Rais wa TFF, Leodegar Tenga (kulia) akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura.
Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) limeliamuru Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutofanya mkutano mkuu wa uchaguzi uliokuwa umepangwa kufanyika jijini Dar es Salaam Februari 24 kutokana na mkanganyiko uliojitokeza katika mchakato wa uchaguzi huo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za TFF zilizopo Karume jijini Dar es Salaam jana, Rais wa TFF, Leodegar Tenga alisema FIFA imetuma barua ikiagiza mchakato wa uchaguzi usimame baada ya kupata malalamiko kutoka kwa baadhi ya watu wanaotaka haki itendeke.
Tenga, ambaye anamaliza muda wake wa urais katika shirikisho hilo, alisema kutokana na mkanganyiko huo, FIFA katika barua yake ya jana iliyosainiwa na Kaimu Katibu Mkuu wa FIFA, Markus Kattner, imeagiza mkutano huo uahirishwe hadi hapo itakapotuma ujumbe wake nchini katikati ya mwezi ujao kufanya tathimini ya hali iliyotokea na kutuma ripoti yake katika shirikisho hilo na baadaye kutoa mwongozo wa nini kifanyike.
“Nia yetu ni kuona haki inatendeka na ionekane ikitendeka, na nia ya FIFA ni kutafuta ukweli. Hivyo wahusika (wagombea walioenguliwa) wajiandae, watumie wakati huu kuandaa hoja zao ili FIFA wakifika wawasikilize, wapate maelezo ya kina kuhusu utaratibu na malalamiko yaliyotolewa,” alisema Tenga.
"Kamati ya rufaa ya uchaguzi ya TFF wamemaliza kazi yao. Wametutaarifu kwamba hawawezi kupitia upya maamuzi yao, wako sahihi kwavile hayo ni masuala ya kisheria. Sasa tuwaachie FIFA wafanye kazi yao," aliongeza.
Tenga, ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), aliwaomba radhi wajumbe wa mkutano mkuu wa TFF kwa usumbufu uliojitokeza kutokana na uamuzi huo wa FIFA, hivyo hakutakuwa tena na mkutano huo Jumapili mpaka hapo watakapotaarifiwa baadaye.
Juzi kamati ya rufaa ya uchaguzi ya TFF inayoongozwa na mwenyekiti Idd Mtiginjola ilituma maombi ya kupitia upya maamuzi ya rufaa iliyoyatoa, maombi yaliyowasilishwa na waombaji uongozi watano kwa vile hakuna kipengele chochote kwenye katiba ya TFF na kanuni za uchaguzi kinachotoa fursa hiyo kama ilivyodaiwa na Tenga.
Waombaji hao walikuwa Jamal Malinzi aliyeenguliwa kugombea urais wa TFF na Hamad Yahya aliyeondolewa kwenye kinyang’anyiro cha uenyekiti wa bodi ya ligi kuu (TPL).
Wengine walioomba kuwania ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF na Kanda zao kwenye mabano ni Eliud Peter Mvella (Iringa na Mbeya), Farid Salim Nahdi (Morogoro na Pwani) na Mbasha Matutu (Shinyanga na Simiyu).
BMT
Katika hatua nyingine, wajumbe wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT) walikutana jijini Dar es Salaam jana kujadili suala waliloagizwa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuhusu madai ya Michael Wambura kwamba katiba ya sasa ya TFF ni batili.
Msemaji wa baraza hilo Maulid Kitenge aliwaambia waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa kikao kuwa tayari baraza hilo limeshatoa mapendekezo ya nini kifanyike kuhusu madai hayo ya Wambura na yatatangazwa baadaye na wizara hiyo.
"Sisi kama baraza tumemaliza kazi yetu tuliyoagizwa na wizara kuhusu katiba mpya ya TFF iliyozua mjadala. Tayari mapendekezo yetu yametoka, lakini waziri ndiye atakayetangaza," alisema Kitenge.
Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla aliiambia NIPASHE jana jioni kuwa ameshapokea mapendekezo ya BMT na kwamba atayawasilisha kwa waziri mwenye dhamana, Dk Fenella Mukangara, ambaye atatoa tamko kuhusu suala hilo.
Wiki iliyopita Wambura ambaye aliwahi kuwa katibu mkuu wa kilichokuwa Chama cha Soka Tanzania (FAT sasa TFF) aliibuka na kudai kuwa katiba ya sasa ya TFF ni batili na msajili aliisajili kimamkosa kwa vile haikuzingatia taratibu.