Wednesday May 22, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Tusipoziba ufa Zanzibar, tutajenga ukuta

20th February 2013
Print

Matukio yenye taswira ya kuwepo hujuma dhidi ya viongozi wa dini yanazidi kuibuka na kuligubika eneo la visiwa vya Zanzibar, vile vinavyosika kwa ustaarabu, ingawa sasa hali inaonekana kutokuwa hivyo.

Novemba mwaka jana, Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Suleiman Soraga, alimwagiwa kimiminika kilichosadikiwa kuwa tindikali, akadhurika.

Taribani mwezi mmoja baadaye, Padri Ambrose Mkenda wa Kanisa Katoliki la Mpendae, alipigiwa risasi na ‘watu wasiojulikana’, akaumizwa na kuugua majeraha!

Juzi, damu ya Padri Evaristus Mushi ikamwagika baada ya kupigwa risasi na ‘watu wasiojuliaka’, mwili wake ukaanguka chini na sasa amelala katika kusingizi wa milele; ameuawa.

Matukio hayo na mengine yanayoweza kutokea visiwani humo, hayatoi taswira njema kwa nchi, lakini zaidi kwa visiwa hivyo na wakaazi wake.

Ni matukio yanayotoa ishara mbalimbali zenye ukweli na nyingine zikiwa hisia, lakini yote kwa ujumla wake yana athari hasi kwa jamii.

Yapo matukio mengine yaliyowahi kutokea visiwani Zanzibar, yakisababisha vifo vya raia wasiokuwa na hatia kama ilivyotokea kwa Padri Mushi-Mwenyezi Mungu ampumzishe katika usingizi wa amani-Amina

Matukio ya aina hiyo yamepigiwa kelele, yamekosolewa, yamelaaniwa. Kada tofauti zimehoji namna watawala kupitia vyombo vya ulinzi na usalama, walivyoshindwa kuidhibiti hali hiyo.

Ikumbukwe kwamba, Wazanzibar wamekuwa waathirika, japo kwa namna tofauti, na matukio ya mauaji.

Kizazi cha Zanzibar ‘kinarithishwa’ fikra hasi ya kuyaona mauaji kama sehemu ya kawaida katika maisha yao.

Kwamba kupitia harakati za siasa, wapo waliouawa ‘kimzaha’, wakapoteza maisha na kuwaacha mke, mume, watoto, ndugu, jamaa na marafiki.

Hata hivyo, hatua za maridhiano ya kisiasa zilipofanyika na kuwezesha kundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa, mauaji yanayotokana na siasa yamepungua. Hatujui baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015, hali itakuwaje!

Hata hivyo, ipo haja ya kuhoji, ni kwa namna gani hujuma na mauaji dhidi ya viongozi wa dini, yanashindwa kudhibitiwa, badala yake mamlaka husika zinabaki ‘kuwalilia’, kuwapa pole waathirika, huku zikitangaza kufanyika kwa ‘uchungizi wa kina’?

Ina maana taifa limeshindwa kubaini kiini cha matukio hayo ili kuyashughulikia, ikibidi kuyapatia suluhu ya kudumu? Tunabaki kulia, kulalamika na kulaani tu!

Mauaji kama yaliyotokea kwa Padri Mushi, yanaweza kuhusishwa na masuala ya kidini, kisiasa ama kijamii. Lakini iwe iwavyo, hayataishia katika hayo tu.

Mauaji ya aina yoyote ni dhambi, ile ambayo ikiingia ndani ya damu za watu wa jamii fulani, wakaiishi dhambi hiyo dhidi ya wenzao, haiwezi ikaishia hapo.

Jamii ‘inayopuuzia’ mauaji na kuyaona ya kawaida, kwa sababu, pamoja na mambo mengine, aliyeguswa ‘si mwenzatu’…inapotea.

Kwa maana jambo la msingi katima dhambi ya mauaji si aliyeuawa, bali tendo lenyewe. Kwamba dhambi hiyo ‘inapokomaa’, wakawaua ‘wale’ huku wajiona ‘wao’ wapo salama, wanadanganyika.

Wanaweza kuwaua ‘wale’ hata kuwamaliza katika hesabu yao, lakini itakapofikia ukomo ama kabla ya kufika hapo, wataanza kuuana ‘wao kwa wao’.

Kwa maana litakuwa jambo la kawaida, kwamba kwa vile ‘wao’ hawatakuwepo, na dhambi ya maujai inaishi ndani yao, atamuelekea mjomba, shangazi, kaka, dada, jirani…hali itakuwa mbaya zaidi zaidi.

Kwa maana hiyo, jambo la msingi kuhusu matukio ya mauaji na uhalifu mwingine wa kibinadamu unaoendelea kushamiri visiwani Zanzibar, ni kukabiliana na dhambi hiyo.

Kamwe haiwezi kuishia katika kummwagia tindikali Katibu wa Kadhi, kuwapiga risasi mapadri Wakatoliki ama mwingine awaye yote, itaendelea mbele zaidi. Ndivyo historia na mapokea ya uhalifu inavyopaswa.

Dhambi hiyo itakabiliwa kwa kila kada kuchukua nafasi na wajibu wake. Kuomba na kusali, kuimarisha ulinzi na usalama na kukiepusha kizazi cha sasa kishiriki kwa namna yoyote katika uovu huo.

Kwa maana kama mzazi ama mlezi, atashawishi, kushinikiza ama kushiriki kwa namna na hatua yoyote itakayofanikisha utekelezaji wa kuwashambulia na kuwaua viongozi wa dini, atakuwa anaichafua nchi na watu wake.

Ni lazima mamlaka husika zichukue tahadhali kuziba nyufa zinazoonekana sasa. Nyufa ambazo kama zikaachwa zikue, ziongezeke na kuweka ‘mizizi’ yake, basi athari zake zitakuwa kubwa kuliko hivi sasa.

Hilo linaweza kufanyika kwa namna tofauti kwa kadri ya maadili, mafundisho na wajibu wa kila kada, lakini je, watawala wenye dhamana ya kuhakikisha ulinzi na usalama vinadumu miongoni mwa umma, wanafanya nini?

Kwa nini asitokee miongoni mwa wenye dhamana, akajizulu kutokana na kushindwa kudhibiti vitendo hivyo, ili atakayefuata, aiepuke njia ya mtangulizi wake kwa kushiriki kikamilifu kuidhibiti hali hiyo.

Mashaka Mgeta ni Mhariri wa Makala. Anapatikana kupitia simu namba +255 754 691540 ama barua pepe: mgeta2000@yahoo.com.

 

SOURCE: NIPASHE