


Spika wa Bunge, Anne Makinda amekuwa akilalamikiwa na baadhi ya wabunge hasa wa vyama vya upinzani kuhusu utendaji wake anapoendesha vikao wengine wakisema kuwa anawapendelea zaidi wabunge wa chama chake na serikali.
Mwandishi Wetu amezungumza na Mbunge wa Muhambwe (NCCR Mageuzi), Felix Mkosamali, ambaye anaelezea mambo mbalimbali kuhusu kanuni za Bunge na namna ambavyo zimempa madaraka makubwa Spika.
Mkosamali anaanza kwa kukosoa uwezo wa Spika kwamba anashindwa kulimudu Bunge na amekuwa akiliendesha mithili ya lile la wakati ule wa chama kimoja hali ambayo imekuwa ikizua mtafaruku mara kwa mara kwa wabunge wanaoona hawatendewi haki.
Anasema si kweli kwamba kuna wabunge ambao ni wakorofi bungeni ila wabunge hao wamekuwa wakisimama kidete kudai haki yao wanapoona Spika ama Naibu Spika anatumia vibaya madaraka yake kwa kutaka kuikingia kifua serikali na wabunge wa chama chake.
Anasema kuna miongozo na taarifa nyingi zilizowahi kutolewa na wabunge lakini Spika kwa kutumia madaraka yake amezikalia kwa muda mrefu kwasababu kanuni hazisemi asipotoa majibu ya taarifa iliyoombwa na mbunge ama mwongozo anafanywa nini.
“Kanuni inasema baada ya Mbunge kuomba mwongozo Spika anaweza kujibu hapo hapo au baadae, sasa tafsiri ya baadae ni ipi? Lazima kanuni iseme ndani ya muda flani Spika lazima awe ametoa majibu ya mwongozo na asipofanya hivyo nini kinafuata, utaratibu wa sasa unampa Spika mwanya wa kukalia miongozo na taarifa za wabunge miaka na miaka,” anasema.
“Kuna wabunge wengi wanalalamika kuhusu maamuzi ya Spika kuchelewa kwa mambo waliyoyaombea mwongozo, kwa kuwa yeye Spika anajua hakuna hatua za kuchukuliwa dhidi yake ndiyo maana anayaweka kabatini na yanakaa miaka na miaka,” anasema.
Anasema kwa utaratibu wa sasa Spika ndiye mwamuzi wa mwisho katika mambo yote jambo ambalo lazima lipitiwe upya kuhakikisha mambo yanakwenda sawa.
Mkosamali anasema mbunge asiporidhika na maamuzi ya Spika anapaswa kukata rufaa kwenye kamati ya kanuni ambayo mwenyekiti wake ndiye mtuhumiwa (Spika) jambo ambalo limekaa vibaya.
Mbunge huyo anasema kwa kuwa Spika ndiye mwenyekiti wa kamati hiyo ndiye mwenye mamlaka ya kuitisha vikao kujadili masuala mbalimbali yanayolalamikiwa na wabunge dhidi yake.
Anasema kwa kuwa yeye amekuwa mlalamikiwa mara kadhaa anaweza kutumia mamlaka yake vibaya kwa kutoitisha vikao vya kamati hiyo hali inayozidi kukandamiza demokarasia bungeni.
“Sasa inakuwaje mlalamikiwa ndiye aitishe kikao cha kumjadili yeye? Ndiyo maana rufaa nyingi zimewekwa kabatini maana mlalamikiwa ndiye mwenye mamlaka ya kuitisha vikao vya kumjadili mwenyewe hapo haijakaa sawa sawa lazima tubadili kanuni,” anasema.
Anasema kunapokuwa na jambo linalalamikiwa dhidi ya Spika, yeye anaweza kuitisha kikao lakini kikaendeshwa na Naibu wake ili kusiwe na mgongano wa kimaslahi lakini cha kushangaza huwa hafanyi hivyo.
“Mimi binafsi kuna wakati mbunge mwenzangu alisema kuna wabunge wanakula rushwa nikasimama nikaomba Bunge lisiliache juu juu suala hilo na badala yake tulijadili kwa mapana lakini Spika alisema atatoa mwongozo hadi leo ni mwaka sasa hajafanya hivyo,” anasema.
Anasema Spika na wasaidizi wake wamekuwa wakipindisha kanuni wakati fulani kwa lengo la kuzima hoja za msingi za wapinzani na kuibeba serikali hali inayozusha malumbano na kile wanachoita fujo bungeni.
“Bunge lina kanuni lakini wakati mwingine hazifuatwi, unakuta mbunge huyu anaomba jambo kwa kutumia kanuni fulani lakini ananyimwa nafasi lakini kesho mbunge mwingine anaomba jambo fulani kwa kutumia kanuni ile ile uliyotumia wewe anapata nafasi, sasa hapo lazima kuwe na malalamiko ya wabunge wanaoona hawatendewi haki,” anasema Mkosamali ambaye ni Mbunge mdogo kuliko wote.
“Unajua maamuzi ya Spika ni kama ya mahakama, maana Spika ajaye anaweza kutoa maamuzi kwa kutumia maamuzi yaliyowahi kufanywa na Spika aliyepita, sasa ni jambo la kushangaza kama Spika huyu huyu leo anatafsiri kanuni flani hivi kesho kanuni hiyo hiyo anaitafsiri vingine,” anasema
Mkosamali anashauri Spika ajaye asitokane na chama chochote cha siasa ili aweze kutenda haki wakati wa kuendesha vikao tofauti na sasa ambapo lazima watoke kwenye vyama vya siasa.
Anasema kuna baadhi ya nchi ambazo zimeweka utaratibu kama huo ambapo Spika anachaguliwa nje ya vyama vya siasa na wamekuwa wakifanya vizuri zaidi katika kusimamia na kuendesha mabunge yao.
Anasema hata wasaidizi wa Spika ambao ni wenyeviti wa Bunge lazima uwekwe utaratibu ambao utawezesha kupatikana kupitia vyama vingine vya siasa na isiwe lazima CCM tu.
Mkosamali anasema wenyeviti wa Bunge nao wamekuwa sehemu ya chanzo cha zogo bungeni kutokana na tabia yao ya kupendelea wabunge wenzao wa CCM na serikali.
“Zile vurugu ambazo watu wanaona bungeni ni matokeo ya kutosimamia vizuri kanuni, watu wanapenda vyama zaidi kuliko nchi yao na ndiyo sababu hata mbunge wa upinzani akizungumza mambo ya msingi na yenye maslahi kwa taifa yanaweza kutupwa kwasababu tu amezungumza mpinzani,” anasema
Kuhusu mpango wa kutoonyesha moja kwa moja mikutano ya Bunge, Mkosamali anasema ni kinyume na sheria za nchi na ni kuwanyima haki ya msingi wananchi ambao wana haki ya kupata habari.
Anasema kuhariri mikutano ya Bunge na kisha kuonyesha baadae hakutakuwa na tija kwani wahusika lazima watakuwa wanatoa upendeleo kwa serikali na wabunge wa chama tawala.
“Nani atapima uadirifu wa mhariri wa vile vipindi, maana kuna uhakika kabisa kwamba wahusika wa uhariri hawataweka usawa tofauti na kuonyesha moja kwa moja ambapo hakuna ubaguzi maana kila anayezungumza anaonyeshwa hapo hapo,” anasema
“Hivi ni nani atakaye hariri vipindi na kuona jambo muhimu na lisilo la muhimu, maana wewe unaweza kuona jambo fulani ni muhimu kwako lakini kwa mtu mwingine akaona si muhimu kwake,” anasema
Anasema kutoonyesha moja kwa moja kutaharibu ufanisi wa Bunge kwani wabunge watakuwa wanahudhuria vikao wanapojisikia kwa kujua kuwa hakuna anayewatazama.
Mkosamali anasema hata mawaziri wanaweza kuwa wanaleta bungeni majibu ya ovyo ovyo kwa kuwa wanajua hakuna anayewaangalia.
Anashauri Bunge liachane na mpango huo maana hautakuwa na tija kwa wananchi ambao wana haki ya kujua sheria zinavyopitishwa na bajeti ya serikali.
“Hii inaweza kuwa ajenda ya CCM baada ya kuona wabunge wa upinzani wanaibua hoja nzito na kupata umaarufu kupitia Bunge, sasa kwenye mpango huu wanataka wawe wanakata mambo yote ya msingi yanayozungumzwa na wapinzani,” anasema
Miongozi taarifa zilizowekwa kabatini
Spika amekuwa na kawaida ya kukalia taarifa na miongozo na hata mkutano wa Kumi wa Bunge uliomalizika wiki iliyopita ulianza kukiwa na ‘viporo’ vya hoja, miongozo na taarifa mbalimbali za wabunge ambazo ziliibuka tangu Bunge la Kumi lilipossanza mwaka 2011.
Baadhi ya viporo hivyo kile cha Februari 10, 2011 cha mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, alipotakiwa na Spika kuwasilisha ushahidi wa kauli yake aliyosema kwamba mbunge anaweza kuchukua hatua gani ikiwa atabaini kiongozi mkuu wa serikali amelidanganya Bunge.
Lema aliwahi kusema kwamba Waziri MKuu, amelidanganya Bunge na alilazimishwa kuwasilisha ushihidi bungeni lakini miaka imekatika tangu awasilishe ushahidi wake na hakuna kilichozungumzwa.
Kiporo kingine ni kile cha Juni 19, mwaka jana baada ya mbunge wa Meatu (Chadema), Meshack Opulukwa, kumlipua Mkuu wa Wilaya ya Momba, Abihudi Saideya, bungeni kuwa yeye na Mkuu wa Polisi wa wilaya hiyo walihongwa gari la kifahari aina ya Toyota Land Cruiser GX na mwekezaji wa Kampuni ya Mwiba Holding ili awahamishe wananchi wa kijiji cha Makao kwenye eneo la hifadhi tengefu (WMA).
Opolukwa alitoa madai hayo bungeni alipokuwa akiuliza swali la nyongeza kwa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Alidai kuwa, Saideya, alipokuwa Mkuu wa Wilaya ya Meatu, alihongwa gari hilo aina ya GX lenye namba za usajili T 147 ASX na kampuni hiyo ili awaondoe wananchi katika eneo hilo.
Mara baada ya kumaliza kuuliza swali hilo, alisimama Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, na kuomba mwongozo wa Spika.
Lukuvi alisema kwa mujibu wa kanuni za Bunge, Mbunge haruhusiwi kumzungumzia bungeni mtu ambaye hawezi kujitetea ndani ya Bunge.
Alitaka Mbunge huyo kupeleka vielelezo na ushahidi wa tuhuma hizo kwa sababu serikali haiwezi kumvumilia mkuu wa wilaya anayehongwa.
Katika uamuzi wake, Naibu Spika, Job Ndugai alimpa siku saba Opulukwa kuwasilisha vielelezo vinavyothibitisha kuwa Mkuu wa Wilaya huyo na mkuu wa polisi a wilaya walihongwa gari.
“Mheshimiwa Opulukwa ameongea kwa uhakika mambo haya na ametaja jina la mtu, namuomba ama namtaka ndani ya siku saba alete vielelezo vinavyothibitisha jambo hilo kuwa wamehongwa gari,” alisema Ndugai.
Opulukwa alikiri kwamba anaoushahidi ambao aliuwasilisha mezani kwa spika lakini hadi leo hakuna taarifa zozote.
Jambo lingine ambalo halijapatiwa ufafanuzi kutoka mezani kwa spika ni lile la Julai mwaka jana la mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) na Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni kwa Wizara ya Katiba na Sheria, Tundu Lissu kutakiwa kuwasilisha vielelezo vya kuthibitisha kwamba Rais Jakaya Kikwete aliteua majaji wa Mahakama Kuu bila kushauriwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Lissu alitoa taarifa hiyo alipokuwa akiwasilisha hotuba ya kambi hiyo alipokuwa akitoa maoni ya kambi ya Upinzani katika Wizara ya Katiba na Sheria.
Katika maoni hayo ya Upinzani, Lissu alisema madhara ya ukiukwaji huo wa Katiba katika uteuzi wa majaji wa Mahakama Kuu ni makubwa na yameanza kujitokeza wazi.
Madhara hayo kwa mujibu wa madai ya Lissu, ni uwepo wa majaji ambao kwa sababu ya kutofanyiwa usaili na Tume ya Utumishi wa Mahakama, hawana uwezo wa kuandika mwenendo wa mashauri na hukumu zinazosomeka kutokana na ama kutokuwa na uwezo na ujuzi wa sheria au kutokuwa na weledi wa lugha ya Kiingereza ambayo ndiyo lugha rasmi.