wanaopangiwa ajira katika maeneo hayo kutokwenda ama kwenda na baadaye kuzikimbia ajira hizo.
Hatuna budi kukubali kwamba elimu yetu ni mahututi na inahitaji tiba ya kudumu, hivyo kila mmoja ajipange kwa kutoa mchango wake ili tuzikabili changamoto hizo ambazo zinatuathiri wote bila kujali itikadi za kisiasa.
Kwa matukio yalitokea kwenye Mkutano wa Bunge wa hivi karibuni, kwa serikali kukwepa kuwajibika kuhusiana na mwenendo mzima wa sekta ya elimu na kujificha katika kichaka cha kutaka iachwe ijisafishe yenyewe ikisaidiwa na wabunge wa chama tawala kuwa sehemu ya kuficha udhaifu huo, matokeo haya yanaifichua na kutaka hatua za haraka kukomboa elimu ya taifa hili. Kinachotakiwa sasa ni uwajibikaji wa kweli na si ghiliba za kisiasa za kuwepa wajibu. Uwajibikaji huu wafaa uanze na uongozi wa juu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kama kweli tunataka kutoka katika mkwamo huu.