Wednesday May 22, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Simba vitani Mbeya, Azam Chamazi

20th February 2013
Print
Nahodha wa Simba, Juma Kaseja

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Simba ya Dar es Salaam leo wanashuka dimbani kucheza mechi ya ligi hiyo dhidi ya wenyeji wao Prisons kwenye uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini hapa.

Simba iliwasili jijini hapa juzi na kuweka kambi katika mji wa Mbalinzi kilomita 21 kutoka mjini Mbeya wakati wenyeji wao Prisons waliweka kambi Tukuyu ambapo jana jioni ndiyo walirejea mjini hapa.

Wekundu hao waliendelea "kuwaficha" wachezaji wao huko huko Mbalinzi na jioni walifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari Iyunga.

Simba leo itamkosa beki wake tegemeo, Shomary Kapombe, aliyeachwa Dar es Salaam kutokana na kuumia misuli wakati timu hiyo ikiikabili Recreativo de Libolo ya Angola katika mechi ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika.

Katika mechi zake mbili zilizopita, Simba iliambulia pointi mbili tu kati ya sita ilizokuwa ikizipigania baada ya kutoka sare dhidi ya JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kisha 1-1 ugenini dhidi ya Oljoro JKT.

Hiyo itakuwa mechi ya nne kwa Mfaransa Patrick Liewig tangu aanze kuinoa Simba ambapo ameshinda moja tu (3-1) dhidi ya African Lyon inayoshika mkia kwenye ligi hiyo.

Kocha msaidizi wa Simba, Jamhuri Kihwelu 'Julio' aliliambia gazeti hili jana kuwa wachezaji wote waliokuja Mbeya wako vizuri na wamepata muda wa kupumzika ili kujiandaa na mchezo huo muhimu kwao.

"Wachezaji wako vizuri na kila mmoja anataka ushindi ili kurejesha amani ndani ya timu na klabu yetu," alisema mchezaji huyo wa zamani na kocha wa timu ya taifa ya vijana (Serengeti Boys).

Nahodha wa Simba, Juma Kaseja, alisema jana kuwa wachezaji wamejiandaa kuikabili Prisons na wanataka ushindi ili kurejesha heshima yao.

"Tulifika salama na tuko vizuri, kilichobaki sasa ni kuomba tupate ushindi," alisema Kaseja kwa kifupi.

Kocha wa Prisons, Jumanne Chale, alisema jana kuwa vijana wake wako imara na wanaamini watapata matokeo mazuri kwenye uwanja wao wa nyumbani.

Chale alisema kwamba wanafahamu Simba inataka ushindi baada ya kupata sare mfululizo na kupoteza mchezo wao wa kimataifa Jumapili hivyo hasira zitahamia kwao na wamejiandaa kupambana na ushindani.

Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Emmanuel Gabriel, leo anatarajiwa kuongoza mashambulizi kwa upande wa Prisons.

Prisons inaingia uwanjani leo ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya African Lyon katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja huo huo Februari 9 mwaka huu.

Hekaheka nyingine itakuwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 25,000 utakapokuwa mwenyeji wa mechi kati ya Toto Africans na African Lyon. Wakati Lyon ikikamata mkia, Toto Africans yenye pointi 14 inashika nafasi ya 12 katika ligi hiyo inayoshirikisha timu 14.

Mwamuzi Simon Mberwa wa Pwani atakuwa shuhuda wa mechi kati ya Coastal Union ya Tanga na Oljoro JKT ya Arusha itakayofanyika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. Mechi hiyo inatarajiwa kuwa na upinzani mkubwa kutokana na uimara wa timu zote mbili.

Nayo JKT Ruvu ambayo haijafanya vizuri msimu huu kulinganisha na minne iliyopita itacheza na Azam kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, Dar es Salaam. JKT Ruvu chini ya kocha Charles Kilinda inakamata nafasi ya nne kutoka chini ikiwa na pointi 16 baada ya kucheza mechi 15.

Iwapo itafanikiwa kushinda mechi hiyo, Azam itaendelea kujiimarisha katika nafasi ya pili nyuma ya vinara Yanga. Azam ambayo ni moja ya timu zenye safu kali ya ushambuliaji katika ligi hiyo ikiwa imefunga mabao 27 ina pointi 33.

Vinara wa ligi, Yanga watashuka dimbani Jumamosi kuikaribisha Azam wakati Simba itacheza tena Jumapili dhidi ya Mtibwa Sugar ya Manungu, Morogoro.

SOURCE: NIPASHE