


Taasisi ya Utafiti na Udhibiti wa Viuatilifu (TPRI) yenye makao makuu yake jijini Arusha, imeyafungia maduka matano ya pembejeo kwa kosa la kuuza dawa za kuulia wadudu bandia kwenye mashamba ya kahawa katika Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma.
Hatua hiyo imekuja baada ya TPRI kufanya ukaguzi katika baadhi ya maduka yanayouza pembejeo za kilimo mkoani Ruvuma.
Msajili wa Viuatilifu nchini kutoka TPRI, Dk. Bakari Kaoneka, alisema walifanya ukaguzi kwenye baadhi ya maduka ya pembejeo yaliyoko mjini Mbinga na kukuta dawa nyingi aina za Dursban 4E na Basophate 482 SL bandia. Dk. Kaoneka alisema dawa hizo bandia
zimesababisha madhara makubwa ya kiuchumi na kiafya. Alisema wakulima wa zao la kahawa wamekuwa wakipoteza kiasi kikubwa cha mavuno hasa ikizingatiwa kuwa zao hilo haliwezi kuwa bora bila kutumia kiuatilifu kwa kuua wadudu mashambani mwao.
Dk. Kaoneka alieleza kuwa juhudi za serikali za kupunguza umaskini zinahujumiwa na baadhi ya wafanyabiashara ambao si waaminifu kwani wamekuwa wakiwauzia wakulima dawa bandia.
Alisema TPRI imefanya ukaguzi na kukamata viuatilifu vingi bandia na kulazimika kuyafunga maduka yaliyokutwa yakiuza dawa hizo. Aidha, alisema TPRI pia ilifanya ukaguzi na kubaini viuatilifu bandia katika mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Lindi, Mtwara, Dar es Salaam, Mbeya, Rukwa.
Aliwaasa wakulima wa zao la kahawa kuwa makini wanapokwenda kwenye maduka ya pembejeo kununua viuatilifu ambavyo vingi vimeonekana kuwa ni bandia.
Alisema dawa halisi inayoua wadudu katika mashamba ya kahawa lazima iwe na namba ya usajili ambayo inaanza na IN na kufuatiwa na tarakimu. Aliwataka maafisa ugani wa vijiji kuwa karibu na wakulima wa zao la kahawa kwa kuwapa ushauri.