Saturday May 18, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Wanane mbaroni kwa kulipa mishahara hewa

4th July 2012
Print
Comments

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Kagera, imewatia mbaroni watumishi wanane kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma kwa njia ya kupitisha mishahara hewa.

Kati ya watuhumiwa hao, wawili ni watumishi katika ofisi ya mkuu wa mkoa wa Kagera na sita wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba.

Taarifa iliyotolewa na kuthibitishwa na Takukuru mkoani hapa ilieleza kuwa watuhumiwa hao tayari wamefikishwa mahakamani.

Kaimu Kamanda wa Takukuru mkoani Kagera, Samsoni Bishati, alisema watumishi hao wanakabiliwa na makosa ya kujihusisha na suala la kupitisha fedha ambazo ni mishahara ya watumishi hewa na kujinufaisha wenyewe.

Bishati alidai kuwa katika kupambana na rushwa inayofanywa na baadhi ya watumishi wa serikali wasio waaminifu, Takukuru mkoani Kagera imefanikiwa kuwakamata watumishi hao na baadhi yao tayari walifikishwa mahakamani jana.

Aliwataja waliofikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Bukoba kuwa ni Shabani Kitimbisi na Sifa Mussa wa Idara ya Fedha katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera.

Wengine ni Davidi Buhenyenge na Martin Muganyizi, wa Idara ya Afya katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa Bukoba.

Aidha, alisema watumishi wengine bado wanatafutwa na taasisi hiyo na hakuwataja majina yao.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment