

Umati wamzika Padri Mushi, Pengo aongoza mazishi
Kauli ya Waziri yaamsha miguno, Askofu amsahihisha
Simanzi na vilio vilitanda katika misa ya kumuaga Padri Evaristus Gabriel Mushi (55) wa Kanisa Katoliki iliyofanyika katika kanisa la Minara Miwili mjini Zanzibar na kuhudhuriwa pamoja na watu wengine, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.
Umati wa wananchi wa Zanzibar walifurika katika mazishi hayo, wengi wakiangua vilio kwa uchungu wa kifo cha Padri Mushi aliyeuawa kikatili kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana Jumapili iliyopita mjini Zanzibar.
Watu hao walianza kukusanyika majira ya asubuhi katika Kanisa Katoliki la Minara Miwili eneo la Shangani na kufanya ibada ya kumuombea marehemu iliyoongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, huku maaskofu na mapadri wakiingia kanisani kwa maandamano kabla ya misa kuanza.
Misa hiyo ambayo ilichukua takribani saa tatu, ilitawaliwa na simanzi, majonzi na huzuni ndani na nje ya kanisa, baada ya waumini kuanza kutoa heshima zao za mwisho kwa marehemu kabla ya msafara kuelekea katika maziko katika makaburi ya mapadri eneo la Kitope Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Kutokana na wingi wa watu na magari, msafara huo uliongozwa na gari la polisi, magari yaliyokuwa na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) walioimarisha ulinzi katika maeneo ya kanisa na makaburini.
WAZIRI APATA WAKATI MGUMU
Akitoa salamu za Serikali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Aboud Mohamed, alisema serikali imepokea kwa huzuni kubwa kifo cha Padri Mushi na kwamba ina maumivu kama waliyonayo waumini na wananchi kutokana na mazingira ya kifo chenyewe.
Alisema marehemu Padri Mushi alikuwa ni kiongozi wa kiroho muadilifu, mpenda amani na umoja, akihubiri mambo hayo kila siku kwa manufaa ya waumini na taifa kwa ujumla. Alisema kuondoka kwake kumeacha pengo lisilozibika ingawa kazi hiyo ni ya Mungu isiyo na makosa.
Hata hivyo kauli ya kazi ya Mungu haina makosa ilizua manung’uniko kutoka kwa waumini ambao walioneka kuyapinga maneno hayo na kuingilia kati hotuba ya Waziri huyo huku wakisema “Padri Mushi amekatishwa maisha yake na magaidi na siyo kazi ya Mungu.”
Waumini wengine walisikika wakisema kuwa marehemu hakuugua, hakugongwa na gari au kuzama baharini, bali uhai wake ulikatishwa na watu wakatili ndiyo waliokula njama na kukatisha maisha yake kinyama.
ASKOFU SHAO
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar, Dk. Augustino Shao. aliunga mkono msimamo wa waumini wake na kusema kifo hicho siyo mapenzi ya Mungu, bali kimetokana na kukatishwa maisha yake na watu wenye nia mbaya kwa kanisa na maendeleo ya imani yao.
“Kifo chake hakikutokana na mapenzi ya Mungu...tusikubali na kukumbatia maovu, ingawa natoa shukrani za kanisa kwa viongozi wa serikali na watu wote walioungana nasi kuja kumpumzisha mwenzetu katika nyumba ya milele,” alisema Askofu Shao.
Msemaji wa wana familia ya mrehemu Padri Mushi, Francis Boniface Mushi, alisema wamepokea kifo cha ndugu yao kwa masikitiko makubwa kwa kuwa hakuugua na kulala kitandani, bali maisha yake yamedhulumiwa na kundi la wahalifu na kwamba wataendelea kumuombea.
ASKOFU HAFIDH
Naye Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Zanzibar, Michael Hafidh, alisema kanisa lake halina imani na Jeshi la Polisi wala Serikali kutokana na kushindwa kulinda haki za kikatiba za raia wake ikiwamo haki ya kuishi na kuabudu.
Askofu Hafidh, alisema Zanzibar imepoteza mwelekeo wa kujengeka amani kutokana na kuongezeka vitendo vya uhalifu jambo ambalo linatokana na viongozi kuzembea kwa utendaji wa serikali.
Alisema Jeshi la Polisi lina uwezo wa kukabiliana na uhalifu huo, lakini bado halijawa tayari kuwalinda na kuwakingia vifua watu wanaoendesha ukatili na kwamba kanisa lake limekataa ulinzi wa jeshi hilo.
DK. SLAA
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, alisema umefika wakati Watanzania wasikubali kuimba wimbo “bwana alitoa bwana aliumba” badala yake wadai haki na kuhakikisha haki ya kuishi inaheshimiwa kama ilivyoainishwa katika Katiba ya Tanzania.
Alisema viashiria vinavyojionyesha si mambo ya kupuuzia na kuchezea kama viongozi wa kiroho imefikia wakati wanashambuliwa na kuwaua na kuongeza kuwa ufike wakati serikali itafakari kwa kina na kuja na majibu ya kuondoa tatizo lililopo.
Alisema uamuzi wa Serikali kuleta askari na makachero wa Scotland Yard au FBI siyo ufumbuzi wa matatizo yanayojitokeza bali ni urasimu unaokwepa majukumu ya kupata suluhisho la kudumu. “Kuleta wachunguzi toka nje ni sawa na kuhangaika na matawi wakati shina na mizizi yake ikiwa imeliwa na mchwa na hatma yake ni kuanguka,” alisema.
JAMES MBATIA
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema viongozi ni lazima watekeleze kwa vitendo viapo vya kulinda katiba na kuhakikisha wanalinda uhai na maisha ya raia wanaowaongoza.
Mbatia alisema matatizo ya umwagaji wa damu yameanza kuwa mazoe nchini wakati vyombo vya ulinzi na usalama vikiendeshwa kwa gharama za walipa kodi huku vikishindwa kusimamia majukumu ya kazi zilizowapa ajira hiyo.
“Serikali isifanye kazi ya kutoa rambirambi kila mauaji yanapotokea baada ya kuwasaka na kuwakamata wahalifu ili kuwafikisha mbele ya sheria na kuwaadhibu, jambo hili linatia shaka,” alisema.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alisema mauaji ya Padri Mushi ni kitendo cha kigaidi na lazima Serikali kwa kutumia vyombo vyake vya dola ifanye kazi ya ziada ya kuwasaka na kuwakamata waliofanya unyama huo.
Baada ya maziko kumalizika, baadhi ya wananchi walisema kwamba maisha yao yamekuwa ya wasiwasi na kulazimika kufanya ibada katika mazingira ya wasiwasi kutokana na serikali kusindwa kuwalinda.
Yakude John anayeishi Bungi Miembe Mingi, alisema Zanzibar imebahatika kuwa na vikosi vya SMZ na vile vya Muungano na kuhoji kuwa wahalifu wanapata wapi nguvu ya ushindi huo wa kinyama bila ya kutiwa mbaroni na kuhukumiwa kwa mujibu wa sheria.
Viongozi wa kiroho waliohudhuria mazishi hayo mbali ya Pengo ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini (TEC), Askofu Taracius Ngalaku mtumwa; Mwakilishi wa Papa nchini, Askofu Francisco Padila; Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki la Tabora, Paul Ruzoka;
Askofu Damiani Dallu (Geita); na Askofu Renatus Mkande (Bunda); Askofu Gervas Nyaisonga (Dodoma); Askofu mstaafu Mkuu John Ramadhan wa Kanisa la Anglikana na viongozi mbalimbali wa makanisa kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Viongozi wa serikali ya Zanzibar na Serikali ya Muungano waliohudhuria ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad; Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Zanzibar (Utumishi na Utawala Bora), Haji Omar Kheri; Waziri Asiye na Wizara Maalum, Machano Othman Said; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini; Waziri wa Habari, Utamaduni,Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk na Naibu Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Issa Haji Usii Gavu.
Jumuiya ya kikristo Tanzania
Jumuiya ya kikristo Tanzania (CCT), imesema uhalifu unaoendelea nchini, yakiwamo mauaji ya viongozi wa kidini na uharibifu wa nyumba za ibada upo nyuma ya vikundi kadhaa vilivyopatiwa mafunzo maalumu nje ya nchi kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo.
Tamko hilo lilitolewa jana kwa waandishi wa habari na Askofu wa kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa, Dk. Owdenbug Mdegela.
Ingawa hakuvitaja moja kwa moja vikundi hivyo, Askofu Mdegela alisema kwamba vikundi hivyo vimepata mafunzo hayo na kwamba lengo ni kukamilisha mkakati huo.
Kufuatia hali hiyo, Mdegela aliwaandikia waraka, wanachama wote wa CCT kuanza mara moja mfungo wa saa 24 kuanzia jana (Maombi ya mnyororo), kusali dhidi ya uhalifu huo kwa minajili ya kuwasaidia makachero kutoka ndani na nje ya nchi kuwabaini wanaotekeleza mkakati huo.
IBADA YA KULIOMBEA TAIFA DAR
Mamia ya waumini wa Kanisa Katoliki Jiji la Dar es Salaam jana jioni walikusanyika katika Kanisa la Mtakatifu Joseph katika misa ya kumwombea Padri Mushi.
Misa hiyo iliyoongozwa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa, pia ilikuwa na lengo la kuiombea nchi amani kufuatia migogoro ya kidini inayoendelea.
Askofu Nzigilwa aliwataka waumini kusali rozali katika familia na kuhudhuria misa.
Askofu Nzigilwa aliwataka waumini hao kuwapenda maadui zao na kuwaombea kama maandiko ya Biblia yanavyoelekeza.
Misa hiyo pia ilihudhuriwa na Padri, Ambrose Mkenda, ambaye alipigwa risasi na kujeruhiwa vibaya na watu wasiojulikana Desemba mwaka jana mjini Zanzibar kisha kulazwa hadi wiki iliyopita aliporuhusiwa.