Friday May 24, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Azam waipasua kichwa Yanga

21st February 2013
Print
kocha Mholanzi wa timu ya Yanga, Ernest Brandts

Baadhi ya maafisa wa benchi la Ufundi la Yanga wakiongozwa na kocha wao Mholanzi, Ernst Brandts walikuwa ni miongoni mwa mashuhuda wakati Azam wakicheza soka safi na kushinda 4-0 dhidi ya JKT Ruvu katika mechi ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam jana.

Mbali na Brandts, maafisa wengine wa Yanga ambao wanaongoza ligi hiyo kwa tofauti ya mabao tu dhidi ya Azam iliyofikisha pointi 36 ni kocha msaidizi Fredy Felix Minziro na kocha wa makipa, Mkenya Razak Siwa.

Wanajangwani walilazimika ‘kuzamia’ mechi ya Chamazi jana ili kuisoma Azam kabla ya kuivaa katika mechi yao itakayochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambapo mshindi anatarajiwa kujiweka katika mazingira mazuri ya kufukuzia ubingwa wa ligi ya Bara msimu huu.

“Ninajivunia kikosi changu. Kiwango walichoonyesha leo (jana) kinanipa matumaini ya kufanya vizuri pia katika mechi yetu ijayo dhidi ya Yanga,” alisema jana kocha wa Azam,
raia wa England Stewart Hall ikiwa ni muda mfupi tu baada ya kumalizika kwa mechi yao dhidi ya JKT.

Azam ilitawala mechi nzima licha ya kutowatumia nyota wake kadhaa, wakiwamo Mganda Brian Umony, kiungo wa Taifa Stars, Salum Aboubakar ‘Sure Boy’, Mkenya Aturdo na mchezaji wa kimataifa kutoka Ivory Coast, Kipre Bolou.

“Sure Boy hakucheza kwa sababu ya kadi tatu za njano… wengine hawakucheza kwa sababu kimwili hawakuwa sawasawa wakati tulipowachunguza asubuhi… hata hivyo, nimeshangazwa na kiwango kizuri kilichoonyeshwa na kila mmoja leo (jana). Sikuamini kama wangecheza hivi na kutupatia ushindi huu mkubwa ,” alisema Hall.

KAMBI BAGAMOYO
Wakati Azam wakiendeleza kasi yao ya ushindi huku wakishuhudiwa na kina Brandts jana, vinara wa ligi hiyo, Yanga wanaonekana kuingiwa hofu na hivyo kuamua kujipanga zaidi kwa kupeleka kikosi chao Bagamoyo kuweka kambi maalum kabla ya kuteremka dimbani Jumamosi.

Hatua hiyo ni mwendelezo wa desturi yao iliyoibuka hivi karibuni ya kujichimbia kambini kila wanapokaribia kucheza dhidi ya Azam. Kabla ya hapo, ‘Wanajangwani’ walizoelekea kupiga kambi kwa mechi za ligi kujiandaa tu dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Simba.
 
Hata katika maandalizi ya mechi yao ya mzunguko wa kwanza wa ligi dhidi ya Azam simu huu, Yanga pia walikwenda kujichimbia Bagamoyo na mwishowe kuibuka na ushindi wa 2-0.
Kaimu Afisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto aliiambia NIPASHE jana kuwa kikosi cha timu yao chenye wachezaji 26 kilianza mazoezi jana asubuhi kwenye Uwanja wa Mbegani mjini Bagamoyo kujiandaa kwa mechi yao muhimu dhidi ya Azam.

Baada ya ushindi wa 4-0 dhidi ya JKT Ruvu, Azam sasa imefikisha pointi 36, sawa na vinara Yanga lakini wakizidiwa kwa tofauti ya mabao.

Yanga imeshinda mechi 11, kupata sare tatu na kupoteza mechi mbili huku ikiwa imefunga mabao 33 na kuruhusu wavu wake kutikiswa mara 12.
Azam wamebaki katika nafasi ya pili baada ya kufunga mabao 31 na kufungwa magoli 14.

SOURCE: NIPASHE