Thursday May 5, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Waanzisha taasisi kutoa mikopo ya elimu ya juu

24th May 2012
Print
Comments

Taasisi ya Mfuko wa Elimu ya kuwasaidia wanafunzi wa Elimu ya Juu hapa nchini (HLSSF), imetangaza neema kwa  wanafunzi wanaohitaji msaada wa mikopo ya elimu ya juu kujiunga na taasisi hiyo ili waweze kupata fedha za masomo.

Akizungumza na NIPASHE jijini Dar es Salaam jana Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Respicius Kamuhabwa, alisema HLSSF imeanzishwa ili kutoa fursa kwa wanafunzi kupata mikopo yenye masharti nafuu.

Alisema kuwa maombi ya mkopo kwa mwaka wa masomo 2012/2013 yanapokelewa na maombi yatasitishwa Oktoba 30, mwaka huu na kwamba malengo ni kutoa mikopo kwa wanafunzi 1,000 katika kipindi hicho.

Alisema mkopo huo utamwezesha mwanafunzi kukidhi mahitaji kama karo, chakula, malazi, ununuzi wa vitabu na gharama za mafunzo kwa vitendo.

Alisema wanafunzi wanaohitaji kujiunga na vyuo vikuu ni wengi lakini upatikanaji wa mikopo kutoka Bodi ya mikopo Elimu ya juu (HESLB) ni mgumu kwa kuwa wengine hawaipati.

Kamuhabwa alisema taasisi hiyo ilipata usajili wake mwaka 2008 kupitia Wizara ya Maendeleo Jamii, Jinsia na Watoto.
“Itafikia wakati Serikali itashindwa kutoa mikopo kwa wanafunzi kutokana na idadi kuwa kubwa kama Watanzania tumeona ni vema kuanzisha taasisi hii, ili kupunguza usumbufu lakini pia kuipunguzia Serikali mzigo,” alisema Kamuhabwa.

Alisema taasisi hiyo itawasajili wanachama na kuunda Mfumo wa Bima ya Elimu kupitia HLSSF ili kusomesha wanafunzi wengi zaidi kwa miaka ijayo kadiri ya ongezeko la uhitaji.

Aidha mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya juu bado ni tatizo kwa kuwa Mei 17, mwaka huu wanafunzi wa vyuo vikuu vya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Elimu ya Biashara (CBE) na St. John’s tawi la Dar es Salaam walivamia Bodi ya mikopo ya Elimu ya juu (HESLB) kufuatilia mikopo yao.

Hata hivyo bodi hiyo kwa kupitia Mkurugenzi mtendaji wa bodi hiyo, George Nyatega alisema kuwa kwenye akaunti yake inayotumika kuwalipa mikopo wanafunzi inasoma ziro, kwa hiyo ilishindwa kuendelea na huduma.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles