Kiungo aliye katika kiwango chake cha juu Amri Kiemba.
Simba ilipata ushindi wake wa kwanza katika mechi nne za michuano yote baada ya kuilaza Prisons kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine mjini Mbeya, huku Azam wakitoa kipigo kizito cha 4-0 dhidi ya JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
Kiungo aliye katika kiwango chake cha juu Amri Kiemba, aliifungia Simba goli lililoamua mechi kufuatia pasi ya Haruna Moshi 'Boban', lakini "bonanza la mabao" lilikuwa kwenye Uwanja wa Chamazi ambako Khamis Mcha alifunga magoli mawili (dk.2 na dk.46), John Bocco 'akatupia' moja (dk. 44) na Abdi Kassim 'Babi' akaongeza jingine katika dakika ya 72 akitumia mpira wake wa kwanza kuugusa baada ya kuingia uwanjani akitokea benchi kuchukua nafasi ya Bocco.
Lilikuwa ni goli la pili katika mechi ya pili mfululizo kwa Bocco, ambaye pia alifunga katika mechi yake ya kwanza dhidi ya Al Nasr ya Sudan Kusini waliyoshinda 3-1 katika Kombe la Shirikisho Jumamosi, akitokea kupona majeraha yaliyomuweka nje ya uwanja kwa muda mrefu.
Matokeo hayo yalimaanisha kwamba Azam imewafikia vinara Yanga (ambao wana mechi moja pungufu) kwa pointi 36 kileleni mwa msimamo kabla ya mechi baina yao itakayochezwa Jumamosi. Hata hivyo, Yanga inabaki kileleni kwa kuwa na tofauti bora ya magoli. Wakati Yanga imefunga magoli 32 na kufungwa 12, Azam imefunga magoli 31 na kufungwa 14.
Baada ya ushindi wa jana, Simba imeendelea kubaki katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 31 baada ya mechi 17, huku Coastal Union ya Tanga nayo ikijiimarisha katika nafasi ya nne kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya JKT Oljoro kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na hivyo kufikisha pointi 30 baada ya mechi 18.
Toto African iliondoka kwenye mstari wa kushuka daraja kwa kukwea nafasi moja juu hadi nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kufutia ushindi wa 2-0 dhidi ya timu inayoburuta mkia ya African Lyon yenye pointi 9. Toto sasa imefikisha pointi 17, moja nyuma ya Prisons iliyo katika nafasi ya 10 ya msimamo wa ligi hiyo ya timu 14.
Licha ya kipigo kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, ilikuwa ni Prisons iliyoishambulia zaidi Simba.
Jumanne Elfadhil alikaribia kuifungia timu yake ya Prisons goli la kusawazisha katika dakika ya 67 wakati shuti lake zuri lilipogonga mwamba na mpira kutua miguuni mwa kiungo Peter Michael, ambaye hata hivyo, alipaisha juu ya lango.
Elias Munguri alikuwa na nafasi ya mapema katika dakika ya 12 ya kuipa Prisons goli la kuongoza wakati alipobaki yeye na kipa wa Simba, Juma Kaseja, lakini alipiga pembeni.
Dakika tano baadaye, Munguri tena akiwa jirani na lango alipiga mpira nje wakati alikuwa ameshamtoka beki Juma Nyosso.
Katika dakika ya 29, Prisons walifanya shambulizi jingine la kustukiza kupitia kwa beki wao Aziz Sibo, lakini shuti lake lilishindwa kulenga lango.
Sino Augustino alikimbia vizuri ndani ya boksi kwenda kumuona Kaseja katika dakika ya 59, lakini kipa huyo nahodha wa timu ya Taifa, aliwahi kuudaka mpira uliokuwa jirani na Sino.
Munguri ambaye alikuwa tishio, alipiga tena pembeni shuti akiwa katika nafasi ya kufunga na kuikosesha timu yake goli la kusawazisha katika dakika ya 64.
Hadi katika dakika za lala salama, wenyeji walionekana kuwa wakali wakisaka goli la kusawazisha, jambo lililomfanya kocha Mfaransa Patrick Liewig kuwapumzisha Amri Kiemba (dk.70), Mrisho Ngassa (dk.77) na Amir Maftah (dk.86) na nafasi zao kuchukuliwa na Haruna Chanongo, Felix Sunzu na Kigi Makasi, mabadiliko ambayo yaliwasaidia Simba kushikilia ushindi wao wa kwanza katika mechi nne zilizopita.
Baada ya mechi kwenye uwanja wa Azam, kocha wa klabu hiyo, Muingereza Stewart Hall alisema anajivunia kikosi chake na kwamba hakutegemea kama kingecheza vizuri kiasi hicho licha ya kuwakosa nyota wake kadhaa.
Alisema kiwango hicho kimempa matumaini ya kufanya vizuri katika mechi yao ya Jumamosi dhidi ya Yanga.
Hall alisema Salum Aboubakar 'Sure Boy' hakucheza kwa sababu alikuwa akitumikia adhabu ya kadi, wakati mshambuliaji Brian Umony na Kipre Bolou walifeli vipimo vya uzima asubuhi ya jana.
Kocha wa Ruvu, Charles Kilinda alisema amekubali matokeo kwa sababu timu yake ilizidiwa.
Kama ilivyo kawaida, wachezaji 25 wa Azam waligawiwa hapo hapo bonasi ya Sh. milioni 3, ambazo hupewa kila wanaposhinda mechi. Kiasi hicho ni sawa na Sh. 120,000 kwa kila mchezaji.
Vikosi kwenye Uwanja wa Sokoine vilikuwa; Prisons: David Abdallah, Aziz Sibo, Laurian Mhalile, Jumanne Elfadhil, Sino Augustino, Freddy Chudu, Emmanuel Gabriel/ Jeremiah Juma (dk.54), Elias Manguri na John Matel.
Simba: Juma Kaseja, Nasor Masoud 'Chollo', Amir Maftah/ Kigi Makasi (dk.86), Komalbil Keita, Juma Nyosso, Abdallah Seseme, Mrisho Ngassa/ Haruna Chanongo (dk.77), Amri Kiemba/ Felix Sunzu (dk.70), Mwinyi Kazimoto, Haruna Moshi 'Boban' na Ramadhani Chombo 'Redondo'.